HULKA YA KIONGOZI

NA ADELADIUS MAKWEGA

MMWAKA 2019 watumishi kadhaa wa Serikali walifika Kijiji cha Ujamaa Shilanga kilichopo katika Kata ya Ihanda wilayani Mbozi wakielekea kijiji cha mbali na hapo kutoa huduma ya matibabu inayofahamika kama Kliniki Tembezi.

Kundi hilo likiwa na magari matatu wakapita kando ya Shule ya Msingi Shilanga na kiongozi wa msafara huo akawaambia, “Jamani siyo hekima kupita shule hii bila ya kuwasalimu wenzetu wanaofanya kazi hapa, tushuke.”

Katika msafara huo alikuwapo kiongozi mkubwa wa Halmashauri ya Mbozi hii wakati huo, pia alikuwapo Afisa Elimu Sekondari Hosana Nshullo akatangulia kumuongoza kiongozi wake kuelekea shuleni hapo na walimu waliokuwa mapumziko wakazungumza kwa haraka haraka changamoto walizokuwa nazo zikiwamo ubovu wa madarasa.

Hosana Nshullo alijibu hoja kadhaa za Idara ya Elimu Msingi ambayo wakati huo haikuwa na Afisa Elimu Msingi, kwani wa awali alipandishwa cheo na hapo akisubiriwa Afisa Elimu Msingi mpya.

Akakaribiswa kiongozi mkubwa katika safari hiyo na yeye kuongea kidogo wakatoka nje ya ofisi ya walimu na kuelekea katika gari.

Wakati hawa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi wanatoka ofisi ya walimu wa shule hii wakakutana na wanafunzi wanarudi madarasani baada ya mapumziko ya saa nne. Miongoni mwao alikuwapo mwanafunzi mmoja akitembea kwa gogo moja huku mguu wake moja ameukunja.

Huyu kiongozi akamuita yule mwanafuzi wewe njoo! na hapo hapo yule Mwalimu Mkuu akamuita Erick njoo mara moja. Akafika yule mwanafunzi mwenye gongo pale walipo madaktari wakakimbilia, wakiambiwa mtazameni huyu mtoto na je tunamsadiaje?.

Katika msafara huu kumbuka wanakwenda kutibu wagonjwa vijijini na kuhamasisha maendeleo, kulikuwa na ndugu wafuatao Alexia Njogela (Muuguzi na Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Wilaya), Togolai Gembe (Afisa Afya Mratibu Majengo), Khanifa Nyaruke (Muuguzi na Mratibu wa Lishe), Dkt. Mkilo Ambalike (Meno),Dkt. Kapota Mwanahamisi (Mratibu –HIV &UKIMWI) Dkt.Bashasha Easter (Mratibu wa Kifua Kikuu&Kaimu Mganga Mkuu).

Madaktari wakaendelea kumkagua, naye Mwalimu Mkuu akisema kuwa huyu mtoto aliungua moto mwaka 2017 akiwa darasa la pili kwa hiyo ndipo nyama za paja zikaungana na za mguu.

“Mwanafunzi huyu ni yatima na analelewa na babu yake, akiwa darasa la pili alirudi nyumbani kutoka shuleni, jioni akajipikia chakula chake, alipokuwa anataka kula kulikuwa na giza, akawasha kibatari lakini hakikuwaka kwani kilikosa mafuta . Kwa hiyo alichukua pesa na kwenda dukani kununua mafuta ya taa. Alipofika dukani akalipa pesa ya mafuta ya taa na muuzaji dukani kuyafunga katika mfuko wa nailoni akayafunga kwa juu halafu akampa mwanafunzi huyu na akayaweka mfukoni katika kaptula yake, kuanza safari ya kurudi nyumbani kupata mwangaza katika chumba chake.”

Mwalimu Mkuu Shilanga alisimulia mbele ya viongozi kadhaa wa wilaya na diwani wa eneo hilo wakati huo kutoka CHADEMA wakati huo huo alikuwa ni Katekista.

Kumbuka wazazi wa Erick wemefariki na anakaa kwenye nyumba hiyo hiyo ya wazazi, lakini kwa kando kuna nyumba ya babu ambaye ndiye mkubwa jirani.

