BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 50

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... Kimsingi hiyo huwa siyo ndoto bali ni kweli, asubuhi ukiamka kitandani kwako huwa kuna mchanga mwingi. Pia katika shuka yako kuna.

Endelea..

Upande wa nje sehemu ya pembe ya kulia huwa kuna vidoa vyeusi vidogovidogo vingi. Kwa haraka haraka kama haujaambiwa maana ya vidoa hiyo ni vigumu kutambua kama ulikwenda kujenga uchawini.

Majengo yaliendelea kuota kama uyoga katika kambi hiyo, yalipandishwa haraka kulingana na idadi kubwa ya mafundi waliokuwa wakijenga kila siku usiku.

Ndugu msomaji, katika ulimwengu wa giza kuna mambo mengi sana ambayo huwa raia wa kawaida anafanyiwa. Mara nyingi wanaoonewa sana ni wale wanaosali, madawa mengi ya kichawi wao ndiyo hufanyiwa majaribio.

Majaribio hayo yanaweza kufanywa wakati wowote, inaweza kuwa mchana, jioni hata usiku kulingana na nafasi za wachawi wahusika.

Kumbuka wachawi huendesha shughuli zao kulingana na nguvu za madawa walioyonayo, wapo ambao hawafungwi na muda wao hufanya shughuli zao muda wowote iwe mchana, jioni au usiku.

Hapa nikuibie siri kidogo, kama wewe unapenda kutembea usiku jitahidi kufanya mambo yafuatayo ili usisumbuliwe na wachawi.

Ikiwezekana tembea ukiwa uchi wa mnyama, hapa kamwe hauwezi kukutana na changamoto za kichawi. Kwa ufafanuzi zaidi soma simulizi ya JICHO LA SHETANI MGONGONI MWA SHEKHE au MAINI YA MZUNGU MIKONO MWANGU zimefafania kiundani zaidi.

Kama utashindwa kutembea uchi wa mnyama basi hakikisha mavazi yako yote yavae kinyume na asili yake.

Mfano viatu ama malapa yageuze kushoto kulia, chupi, kaptula, suruali ama sketi vigeuze nje ndani. Upande wa nje uingie ndani kisha upande wa ndani wa nguo hiyo utoke nje.

Kama umevaa saa ipeleke upande wa kulia usiivae kushoto, kama utaweza zaidi tembea kwa kurudi nyuma unakoelekea, yaani badala ya kutanguliza tumbo basi mgongo ndio utangulie kule unakoelekea.

Hakuna mchawi ambaye anaweza kukuchezea wakati huo unapotembea usiku, hii ni kwa kuwa unakuwa umevunja mwiko wa nguvu za kichwani. Kwa ufafanuzi zaidi kasome simulizi ya VITA VYA MGANGA THE BOMBOM NA WACHAWI.

Kazi ya ujenzi wa GAMBOSHI MPYA ilikuwa imepamba moto, hakika ingekuwia vigumu kuamini kuwa ile ilikuwa ni kambi ya kichawi.

Ungebahatika kuyaona majengo hayo usingeamini, ingekuwia rahisi kusema ule ulikuwa ni mojawapo ya miji ya kisasa iliyojengwa na wajenzi huru wa kikatoliki.

Ama ungesema labda mji huo ni miongoni mwa miji maarufu katika simulizi ya Alfa lela Ulele. Mpangilio wake ulikuwa nadhifu na wa kuvutia, ramani ya mji huu iliandaliwa na mkuu wa giza na nilisafiri mwenyewe kuifuata makao makuu ya mkuu wetu kwenye mji wa Heaven.

Kila eneo la mji huo lilikuwa na kazi yake maalumu katika shughuli za kiuchawi. Kulikuwa na eneo ambalo ni makao makuu ya mchawi mkuu THE BOMBOM, kulikuwa na eneo la kukutana na mkuu wa giza anapotembea kambini kwetu.

Kulikuwa na sehemu ya kuhifadhi madawa yetu ya kichawi, sehemu hizi ziligawanyika kulingana na kazi ya madawa hayo.

Kulikuwa na eneo la ofisi za wachawi wasaidizi wangu pamoja na ofisi za wachawi wadogo zaidi kulingana na uwezo wao. Kulijengwa pia kumbi za mikutano yetu ya aina mbalimbali.

Majengo mengine yalijengwa maalumu kama sehemu ya kuandalia mafuta ya binadamu, hapa niseme kidogo eneo hili lilijengwa majiko maalumu kwa ajili ya kuchemsha miili ya binadamu hao.

Faida mojawapo ya mafuta hayo ni katika kurusha ungo na usafiri wa aina hiyo, hutumika pia kujipoteza endapo utanasa kwenye majumba ya watu waliozindika zaidi.

Mafuta mengine hutumika kuingia kwenye mabenki kwa ajili ya kuiba fedha, haya ni yale mafuta ya mjukuu wa msukule.

Mafuta haya ni ghali na hata wazungu huyatafuta sana kwa shughuli zao za kichawi na wizi. Tukiachana hilo mji huo ulikuwa na eneo la kuhifadhi usafiri wa kichawi, sehemu ya usafiri wa anga ilikuwa pekee. Sehemu ya usafiri wa wanyama ilikuwa kivyake na sehemu ya usafiri wa majini ilitengwa eneo lake.

