BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 51

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...niliwaagiza wasaidizi wangu wa karibu kumfuata fundi huyo, adhabu yake ingekuwa kubwa zaidi. Hapa niseme kidogo...

Endelea...

Ni hatari kubwa sana kwa mtu wa kawaida kuweka zindiko la kawaida nyumbani kwako. Kitu usichokijua ndugu msomaji, upo uhusiano mkubwa wa kinguvu baina ya dawa ya zindiko na wachawi. Unapoweka zindiko nyumbani kwako ni chanzo cha kukaribisha wachawi nyumbani kwako.

Nguvu zilizoko kwenye mazindiko huwa zina tabia ya kuwavuta wachawi, mara nyingi mchawi yeyote anapopita karibu ya nyumba hiyo atakutana na nguvu hizo.

Badala ya kuendelea na safari yake husitisha na kuanza kujaribu kuingia kwenye miji husika. Akishindwa huendelea na shughuli zake, katika safari zake hizo huwasimulia wachawi wenzake atakaokutana nao.

Kila mchawi atakayesimuliwa huja eneo hilo kujaribu dawa zake, katika ushirikiano huo endapo watafanikiwa kupenya kwenye zindiko hilo ni hatari kwa mji na mganga mwenyewe.

Miongoni mwa hasara ni pamoja na familia kupoteza wanafamilia au kufanyiwa vitu vya ajabu. Huwa ni vigumu kwa wachawi kushindwa kuingia labda zindiko hilo liwe limewekwa na mganga Mkuu. Na hapo hakikisha kuwa umepewa zindiko pia la mwili, maana kama utakuwa umezindika nyumba lakini mwili ukauacha watakukamata kirahisi sana.

Upo uhusiano mkubwa sana baina ya mchawi na mganga, kuna baadhi ya vizimba hasa vya binadamu waganga huja kuchukua kwetu.

Mganga yeyote mkubwa anayefahamika na kuogopwa ndani ya jamii, tambua kuwa dawa zake hutumia vizimba vya binadamu.

Kwa upande mwingine wachawi tunaweza kumpa ajira mganga kama tunaelewana. Mfano tunaweza kumloga mtu kisha tukamuelekeza kupitia dawa kwenda kutibiwa kwa mganga ambaye huwa tumemuelekeza tiba yake.

Mara nyingi waganga wa hivi huwa tuna mahusiano mazuri, endapo tutakuwa tunamhitaji mtu wetu aliyekimbilia hapo ni rahisi kutukabidhi. Hii huturahisishia kumchukua kama tulivyokuwa tumekuzudia

Ukisikia mtu kafia kwa mganga au kaagwa kwa mganga kisha baada ya siku mbili akafa, tambua hapo kuna biashara kubwa imefanyika baina ya mganga na wachawi. Pia kuna waganga vichwa ngumu, hawa ndiyo ni washenzi wakubwa. Huwa hawapendi suluhu baina yetu na wao, kuna muda huwa wanazindika mpaka maeneo yetu ya kuchezea.

Huja hata kwenye sherehe na mikutano yetu wakiwa hawaonekani, hutusumbua sana katika shughuli zetu kwa ufafanuzi zaidi fuatilia simulizi ya VITA VYA MGANGA THE BOMBOM NA WACHAWI, hapo ndipo utaona namna waganga hao husumbua.

Walikwenda wasaidizi wangu kwenye nyumba ya fundi huyo aliyekuwa ameshindikana kuja kujenga. Baada ya muda walirudi wakiwa na jibu kuwa wameshindwa kumchukua fundi huyo, jambo hilo lilinikera sana. Kwa kuwa ilikuwa ni saa tisa za usiku tuliamua kumuache fundi huyo mpaka kesho yake. Tuliwaruhusu mafundi wengine kurudi makwao huku nikiwa na hasira kedekede kwa fundi huyo.

Kesho yake asubuhi tuliendelea na ratiba yetu kama kawaida, mchawi aliyekuwa zamu alitoa taarifa za siku kisha nikazichunguza kabla ya kuzituma makao makuu kwa mkuu wa giza.

Tuliendelea na shughuli zetu kama kawaida mpaka ilipofika jioni, GAMBOSHI MPYA ilikuwa imefikia kiwango kizuri katika ujenzi wake. Siku hiyo hatukuwa na ratiba ya ujenzi nikaamua kuitumia siku hiyo kumtembelea fundi huyo aliyegoma kuja kujenga GAMBOSHI MPYA.

Muda wa saa nne usiku tuliondoka na jopo dogo la wachawi kuelekea kwa fundi huyo aliyezindika kwake. Tulitumia usafiri wa upepo kwa kuwa haikuwa mbali sana.

Tulipofika tulisimama mbali na mji huo, tukiwa tumesimama nilinyoosha mkono wangu akatua popo kiganjani mwangu.

Popo yule nilimkamata vyema nikamunuia maneno fulani kisha nikampaka dawa, baada ya hapo nilimruhusu kwenda kwenye nyumba hiyo. Yule popo alipofika eneo husika alipoteza uelekeo kisha akaenda kujibamiza juu ya paa la nyumba ya fundi huyo.

Hapa niseme kidogo, kuna muda majumbani mwenu wakati wa usiku kuna vitu huanguka batini. Pia kuna popo, bundi au wadudu fulani wadogo wanaofanana kifaru, unapowaona nyumbani kwako kuwa makini.

