HATUWEZI KUMTUPA KAMA MPAGANI-I

NA ADELADIUS MAKGWEGA

“Rais John Magufuli ameongoza mazishi ya mwanasiasa mkongwe hapa nchini Kingunge Gombare Mwiru, aliyezikwa kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, shuguhuli iliyotanguliwa na ibada iliyofanyika nyumbani kwake kabla ya kuagwa kitaifa katika kiwanja cha Karimjee, Kingunge alikutwa na umauti siku ya ijumaa Februari 2, 2018 wakati akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”
Haya yalikuwa maelezo ya mtangazaji Charles Hillary katika taarifa ya habari ya chombo kimoja cha habari nchini Tanzania.Sikupepesa kando macho yangu na sasa msafara ulielekea makaburi ya Kinondoni kwa maziko. Nilisikia wimbo wa dini ukiimbwa huku jeneza likiingizwa kaburini. “Kwa ishara ya msalaba tuokoe.”

Kwa kuwa wimbo huu ninaufahamu wenye kiitikio kifupi na mashairi mafupi mafupi, nikaimba moyoni ubeti wake wanne, “Wafalme nao wa dunia wanajipanga panga Mungu wetu- Kwa ishara ya msalaba tuokoe.” Kweli niliamini Kingunge Ngombare Mwiru anazikwa kwa taratibu za Kanisa Katoliki.

Kwa kuwa Kingunge Gombare Mwiru nilikuwa namfahamu kiasi, nikiipenda tabia yake ya ukweli nilitamani sana kumfahamu kwa kina alikuwa ni mtu wa imani gani na maisha yake yalikuwaje katika imani yake ya dini? Jambo hili lilikuwa gumu sana kupata majibu lakini baadaye nilipatia nyaraka moja ambayo ilipewa kichwa “Gumzo kuhusu Kanisa kumzika Hayati Kingunge latolewa ufafanuzi.” Maelezo hayo yalikuwa haya,

“Ni kweli Mzee Kingunge enzi za uhai wake kuna masuala mbalimbali ambayo yalimsababisha aasi imani Katoliki, lakini wakati akiwa mgonjwa alijirudi na kuonesha nia na utayari wa kumrudia Mungu wake. Muda wa kumrudia Mungu wakati mwingine hautabiriki na yeye alikuwa na viashiria vya imani na kwamba alitaka kurudi kwenye imani Katoliki. Viashiria hivyo ni kutubu na kuomba sakramenti ya upako wa wagonjwa na Kanisa lipo kwa ajili ya mtu anayetubu. Kanisa halihukumu ila lipo kwa ajili ya kumpatia mwanadamu huduma za kiroho katika safari yake ya kwenda mbinguni. Mzee Kingunge mwishoni mwa maisha yake ameonesha nia yake na heshima kwa kanisa ingawa kuonesha nia ni kitu kingine na kutekeleza masharti ni kitu kingine,”

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Euzebius Nzigilwa alinukuliwa haya. Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam si kawaida Katekista kuendesha ibada ya mazishi kutokana na mazingira na uwepo wa mapadri wa kutosha ingawa kwa mazingira ya watu wanaoishi vijijini ni kawaida. “Mtu aliyeasi imani akionesha nia ya kurudi, kanisa linafungua milango na kumpokea ingawa lazima apewe masharti kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Kanisa Katoliki.

“Mzee Kingunge alionesha nia, lakini kuna baadhi ya vipengele alikuwa hajakamilisha akafariki, kuwa na nia ni kitu kingine na kutimiza masharti kulingana na taratibu za Kanisa ni kitu kingine. Kwa sababu hakupata nafasi ya kutekeleza kanuni na taratibu mbalimbali na kufariki, basi ilibidi azikwe na Katekista kuonesha kuwa bado ana pungufu flani hivyo hapati ile huduma kamili ya kanisa anapata huduma ndogo. Angekuwa ametimiza kila kitu angezikwa kwa misa takatifu na maadhimisho yote anayopaswa kupatiwa mkristo kamili wa Kanisa Katoliki,”

Maelezo hayo ya Askofu Msaidizi Nzigilwa yaliendelea kunukuliwa huku akiwaasa waamini wote wa Kanisa Katoliki kujitahidi kushika imani kwa nia na matendo kulingana na taratibu za kanisa. “Mzee angefariki ghafla na kukosa nafasi ya kuonesha nia asingepata hata hiyo huduma ndogo ya kanisa ingekuwa kitu kingine kabisa.”

Hapo mwanakwetu sasa nilipata maelezo ya jumla la kanisa hilo, baadaye alinukuliwa na vyombo vya habari marehemu Monsinyori Deogratius Mbiku ambaye ni ndugu yake Hayati Kingunge na ndiye aliyempatia huduma ya kiroho kwa mara ya mwisho na kuzungumza naye mara ya mwisho hiyo nia yake ya kurudi katika imani ilipoonekana.

Monsinyori Mbiku ambaye wakati wa uhai alikuwa miongoni wa mapadri wa zamani katika Jimbo Katoliki la Dar es Salaam akiwa paroko katika parokia kadhaa alikuwa na nasaba na mwanasiasa huyu.“Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa Mkristo Mkatoliki aliyebatizwa akapata sakramenti ya komunio ya kwanza na kipaimara, akasoma kwenye shule ya misheni pale Msimbazi alikaa bweni na baadaye shule ya kati ya Ilala lakini alikuwa anarudi kukaa pale Msimbazi Parokiani, huku akiwa miongoni mwa vijana watumishi wa misa enzi hizo.”

Tangu utoto wake Kingunge alikuwa na akili nyingi na akili hizo zilimsababisha kuhoji masuala mbalimbali ya imani, mathalani dini ni nini? Mungu yupo wapi? Hata katika mafundisho ya Katekisimu alikuwa mdadisi sana.

“Yeye mwenyewe Kingunge alinisimulia kuwa, wakati fulani Padri Clement M Mkapuchini alimuona anadadisi mno masuala ya imani na kumtilia shaka. Ndipo akamtenga na kanisa akiwa darasa la sita. Huyo Padri alimuuliza kama Kingunge alikuwa ni mkomunisti?(mtu asiyeamini Mungu). Kama ni mkomunisti ninakutenga na kanisa.”

Je kipi kitaendelea? Subiri matini ijayo.

(NB Monsinyori /Mosinyo ni mtu anyefanya kazi katika ofisi ya Askofu, akitekeleza majukumu ya Kiaskofu japo hajafikia daraja hilo).


0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news