Kulikuwa na eneo maalumu la kuchoma au kupikia nyama, eneo hilo lilikuwa maalumu kwa ajili ya nyama za binadamu au wanyama.

Moja ya vitu ambavyo wachawi tunapenda ni kula nyama, kwa kiasi kikubwa wachawi wengi tunapendelea nyama ya binadamu kulingana na utamu wake.

Yote haya ni kwa sababu ya maagano ya kichawi ambayo kwayo kila mchawi ameapa. Nyama nyingine inayopendelewa na wachawi ni ile ya ng'ombe, mbuzi, kondoo, mbwa, punda nk.

Katika mji huo kulikuwa na eneo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi misukule. Eneo hilo kiligawanywa katika maeneo kadha wa kadha, kulikuwa na sehemu ya vyumba vya misukule viongozi, misukule waliooana, misukule wasio na wenza, misukule wakorofi na misukule wageni.

Pia mji huo ulijengwa jengo maalumu kwa ajili ya BUNDI WA GAMBOSHI, bundi huyu alikuwa na umuhimu wa kipekee kuliko aina zote za usafiri. BUNDI WA GAMBOSHI ndiye aliyetumika kunipeleka THE BOMBOM makao makuu ya mkuu wa giza kwenye mji wa Heaven.

Kulikuwa na majengo maalumu kwa ajili ya wageni wa kuzimu, wageni wa Heaven na wageni wa duniani. Majengo hayo yalitofautiana hadhi kulingana na hadhi ya mgeni husika. Kwa kifupi mji huo ulikuwa umesheheni kila kitu kinachohitajika kama hudumu kwenye mji wowote ule wa kisasa.

Uzuri wa GAMBOSHI MPYA ilikuwa tofauti kabisa na ile GAMBOSHI iliyopo katikati ya Ramadi na Bariadi. Gamboshi hii ilikuwa kubwa na ya kisasa, ilijengwa ikajengeka huku ikiwa na barabara safi zilizounganishwa na barabara ya lami itokayo Kigoma kuelekea Tabora. Ndugu, msomaji ingekuwia ugumu kuiona kambi hiyo kwa macho ya kawaida labda uwe na macho matatu.

Wakati huo ilikuwa ni muda wa saa saba za usiku, kazi ilikuwa imepamba moto.Mafundi walikuwa wakipishana kwa utendaji kazi, fundi huyu akiwa anamalizia ukuta ule fundi mwingine anafanya kazi nyingine.

Wakati huo nilikuwa nimezungukwa na wasaidizi wangu wa kichawi tukiangalia maendeleo ya ujenzi. Mara nyingi sehemu kama hizo ni rahisi kunitofautisha na wachawi wengine kwa kuwa mie huwa nimevaa ngozi za binadamu.

Pia kiti changu huwa kimezungukwa na mifupa ya binadamu ila sehemu ya kukalia huwa kuna fuvu la binadamu.

Wakati huo sikuwa nimekali kiti hicho isipokuwa nilikuwa nimemkalia Shekhe mmoja wa jumuia ya Answali Suni kutoka msikiti wa All- Nuur.

Shekhe huyu anaitwa Nassoro ibn Mahamud, hufanya pia kazi ya kutibu watu mbalimbali kwa kutumia kitabu.

Kupitia kazi yake alikuwa kikwazo kwa kazi zetu, maana kuna muda alivuka mipaka ya kazi yake akaingia upande wetu.

Tulitumia gepu hilo kumshikisha adabu, nilikuwa nimemkalia mgongoni kwake akiwa katopea kwenye lindi la usingizi mzito.

Kila mchawi aliyekuwepo eneo hilo alikuwa akinipongeza kwa hatua kubwa na muhimu ya kuifikisha kambi yetu hapo.

Ilikuwa ni hatua kubwa na ya msingi sana kwa muda mfupi niliyokabidhiwa. Wachawi wote walikuwa wamefyata mkia wakiniheshimu kwa nguvu za kichawi nilizokuwa nazo.

Isingekuwa rahisi kwa mchawi yeyote kwenda kinyume na utaratibu niliokuwa nimepanga, kwani adhabu yake ilikuwa ni kifo tu.

Yule Shekhe Nassoro ibn Mahamud alikuwa akihenyeka kwa uzito wangu, nilimkalia akakalika haswa. Tukiwa tumekaa eneo hilo alikuja mchawi mmoja akanitaarifu kuwa wamekwenda kwenye nyumba moja kumchukua fundi wameshindwa.

Taarifa hizi zilikuwa mbaya sana masikioni mwangu, iweje mtu agome kuja kufanya kazi kisa ameweka zindiko nyumbani kwake?

Niliwaagiza wasaidizi wangu wa karibu kumfuata fundi huyo, adhabu yake ingekuwa kubwa zaidi. Hapa niseme kidogo.

Unadhani nini kitaendelea sehemu inayofuata? Usisite kufuatilia simulizi hii ya BUNDI WA GAMBOSHI sehemu inayofuata.


ZIMUHILA?

THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news