KUPANDAPANDA KWA BANDO, SUBIRINI HAPOHAPO

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 21, 2022 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye amewataka watoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kutobadilisha vifurushi vya vya inteneti hadi pale watakapotoa bei elekezi Januari, 2023.

Mheshimiwa Waziri amesema wako katika hatua za mwisho kukamilisha tathmini ya gharama za huduma za mawasiliano nchini na kwamba wanategemea kushusha gharama za vifurushi hivyo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijni Dar es Salaam ambapo alisema kuwa, kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala wa vifurushi mbalimbali vya simu ikiwemo intaneti huku watumiaji wakihoji hatua zinazochukuliwa na serikali.

Pia amesema kuwa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikifanya tathmini kila baada ya miaka mitano na kwamba tathmini ya mwisho imefanyika mwaka 2018 huku gharama za huduma hizo zikiwa kati ya shilingi 2.03 na 9.35. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwanbande anasema, subira yavuta heri kwani tathmini ndiyo jawabu, endelea;


1.Hizi gharama za data, zisimame hapohapo,
Haya tunayoyapata, Serikali ipo hapo,
Ni muda wa kuchakata, kuongezaongeza po,
Kwa hamu twasubiria, gharama kukokotoa.

2.Kupandapanda kwa bando, subirini hapohapo,
Tathmini ndiyo mwendo, tujue hapa tulipo,
Hiki kizuri kitendo, tuache tupumuepo,
Kwa hamu twasubiria, gharama kukokotoa.

3.Hivi sasa ukicheki, bei za bando zilipo,
Huwezi ukalaiki, tofauti kubwa zipo,
Zingine hazipimiki, ni malalamiko hapo,
Kwa hamu twasubiria, gharama kukokotoa.

4.Hili jambo jema sana, walalamikaji mpo?
Serikali inaona, kama lidhani haipo,
Hatua mnaziona, tufikie tutakapo,
Kwa hamu twasubiria, gharama kukokotoa.

5.Huduma tunazipenda, walipo na sisi tupo,
Bando kwa kupandapanda, hufanya tuwepowepo,
Ndiyo maana twapenda, kupanda kumekuwa po,
Kwa hamu twasubiria, gharama kukokotoa.

6.Twaunganisha mikono, ya kwamba mwanga uwepo,
Tathmini liwe neno, na unafuu uwepo,
Tusijishike kiuno, bei zinazokuwepo,
Kwa hamu twasubiria, gharama kukokotoa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments