Mbunge Silaa aahidi kushirikiana na wenzake kuhakikisha tasnia ya habari inakuwa na sheria rafiki nchini

NA DIRAMAKINI

MHESHIMIWA Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga mkoani Dar es Slaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kushirikiana na wabunge wenzake katika kuhakikisha tasnia ya habari inakuwa na sheria rafiki zinazotekelezeka.
Silaa ametoa kauli hiyo leo Novemba 8, 2022, wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) jijini Dodoma.

TEF na CoRI wamekutana na mbunge huyo ili kuzungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye Sheria ya Habari ya mwaka 2016 vinavyokandamiza uhuru wa habari nchini.

‘‘Mimi na wabunge wenzangu tutashirikiana. Dunia imebadilika na hatuwezi kubaki hapa tulipo,"amesema Jerry na kuongeza, ‘‘nitazungumza na wenzangu na kisha tutaona namna ya kufanya.’’
Kikao hicho nje ya viwanja vya Bunge, kimeongozwa na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF ambapo amemweleza Jerry kwamba, Sheria ya Habari ya mwaka 2016 imeweka mazingira makubwa ya kumuhofisha mwandishi wa habari.
Na kwamba, ndani ya sheria hiyo kuna vipengele mbalimbali kwa undani wake, vinaua tasnia ya habari akitolea mfano kipengele kinachompa nguvu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kufungia chombo cha habari kwa namna anavyoona inafaa.

‘‘Katika safari ya mabadiliko haya, tumeungana na taasisi zote za habari ili kuwa na kauli moja. Tumeunganisha nguvu ili kufikia lengo,"amesisitiza.

James Marenga, Mjumbe wa CoRI kutoka Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania amemweleza Jerry kwamba, tasnia ya habari haina tofauti na tasnia nyingine nchini katika utendaji kazi.

Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea amesema, ikiwa mawakili wanatengeneza taratibu zao na kuzifanya kuwa rejea katika kazi zao, inashindikanaje wanahabari nao wakajiwekea utaratibu wa ‘kujihukumu’ kama ilivyo tasnia nyingine?.

‘‘Mimi ni mwanasheria, katika taasisi yetu tulitengeneza cord of conduct wenyewe na hizo ndio zinatuongoza, ni busara na wanahabari wakawa na utaratibu wao kisheria unaosimamiwa na wenyewe katika kuhakikisha maadili ya uandishi wa habari yanafuatwa,’’ amesema.
Jessy Kwayu, Mkurugenzi Mkuu wa Media Brains Inc Ltd amesema, Sheria ya Habari ya mwaka 2016 ilipitishwa katika mazingira ambayo si rafiki.

‘‘Vipengele 19 vya sheria hiyo vilijaribiwa kwenye sheria za nchi, vikaonekana kutoingia katika mizani ya kisheria,’’ amesema Kwayu.
Rose Reuben, Mkuu wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) amesema, kwa mazingira ya sasa, waandishi wanashindwa kuandika habari kwa uhuru.

Hayo yanajiri ikiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro alipokutana na uongozi wa TEF na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) hivi karibuni jijini Arusha alisisitiza wakati ni sasa.

Mheshimiwa Waziri alisema, kama kuna wakati mzuri wa kulisukuma suala la kubadili sheria za habari ni sasa.

“Rais tuliye naye sasa, Mheshimiwa Samia (Suluhu Hassan) ameonesha moyo na nia kubwa ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini.

“Kwa sasa mazingira ni mazuri na yanaruhusu. Lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, maana mkisubiri miaka 10 ijayo, huwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,”amesema Dkt.Ndumbaro.

Rais Samia tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news