Kwa desturi ya vijiji wazee jioni huwa wanakwenda vilabuni kunywa pombe na hata kama mtu si mwanachama wa pombe anakwenda kuongea na wenzake, babu yake Erick alikuwa akitimiza desturi hiyo.

Erick akafika nyumbani akayatoa mafuta yake aliyoyaingiza katika mfuko wa kaptula yake yakiwa yamemwagikia kaptula hiyo kidogo na kuyaweka katika kibatari vizuri sana. Akakiwasha badala ya kupata mwanga Erick akapata mlipuko na nyumba ya nyasi ikashika moto, kibatari kikawaka, kaptula aliyovaa inawaka.

Erick alianza kulia kwa sauti kubwa, majirani na wapita njia wakidhani kuwa mtoto huyu anaadhibiwa na wazazi wake labda kwa utovu wa nidhamu kumbe anateketea kwa moto.

Watu wakawa wanapita wanaendelea na maisha yao jioni hiyo, hakuna aliyeweza kutilia maanani jambo hilo, akawa anaungua kwa moto huku ajitahidi kupamba na uhai wake anajigalagaza kwenye mavumbi kuhangaika kutoka nje ya nyumba hiyo, akafanikiwa na hapo hapo watu wakagundua nyumba inaungua, wakaja kuuzima.

Babu yake akafuatwa akaja wakaanza kuhangaika na matibabu. akiwa amepata matibabu ya kusuasua kukosa pesa, akitibiwa na mitishamba alikuwa analala chali miguu akining’iniza huku tumbo lake likiwa limeungua kwa moto huo. Hapo akapona na ndipo nyama ya paja ikaungana na naya mguu wake na kushindwa kunyooka.

Watumishi wa Halmashauri ya Mbozi wanamuona miaka miwili baada ya tukio hilo, yupo darasa la nne anaingia darasani akiwa na gogo lake ameshakuwa kilema. Madaktari hawa wa Kliniki Tembezi walibaini kuwa upasuaji unawezekana na gharama ya kati ya shilingi 500,000 hadi 700,000 za Kitanzania.

Wakati huo Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ilikuwa haina uwezo wa kufanya upasuaji huo bali Hospitali ya Binafsi ya Mbalizi au Rufaa Mbeya zilikuwa na vifaa bora.

Hapo hapo alibebwa na kupewa rufaa hadi Mbalizi na pesa ikatolewa taslimu kulazwa hospitali hii na kufanyiwa upasuaji. Naye Dkt. Easter Bashasha (Kaimu Mganga Mkuu wakati huo) akisimamia zoezi hilo.

Kwa hesabu za namba mwanafunzi huyu anayefahamika kama Erick Mbwile mwaka 2022 amehitimu darasa la saba na kwa maendeleo yake darasani atafaulu tu kwenda kidato cha kwanza.

Mwanakwetu kumbuka Erick aliungua mwaka 2017 hakupata huduma, ukaja 2018 hadi 2019 walipopita hawa ndugu.Msomaji wangu nakuomba nikurudishe katika aya hii,

“Watu wakawa wanapita wanaendelea na maisha yao jioni hiyo hakuna aliyeweza kutilia maanani jambo hilo, akawa anaungua kwa moto huku ajitahidi kupambana na uhai wake anajigalagaza kwenye mavumbi kuhangaika kutoka nje ya nyumba hiyo, akafanikiwa na hapo hapo watu wakagundua nyumba inaungua, wakaja kuuzima.”

Mwanakwetu popote ulipo hulka ya kiongozi inaweza kuwa na manufaa sana kutatua changamoto za wananchi lakini pia inaweza kuwa shida kubwa kuwasaidia hao hao wananchi.
Leo hii nimeamua kumkumbuka huyo Afisa Elimu Sekondari Mbozi wakati huo, MwalimuHosana Nshullo (pichani) na wenzake nilioweza kuwakumbuka, lakini pia matini iwe chagizo la kumsaidia kijana huyu wa Kitanzania wa Mbozi na Songwe kama akifaulu apangiwe shule nzuri ya bweni ili aweze kusoma kwa amani.

makwadeladius @gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news