NI MATOKEO YA SENSA, TWENDE TUKAJENGE NCHI

NA LWAGA MWAMBANDE

IDADI ya watu nchini imeongezeka kwa asilimia 3.2 kwa miaka 10 iliyopita kutoka watu 44,928,923 mwaka 2012 hadi kufikia watu 64,741,120 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la watu 19,812,197.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Vitabu vya Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 pamoja na Kitabu cha Muongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Hayo yamebainishwa Oktoba 31, 2022 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati akizundua matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Takwimu ambazo zimeonesha idadi ya wanawake ikiwa kubwa zaidi kuliko wanaume kwa asilimia 51 na asilimia 49, mtawalia.

Pia takwimu nyingine zilizotolewa ni idadi ya majengo ambapo Tanzania kuna jumla ya majengo 14,348,372, vituo vya kutolewa huduma za afya vikiwa 10,067 (zahanati 7,089, vituo vya afya 1,490 na hospitali 688).

Kwa upande wa elimu Tanzania ina jumla ya shule 25,626 ambapo shule za msingi ni 19,769 na shule za sekondari ni 5,857. Baada ya matokeo ya mwanzo, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema sasa twende tukajenge nchi, endelea;

1:Twende tukajenge nchi, tumekwishahesabiwa,
Tusikaekae bichi, na upepo kupepewa,
Wala si kwenye makochi, runinga kuangaliwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

2:Twende tukajenge nchi, sisi tunategemewa,
Sisi ndio wananchi, siyo wa kusingiziwa,
Kazi kuweka makenchi, nyumba ziweze kaliwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

3:Tutumie hata winchi, tuweze kufanikiwa,
Tuko wengi yetu nchi, tulivyo tumeelewa,
Ile hauchi hauchi, kumeshapambazuka wa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

4:Inakua hii nchi, idadi tumesomewa,
Kwamba sisi wananchi, idadi metambuliwa,
Tushike jembe na mchi, kazi tunazielewa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

5:Rais wetu wa nchi, na yeye tumeambiwa,
Taarifa mbichimbichi, hizo tumeshasomewa,
Kazi za kujenga nchi, mipango yaandaliwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

6:Ni matokeo ya Sensa, tumekwishatangaziwa,
Haya yaleta hamasa, kwamba yende kutumiwa,
Ni kazi siyo anasa, jinsi yatavyotumiwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

7:Wote tulioshiriki, zoezi kuhesabiwa,
Kazi yetu imetiki, idadi tumeambiwa,
Takwimu twazimiliki, zinafaa kutumiwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

8:Idadi twajulikana, kama tulivyosomewa,
Makazi yajulikana, idadi tumeambiwa,
Sasa kazi kupambana, tuweze kufanikiwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

9:Hongera kwa serikali, hili limefanikiwa,
Na watu kila mahali, nyote mlohesabiwa,
Idadi mefika mbaali, tunaacha kukisiwa,
Kwa sasa tumejijua, mipango iwe sawia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments