KMC FC yajiandaa kupeleka 'pira spana' kwa Singida Big Star

NA DIRAMAKINI

KIKOSI cha Timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam (KMC FC) kimeanza maandalizi kuelekea katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Singida Big Star utakaochezwa Novemba 23, 2022 katika Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa Novemba 17, 2022 na Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC, Christina Mwagala.

"Kikosi chetu cha cha Manispaa ya Kinondoni kimeanza maandalizi yake leo mara baada ya kutoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji kwa magoli mawili kwa moja.

"Katika maandalizi hayo, Kocha Mkuu Thierry Hitimana amepanga programu mbalimbali ikiwemo kufanya marekebisho ya makosa mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na hivyo kupelekea kupoteza ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

"KMC FC inajipanga kufanya vizuri kwenye mchezo unaokuja licha ya kuwa itakuwa ugenini pamoja na ushindani uliopo kwenye ligi bado timu ipo imara katika kuhakikisha kuwa inafanya vizuri kwenye michezo inayokuja.

"Tunatambua kuwa, tunakwenda kwenye mchezo mwingine mgumu na wenye ushindani ambao tutakuwa ugenini, bado hatujapata matokeo mazuri kwenye michezo minne tuliyocheza ambapo kati ya hiyo tumepata alama moja dhidi ya Geita, ila hatukati tamaa kwa sababu tuna kikosi bora.

"Mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji tulipoteza kutokana na changamoto ya uchovu, na ni matokeo ambayo yalimuumiza kila mmoja, lakini kama timu bado tupo imara na hatujakata tamaa kwa sababu tunafahamu wachezaji wetu wapo kwenye kiwango kizuri,"amefafanua Mwagala.

Pia amewaomba mashabiki na watanzania wote ambao wanawaunga mkono siku zote kutokuwa na hofu. "Pamoja na kwamba hatuna matokeo mazuri kwenye michezo minne mfululizo, lakini bado tuna nafasi nyingine ya kufanya vizuri kwenye michezo inayokuja.

"Kwa upande wa afya za wachezaji wote wako vizuri, lakini Matheo Anton anaendelea na programu ya mazoezi mepesi ya peke yake, Awesu Ally Awesu bado hajajiunga na wenzake na hivyo anaendelea na matibabu pamoja na uangalizi wa daktari,"amefafanua Mwagala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news