Croatia watokea nyuma na kuwalaza Canada mabao 4-1

NA DIRAMAKINI

MABAO ya Wakoratia Andrej Kramaric dakika ya 36 na lile la Marko Livaja dakika ya 44 ya kipindi cha kwanza cha mchuano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 nchini Qatar yalithibitisha kuwa, bao la awali la Alphonso Davies dakika ya pili halikuwa na tija kwa Canada.
Dejan Lovren wa Croatia akijaribu kumdhibiti Kamal Miller wa Canada. (Picha na Hamad I Mohammed/Reuters).

Ni kupitia mtanage huo wa Kundi F ambao umewakutanisha Croatia na Canada katika dimba la Taifa (Khalifa International Stadium) Novemba 27, 2022 jijini Doha, Qatar.

Katika mtanage huo, wawakilishi hao wa Marekani ya Kaskazini walionekana kuanza vema, lakini wenzao Croatia waliwasomea ramani vilivyo.

Dakika 45 za kwanza zilitamatika kwa wa mwisho kuwa wa mwanzo na wa mwanzo kuwa na mwisho, licha ya Wamarekani hao wa Kaskazini kuanza kuona mambo yamekuwa matamu.

Washindi wa fainali za 2018 walikuwa wamefungua kampeni yao ya Kombe la Dunia la FIFA la Qatar 2022 kwa sare tasa dhidi ya Morocco.

Mbele ya watazamaji 44,374 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa, Alphonso Davies alikuwa aliifungia Canada bao la kuongoza dakika mbili tu, akiweka historia kwa kuifungia Canada bao la kwanza kwenye Kombe la Dunia katika mechi yao ya pili baada ya kukosekana kwa miaka 36.
Andrej Kramaric akifurahia kazi yake. (Picha na Reuters).

Kipindi cha pili kilianza kwa pande zote mbili kuonekana kushambuliana vilivyo, ingawa dakika ya 70, Andrej Kramaric alirejea tena nyavuni na kuliwezesha Taifa lake kusonga mbele kwa mabao matatu kwa moja. 

Wamarekani ya Kaskazini licha ya kujitahidi kufanya jambo, mbio zao zilionekana kuishia sakafuni baada ya dakika ya 94 ya kipindi cha pili, Lovro Majer kufunga hesabu.

Canada, ambayo ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Ubelgiji katika mechi yake ya ufunguzi ya Kombe la Dunia, haina alama yoyote baada ya mechi mbili.

Wakati, Croatia wakijihakikishia kuendeleza kampeni yao ya kusalia katika Kombe la Dunia, kipigo hicho kwa Canada kinamaanisha safari yao katika Kombe la Dunia imefikia tamati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news