Maagizo ya Rais Samia marekebisho sheria za habari yaonesha nuru mpya

NA DIRAMAKINI

IKIWA ni miezi kadhaa imepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan atoe maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo, hatimaye nuru imeanza kuonekana.

Ni baada ya Serikali kuwaeleza Wadau wa Kupata Habari (CoRI) kuwa, inaendelea na mchakato wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari na hatua inayofuata ni kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016.

Tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana, Mheshimiwa Rais Samia aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Akizungumza katika kikao cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI), kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 21,2022,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa Serikali imepokea mapendekezo hayo na sasa wanayafanyia kazi.

“Serikali inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria na sasa tunayafanyia mapitio ya mwisho ya mapendelezo ya marekebisho ya sheria,”amesema Mheshimiwa Nape.

Pia Mheshimiwa Waziri Nape amesema kuwa, hatua inayofuata baada ya kikao hicho, ni uandishi wa mapendekezo hayo na kisha kupelekwa kwa watunga sheria.

”Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili.Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua.

…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,” amesema Mheshimiwa Nape.

Aidha, baada ya kikao hicho Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amekiri wazi kuwa, kuna muelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Kikao kilikuwa kizuri,Serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.

‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi Serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’amesema Balile.

Aidha, miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa Serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Pia wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Aidha, wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.

Wadau

Tangu awali wadau wa habari akiwemo mwanahabari na wakili wa kujitegemea nchini, James Marenga alisema kuwa, katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria za Habari,Serikali imeonesha nia ya kufanyia kazi vipengele mbalimbali, hivyo mchakato huo utapata majibu yatakayomaliza kiu sekta ya habari.

Amesema kuwa, nia ya Serikali ni kuhakikisha mwafaka unapatikana katika Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari na wadau wa habari wamekiri kuwepo kwa nia hiyo.

Wadau wa habari wamekuwa wakilenga vifungu vinavyotisha waandishi na uhai wa tasnia ya habari nchini na kwamba, sio sheria yote ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 havifai.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo, kulikuwa na sheria ya mwaka 1976 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,”amesema Marenga.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Neville Meena akielezea kuhusiana na michakato mbalimbali inayoendelea ili maboresho ya sheria za habari nchini yaweze kutekelezeka kwa wakati anasema, awamu hii kuna dhamira njema.

“Awali Serikali haikuonesha dhamira ya kushughulikua maoni ya wadau wa habari nchini, lakini katika utawala huu wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan dhamira imeoneshwa tangu mwanzo, tunaamini tutafanikiwa," anabainisha.

Meena amesema,Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 iliacha mambo ya msingi katika kukuza tasnia ya habari na badala yake ikawa ni sheria ambazo ni ngumu kutekelezwa.

Anasema, kutokana na kuwepo kwa mazingira magumu ya habari na wanahabari nchini, tasnia ya habari iliyumba kwa kiwango kikubwa.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumika. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’amesema Bw.Meena

Alisema kuwa, kuna lawama zinaelekezwa kwa vyombo vya habari kukosa weledi, moja ya changamoto inayovikabili ni kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

Meena alisema, vyombo vya habari vinashindwa kulipa mishahara kwa kuwa, watangazaji wengi hasa Serikali kwenye halmashauri,wanatoa matangazo lakini hawataki kulipa hivyo kuchangia kushuka kwa weledi kwenye vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vinalalamikiwa kukosa weledi, lakini tukumbuke kwamba wanaotoa matangazo na kushindwa kulipa, wanachangia kutengeneza tatizo.

“Wanaoongoza kutolipa ni wakurugenzi wa halmashauri, hili linachangia kuyumbisha vyombo vya habari na ndio maana tumependekeza baada ya miezi sita mtangazaji kushindwa kulipa, licha ya kukumbushwa basi afikishwe mahakamani,’’amesema.

Makunga

Kwa upande wake mwenyekiti wa zamani wa TEF, Theophili Makunga amesema, suala la utashi wa kisiasa ni muhimu katika uandishi wa sheria kwa sababu linatoa mwelekeo wa sheria husika.

"Ikumbukwe kwamba tumetoka mbali kwenye sheria ya waandishi wa habari, kwa muda mrefu nchi yetu ilikuwa inaongozwa na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, sheria ya magazeti ilikuwa na vipengele vingi sana vilivyokuwa vinambana mwandishi wa habari.

"Lakini kulingana na teknolojia iliyokuwepo wakati ule, baada ya Media Service Act, 2016 kufuta ile Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 vile vile kuna vipengele bado vinambana mwandishi wa habari.

"Lakini tunashukuru kwamba, Serikali imeliona hilo na imekubali kuongea na vyombo vya habari kurekebisha baadhi ya vipengele ambavyo tunafikiri vinawabana waandishi wa habari,"amesema Makunga.

Balile tena

Katika mwendelezo wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile anasema vyombo vya habari vinapaswa kujenga tabia ya kuanzisha mijadala yenye kuchochea ukuaji wa uchumi na sio mijadala isiyo na tija kwa nchi na wananchi wake.

Anasema, ni vema masuala ambayo yanahusu uboreshaji wa viwanda, miundombinu na kilimo ambayo yatabadilisha maisha ya Watanzania wote kutoka katika umasikini kupewa kipaumbele na nafasi zaidi kuliko zile za maisha binafsi ya watu na malumbano ambayo hayana tija.

“Kwa wenzetu katika nchi zinazoendelea wanajadili namna ya kukuza biashara na viwanda vyao kwa kuzalisha bidhaa bora pamoja na kutafuta masoko, sisi hapa tuna viwanda, uzalishaji wa gesi, lakini hauoni mijadala mingi kwenye eneo hilo, wanahabari tubadilike,”anasema Balile.

Pia amesema, wataendelea kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya sheria zinazogusa tasnia ya habari kwa kushirikiana na wadau wengine nchini.

“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayotukabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema.

Mhariri Mkuu wa Gazeti la Guardian,Walace Maugo ametumia nafasi hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kupigania haki za Watanzania na kuboresha maisha yao kupitia taaluma yao na kazi wanazozifanya kila siku.

“Kama tunavyofahamu kwamba sisi ndiyo tunaotengeneza mijadala kwenye jamii, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha maisha bora yanapatikana na watu wanafurahia maisha katika nchi yao, tusijione wanyonge kuna hatua kubwa zimechukuliwa kutokana na kazi tunazozifanya,” amesema Maugo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news