Maonesho ya Saba ya Kilimo Mseto yaanza mkoani Mara, Serikali yasisitiza ushirikiano

NA FRESHA KINASA

SERIKALI imesema, itaendelea kushirikiana na mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na kilimo hapa nchini kusudi sekta hiyo iweze kuendelea kuinua maisha ya Watanzania.

Pia imesema itazidi kuwatumia watafiti kusudi watumike kufanya tafiti zenye tija zitakazosaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili kutatua changamoto zao.
Hayo yamesema Novemba 24, 2022 na Mkurugenzi wa Idara ya matumizi na Mipango ya Ardhi ya Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Mhandisi Juma Mdeke wakati akifungua Maonesho ya Saba ya Kilimo Mseto yanayofanyika katika Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma mkoani Mara yakiwa na kauli mbiu isemayo 'Bayoanuai kwa usalama wa chakula na kipato'.

Ambapo wakulima, wafugaji na wadau mbalimbali wa kilimo mseto wanashiriki katika maonesho hayo ya siku tatu.

Mhandisi Juma amesema sekta ya kilimo ina mchango mkubwa wa maendeleo hapa nchini, hivyo serikali itashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi na mashirika ya nje ambayo yamekuwa yakisaidia kuimarisha sekta hiyo katika kuleta ufanisi.
Pia amelipongeza Shirika la Vi-Agroforestry kwa kuwa na mchango mzuri katika sekta ya kilimo kupitia kilimo mseto.

Amesisitiza wakulima wafundishwe njia bora ya kutumia eneo dogo la ardhi kwa kulima mazao machanganyiko kisasa, kwani faida yake ni kubwa katika kuongeza upatikanaji wa mazao mengi.
"Kama wizara tupo tayari kuwa daraja ama chombo cha kuwakutanisha wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya kilimo na kutoa ushirikiano wote muhimu unaotakiwa,"amesema Mhandisi Juma.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Vi-Agroforestry, Thaddeus Mbowe hapa nchini amesema lengo la maonesho yao ni kueneza ujumbe kuhusu mchango wa kilimo mseto katika kuboresha hali ya maisha ya watu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Malengo mengine mahususi ni kuwaleta pamoja washiriki wa sekta ya umma na sekta binafsi zikiwepo taasisi mbalimbali na mashirika yasiyo ya kiserikali wanaofanya kazi katika mapambano ya kupunguza mabadiliko ya tabia nchi na hifadhi ya mazingira.

Pia, kuongeza uelewa kuhusu baiyonuai umuhimu wa kuitunza na vile vile ushiriki wa kilimo mseto katika kuitunza bayonuai. Sambamba na kushiriki katika uchechemuzi wa kudai mkakati na mpango kazi wa kitaifa wa bayonuai ambao ulikwisha muda wake 2020.

Mbowe amesema, tangu shirika hilo limeanza kazi hapa nchini mwaka 1994 limefanikiwa kutoa ruzuku zaidi ya shilingi Bilioni 12 kwa mashirika ya wakulima. Na pia kupanua miradi mbalimbali na kupata ushirikiano mzuri kutoka serikalini.
"Maonesho haya yanahusisha sehemu tatu ambapo wadau wa kilimo mseto kuonesha teknolojia na bidhaa zao mbalimbali, sehemu ya pili kuonesha mashamba ya mfano ambayo yanaonesha kuwa katika ngazi ya mkulima mdogo mdogo yote tunayoyahubiri kwa maneno yanawezekana kwa vitendo. Pia, tunalo banda la uchechemuzi wa masuala au sera mbalimbali hujadiliwa humo vikiambatana na tafiti mbalimbali,"amesema Mbowe.

Amesema, changamoto kuu ni kutambua kuwa kilimo mseto ni suala mtambuka na hivyo utekelezaji wake unahitaji ushirikishwaji wa wadau wengi wa maendeleo zikiwepo wizara na sekta mbalimbali.

Pamoja na uratibu kwani ni changamoto ambayo amesema ni tishio la utekelezaji wa kuweza kufaidi matunda ya kilimo mseto.
Kwa upande wake Rais wa Bodi ya Shirika la Vi- Agroforestry, Charlotta Seczepan Owski amesema kuwa, shirika hilo linajishughulisha na kupambana na umaskini na mabadiliko ya tabia nchi kupitia kilimo mseto.

Ambapo amesema limejizatiti kwenda maeneo ya ukame kwani yanaathirika zaidi huko mbeleni na pia litaendelea kutanua maeneo ya utekelezaji wa kazi zao hapa nchini na maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Ameongeza kuwa, shirika hilo litaendelea kutilia mkazo maeneo ambayo miti inasitiwa binadamu pia anastawi sambamba na kuhimiza kilimo mseto kwa kupanda miti na kuwekeza katika ufugaji.
"Tangu mwaka 1983 tumefanikiwa kuotesha miti milioni 148 maeneo mbalimbali hapa Tanzania na kubooresha maisha ya watu wapatao milioni. 2.4 kupitia kilimo mseto,"amesema.

Dkt.Noel Komba ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara amesema, Mkoa wa Mara bado unakabiliwa na uzalishaji mdogo wa chakula, hivyo shirika hilo linawajibu wa kuendelea kushirikiana na wakulima mkoani Mara kuwapa elimu na mbinu bora za kulima kwa tija sambamba na kutunza mazingira kwa kujiepusha na ukataji miti, ulimaji katika vyanzo vya maji na shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji.
Ameongeza kuwa, Mkoa Mara umepokea tani 500 za mahindi ambapo bei ya sokoni ni shilingi 1400 kwa kilo. Lakini kwa mahindi yanayouzwa na Serikali (NFRA) kwa punguzo la bei ni shilingi 920.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news