WAKILI KIJANA

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWANZONI mwa mwezi wa Oktoba, 2022 nilipigiwa simu na mwenyekiti wa kijiji kimoja huko Tanga akinisalimu ndugu yangu huyu na huku akinijulisha kuwa jamaa wa bomba la mafuta linalopita katika mashamba ya wanavijiji kadhaa watafanyiwa uhakiki kabla ya kulipwa.

Kwa bahati nzuri na mwanakwetu ni miongoni mwao, kweli nilipopata ujumbe huo nilimjulisha mwezangu kuwa jamaa watakuwepo kuhakiki walipwaji wote, jitahidi ushiriki zoezi hilo.

Kweli hilo liliitikiwa vizuri na kwenda kwenye uhakiki. Mwezangu akiwa katika uhakiki aliambiwa kuwa uhakiki wa sasa unafanywa mkiwa mume na mke, kama mume wako ana wake wanne basi wote wake wanne wanapaswa kuwepo.Wahakiki hao walipouliza aina ya ndoa walijibiwa huku wakisisitiza mwanakwetu awepo.

Jambo hilo nilibaini linafanyika ili kuepusha ujanja ujanja unaofanywa na wenza kudhulumu wenzao wao.
Nikawaambia vijana wanaosimamia zoezi hilo kuwa mimi na mwenza wangu tumekubaliana katika haya malipo na tangu mwanzo wa zoezi yeye ndiye anayesimamia na si mimi.

“Dunia ya sasa imeharibika, dhuluma kila kona, lazima muwepo wewe na yeye.” Maombi yangu yaligonga mwamba wakisisitiza uwepo wangu katika eneo hilo kwa kuwa nyaraka za kisheria zinaposwa kusainiwa.

Siku hiyo nilikuwa jirani na Wizara ya Katiba na Sheria nikakata shauri nikisema nitakwenda hapo nitapata kiapo hicho cha kisheria nitakituma ili kuwaondolea utata ndugu zangu hawa wa bomba la mafuta ili mwenza aendelee na zoezi.

Nilipofika Wizara ya Katiba na Sheria nilikutana na mwanasheria mmoja muugwana sana mweusi mrefu, akivaa koti la mistari mistari akanijibu kuwa hicho kiapo kinatwa Power of Attorney nienda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wao watanipa nijieleze vizuri tu.

Mwanakwetu Magufuli amefariki dunia, lakini ametusaidia sana sana ndugu huyu niseme, “Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani, amina.”

Kumbuka nipo Mji wa Serikali Dodoma, ofisi hizi za umma zipo jirani jirani, hata kama mtu yupo Wizara ya Katiba na Sheria akipiga yowe la mwiziii! yule aliyepo Mwanasheria Mkuu wa Serikali anasikia mayowe hayo.

Kama asipofika kutoa msaada wa kupambana na mwizi ni kwa roho yake mbaya tu, maana dunia imejaliwa wema na wabaya

Nilipofika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hapo nikaelekezwa kuwaona mawakili walikuwapo ofisini hapo siku hiyo, lakini kabla ya kuingia kwa mawakili hawa nilikutana na mtu ninayemfahamu miaka mingi nikamsalimu na nikaingia ofisi ya wawakili wa serikali.

Kwa bahati nzuri mmoja wao ninamfahamu kwa sura si kwa majina na nilipoeleza shida yangu mawakili wenzake wakasema huyo wakili kijana atakusaidia kukuandikia Power of Attorney.

Wakati wakili kijana anajipanga kuiandika nyaraka hiyo ya kisheria nikawapigia jamaa wa bomba kuhusu maelezo ya ziada, nikamueleza aliyepokea simu hiyo kuwa nipo na sasa naandikiwa hicho kiapo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,jamaa akasema unajua huyo Mwnasheria Mkuu wa Serikali alisistiza katika vikao vyetu vya pamoja kuwa tusipokee tu kila Power of Attoney bali ni zile zitakazotolewa na mwanasheria wetu au yule tutakayemuagiza tu.

Nikashangazwa sana na jambo hilo, nikasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajiwekea kizingiti yeye mwenyewe? Hayo ndiyo makubaliano, nilijibiwa.

