Magereza yashindwa kufua dafu kwa Tamisemi

NA PETER STEPHEN

MATUMAINI ya timu ya Netiboli ya Magereza Tanzania ya kulitwaa kombe la Muungano la ligi la Netiboli yalififia jana baada ya timu hiyo kukubali kipigo cha magoli 56-31 kutoka kwa Mabingwa watetezi wa Kombe hilo Tamisemi Queens.
Mfungaji hodari wa Tamisemi Queens Lilian Jovin, akifunga mojawapo ya magoli katika mchezo wa jana dhidi ya timu ya Magereza Tanzania ambapo Tamisemi iliifunga Magereza magoli 56-31.

Hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika Magereza walikuwa nyuma kwa magoli 15-10,ambapo katika robo ya pili timu hiyo ilipata magoli 17 dhidi ya 30 ya Tamisemi na katika robo ya tatu iliambulia magoli 25 kwa 43.

Tofauti na mchezo wao dhidi ya JKT Mbweni, ambao wachezaji wa Tamisemi walicheza kwa nguvu katika muda wote, kivutio katika mchezo wa jana kilikuwa kwa wafungaji hodari wa timu zote mbili Lilian Jovin wa Tamisemi Queens na Mariam Shaban wa Magereza Tanzania.

Wakati Lilian ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya netiboli alionyesha ustadi mkubwa wa kurusha mipira ya mbali golini na kufanikiwa kufunga, naye Mariam wa Magereza aliutumia vizuri urefu wake kufunga kila alipopata nafasi ya kutumbukiza mpira katika goli la Tamisemi.

Hadi kufikia sasa Tamisemi Queens imeshinda michezo yake yote saba iliyokwishacheza katika mashindano haya na imesaliwa na michezo miwili, ambayo ni dhidi ya Chuo Kikuu cha Kampala na KVZ kutoka visiwani Zanzibar.
Mchezaji Mersiana Samuel (GD) wa timu ya Tamisemi akijiandaa kumrushia mpira golikipa wake Chuki Kikalao (GK) huku akichungwa kwa karibu na mchezaji wa Magereza Aveline Mihayo (GD) wa Magereza katika mchezo wa ligi ya Muungano ya Netiboli iliyofanyika jana katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambapo Tamisemi ilishinda magoli 56-31.

Kwa upande wa Magereza Tanzania, nayo imesaliwa na michezo mitatu ambayo ni dhidi ya Nyika, JKU na Mafunzo.

Matokeo ya michezo mingine iliyofanyika jana inaonyesha kuwa Mafunzo ya Zanzibar imeifunga Kampala magoli 54-36, Zimamoto imefungwa na Nyika Queens magoli 44-47, JKU imetoka sare na JKT Mbweni kwa magoli 49-49 na KVZ imeichapa Warriors magoli 58-31.
Mchezaji wa kati wa timu ya Magereza Tanzania Magreth Mwafuliwa akitafuta namna ya kumtoka Gloria Benjamin wa Tamisemi Queens katika mojawapo ya harakati za kugomea mpira katika mchezo kati ya Tamisemi na Magereza ambapo matokeo yalionyesha kuwa Tamisemi iliifunga Magereza magoli 56-31.

Bingwa wa mashindano hayo atapatikana tarehe 3 novemba, mwaka huu mara baada ya mchezo wa mwisho wa ligi kati ya Tamisemi Queens na KVZ ya Zanzibar utakapofanyika.

Post a Comment

0 Comments