Wadudu au ndege hao wanaweza wakawa wa kawaida kabisa au wanaweza wakawa wametumwa. Kuweza kuwatofautisha wadudu hao na ndege hao, mara nyingi popo au ndege wa kichawi huwa na fujo kwa dakika chache kisha hupotea.

Baada ya popo huyo kuanguka batini na kufa, nilimuita paka mmoja wa kazi nikamtuma kuingia kwenye mji huo.

Lengo la kuwatuma wanyama hao ilikuwa ni kupima kiasi cha dawa za zindiko zilizoko kwenye mji huo. Yule paka alikuwa amesheheni dawa mwilini mwake, dawa hizo zilikuwa na dawa ya kutegua zindiko hilo.

Hapa niseme kidogo, siku zote nyumbani kwako unapoona paka mweusi tii anatembea kwa haraka haraka kwa uoga tambua yule ni paka halisi.

Ila paka huyo anaweza akawa wa kawaida au kichawi, paka wa kichawi hufanya shughuli zake haraka kisha kuondoka.

Ila ukiona paka mweusi tii mwenye kisirani basi huyo siyo paka ni binadamu aliyechukua umbo la paka.

Paka wa namna hii ukikutana naye ni rahisi kumgundua, kwanza mwili wako utajisikia kusisimkwa. Nywele zitasimama bila sababu, mapigo ya moyo huongezeka bila sababu. Ukiona dalili hizo tambua paka uliyekutana naye siye paka bali ni binadamu, yupo kwenye shughuli zake.

Yule paka alikwenda kwenye mji huo, akiwa pale alifanikiwa kuvuka fensi na kuingia kwa ndani. Alipofika kiwanjani mwa nyumba hiyo alidondoka na kufa, tuligundua hilo kupitia viganja vyetu.

Kwa namna hiyo tulitambua kuwa nyumba hiyo ilikuwa imezindikwa vya kutosha, kwa kuwa ilikuwa bado mapema niliwaambia wachawi wenzangu turudi kidogo kambini tukajipange.

Tulipofika kambini tulichukua dawa za kiwango cha juu tukarudi kwenye mji huo huku hasira zikiwa zimetamalaki nyoyoni mwetu.

Tulikuta kikundi kingine cha wachawi kikihangaika kutaka kuingia kwenye nyumba hiyo. Kama nilivyosema awali siku zote mazindiko huwa yana tabia ya kuita wachawi.

Mji wowote wenye mazindiko hutembelewa kwa kiasi kikubwa na wachawi, kulingana na uhusiano wa zindiko na wachawi.

Tuliamua kuwaacha kwanza makundi hayo kujaribu madawa yao, waliendelea kuhangaika mpaka saa sita za usiku.

Baada ya hapo tuliwazuia kisha tukachanganya dawa zetu, tukatengeneza upepo wa dawa tukautuma kwenye mji huo.

Upepo huo ulipita kwenye mji huo huku uling'oa mazindiko yote yaliyokuwa kwenye mji huo. Hapa niseme kidogo, siyo kila upepo mzito unaoambatana na mchanga wakati wa usiku unaopita kwenye mji wao ni wa heri.

Upepo mwingine unakuwa na malengo yake, nadhani umeona upepo huo ulivyosaidia kuondoa mazindiko ya mji huo.

Zindiko linapoondolewa kwenye mji husika lile joto huondoka, hapa niseme kidogo mji wenye zindiko kali wachawi hatuwezi kuingia kwa kuwa huwa kuna joto kali.

Ukisogea zaidi unaweza kupoteza maisha, ndiyo maana wachawi hugundua kwa urahisi mazindiko ya majumbani mwa watu. Lile joto lilikuwa kimeondoka kabisa, wachawi walikuwa wakishangilia kwa ushindi huo.

Tuliingia kwenye nyumba hiyo kwa hasira, mbaya zaidi tulimkuta mke wa fundi watoto pamoja na ndugu wengine. Tuliwatowa nje na kwenda kuwashikisha adabu, kila mchawi aliwafanya alivyojisikia.

Baada ya hapo waliwachanja dawa fulani na kuwarudisha ndani. Dawa walizochanjwa zilikuwa za kuwafanya kuugua siku zote, leo akipona mmoja kesho wanaugua wawili imradi familia hiyo isipate raha.

THE BOMBOM bado nilikuwa kwenye lindi la mawazo, nilikuwa nawaza juu ya mganga aliyekuwa amemzindika. Haiwezekani mganga akaja mji wa Majengo akafanya shughuli zake na kuondoka bila kujulikana.

Kwa nini hakututafuta kwanza wachawi tukamuelekeza taratibu zetu? Mganga huyo alipaswa kujulikana kwa namna yeyote, harafu kwa nini fundi mwenyewe hajaonekana? Alikwenda wapi usiku huo? Kwa nini ameweka zindiko nyumbani kwake? Yalikuwa ni maswali yaliyohitaji majibu toka kwa fundi huyo.

Kwa namna yeyote alipaswa kusakwa mpaka apatikane, hawezi kuzuia kazi za watu usiku kwa zindiko lake la kipumbavu.

Ndugu msomaji nini kitampata fundi huyo na mganga wake. Je, THE BOMBOM atafanikiwa kumtia mkononi fundi huyo na mganga wake. Endelea kufuatilia simulizi hii.

KOLAKOLA.
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news