Faida za ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma zatajwa

NA MWANDISHI WETU

IMEELEZWA kuwa, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma utaongeza nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa inayohitajika kwenye uzalishaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipotembelea mradi wa ujenzi wa Chuo hicho katika eneo la Nala jijini Dodoma ikiwa ni moja ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa jijini hapa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza kwa vitendo katika kufikia malengo akiwemo ujenzi wa Chuo cha ufundi Dodoma ambacho kina kwenda kujibu hitaji la kuwa na wataalamu wenye ujuzi watakaotumika katika uzalishaji.
“Nampongeza Rais kwa maono makubwa aliyo nayo anasema uchumi unaotegemea viwanda anaweka muunganiko, anajenga vyuo ili kupata wataalamu hao, na nimefarijika kusikia Chuo hiki kitatoa fani ya maabara hii itasaidia sana katika hospitali zetu,”amesema Mhe.Senyamule.

Mheshimiwa Senyamule ametoa rai kwa Taasisi zinazotekeleza miradi jijini Dodoma kuhakikisha zinatunza mazingira kwa kupanda miti ili kutunza uoto wa asili na kupendezesha mazingira.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema utekelezaji mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma ni juhudi za Serikali katika kuongeza ujuzi kwa vijana wa kitanzania ili waweze kuutumia ujuzi huo katika soko la hapa nchini na kimataifa kwa kujiajiri na kuajiri wengine.

“Msisistizo wa Serikali yetu sasa ni elimu ujuzi, tunapitia mitaala ya shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ufundi na Vyuo vikuu. Hii ni kutokana na maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaamini mitaala hiyo itakapokuwa tayari hata majengo yatakuwa tayari ili iweze kutumika kuzalisha ujuzi," amesema Naibu Katibu Mkuu Nombo.
Prof. Nombo ametoa rai kwa watanzania kuuunga mkono juhudi za Serikali kwa kupeleka vijana kusoma katika Chuo hicho pindi majengo hayo yatakapokamilika illi waweze kupata ujuzi.

Nae Mshauri elekezi wa Chuo cha Ufundi Dodoma,Mhandisi Aliki Nziku kutoka BICO amesema Chuo hicho kinajengwa kwa awamu mbili ambapo utekelezaji wa mradi awamu ya kwanza ulianza Juni 2021 na unatakiwa kukamilika Desemba 2022.
Amesema,ujenzi unagharimu zaidi ya Shilingi bilioni saba na umefikia asilimia 75. Ameongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi ukikamilika Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 1,5000 awamu zote zikikamilika kitadahili wanafunzi 3,000.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news