Mwanakwetu nilitafakari hilo nikasema ngoja nimuone huyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali nimuulize swali hili natambua atanijibu. Nikamuaga yule wakili kijana nikasema wanaikataa hata Power of Attorney yenu, ngoja niulize.

Mwanakwetu kumuona Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kazi kubwa sana, Mwanakwetu sikuweza kumuona yeye wala msaidizi wake, japokuwa macho yangu yalifarijiwa kwa kuona vyeo vyao vilivyobandikwa katika milango ya ofisi zao.

Je majengo haya yalijengwa tuyaone kwa mbali na vyeo vyao tu? Tusijibiwe maswali yetu? Swali langu halikujibiwa. Hapo hapo nikakata shauri ya kufunga safari kuelekea Tanga ili niweze kukamilisha kiapo hicho kwa uhakiki huo.

Vijana hawa wa bomba la mafuta wakasema utawezeshwa ili uweze kufika Tanga na kurudi ulipo nikasema sawa, hiyo sasa ni saa 9 alasiri na jua la Dodoma kali mno, nikatoka hapo hadi Buigiri na kusubiri usafiri wa kuunganisha unganisha kuelekea Tanga.

Nilikaa Buigiri kwa saa mbili bila nikingoja usafiri, mweza wangu nikamuomba alale jirani na eneo hilo ili nikifika turudi tena kwa wahakiki wa malipo hayo, kweli alifanya hivyo .

Baada ya muda mchache ikaja gari ndogo, wakanadi Tanga! Tanga! Tanga mmoja ! Tanga mmoja! Nikashusha pumzi maana mwanakwetu unapopata kitu ulichokingoja kwa muda mrefu unaweza kudhani unaota, lakini kumbe majaliwa ndiyo yamekutembelea, nikasogea na kuingia ndani ya gari hii na safari ya Tanga ilianza.

Nilipoingia ndani ya gari hii dereva akaniuliza, Kaka nauli hadi Tanga kiasi gani? Nikamjibu ni shilingi 25,000-30,000 /- akaniuliza una chenji kamili, nikamjibu hapa nina shilingi 25,000/- , shilingi 5000 nitaitoa katika simu nitakupatia. Ndani ya gari hili walikuwapo akina mama wawili na mimi na dereva tukawa wawili safari ikaendelea.

Nikiwa safarini nilibaini kuwa huyu aliniyenibeba katika gari yake alikuwa na mkewe na wanakwenda mazikoni walifiwa na mama yao Tanga Mjini.

Huyu mama mwingine yeye alipewa hisani kama mimi. Tukiwa safarini kaka mwenye gari na mkewe ni wema na wazungumzaji wazuri sana wakaniuliza kaka Dodoma unafanya shughuli gani? Kwa namna walivyokuwa wema na waungwana nikawajibu kuwa niko utamaduni.

Kumbe kaka upo Utamaduni? Nikajibu ndiyo. Akaniambia pale upo na kaka yetu mmoja anaitwa Said Yakub, nikasema ndiyo yule ni Naibu Katibu Mkuu wetu.

“Yakub alikuwa kaka mkuu wetu Usagara Sekondari, mtu mzuri sana, mtu mzuri sana. Alitulinda sana shuleni, alitulinda sana shuleni.”

Mwanakwetu nikasema mtu akishakuwa monita, kiranja na kaka mkuu anakuwa ameshajifunza namna ya kukaa na watu. Kibaya umpe uongozi mtu ambaye alikuwa mpiga kelele darasani, kila orodha ya wapiga kelele yeye yumo au mtu ambaye hajawai kuchaguliwa hata kusimamia hata kufagia darasa, mwanakwetu usitarajie kusimuliwa mazuri na watu wa kawaida.

“Kweli kiongozi anatengenezwa tangu akiwa mdogo, alitusaidia sana shuleni, alitusaidia sana shuleni.”Alisema ndugu huyu kwa hisia kali huku akiendesha gari yake.

Tulisafiri salama na saa nane ya usiku nilishuka Michungwani na wao kuendelea na safari ya yao na kulipokucha nikaenda kijiji husika kukamlisha zoezi hilo.

Mwanakwetu wakati narudi zangu Dodoma, nikamtafakari mno yule kaka aliyenisimulia habari za kaka mkuu, nikasema kwa hakika jamii inawafahamu viongozi wao vizuri sana.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news