Majimaji FC,Njombe Mji FC zapokwa alama 15 kila moja, faini juu

NA DIRAMAKINI

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Novemba 4, 2022 ambacho kilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi kimefanya maamuzi mbalimbali.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 8, 2022 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
 
 Mechi Namba 74: Geita Gold FC O-1  Young Africans SC

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwamuzi wa kati, Florentina Zabron amepelekwa Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema Sheria 17 za mpiga wa miguu katika mchezo tajwa hapo juu.

Aidha, Kamati ya Waamuzi ya TFF italitazama kitaalamu tukio la pigo la penalti ya Klabu ya Young Africans dhidi ya Geita Gold katika dakika ya 18 ya mchezo kabla ya kuishauri kamati kwa kuzingatia Kanuni ya 42:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti waamuzi.

Ligi ya Championship: Mechi Namba 46:Pamba FC 1-0 Pan African FC

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Pan African imepewa onyo kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye mkutano wa maandalizi ya mchezo (MCM) kwa dakika tano huku pia ikichelewa kwenye chumba chao cha kuvalia wakati wa mapumziko jambo lililosababisha kipindi cha pili cha mchezo tajwa hapo juu kuchelewa kuanza kwa dakika tano.

Adhabu hiyo kwa mujibu wa taarifa hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 17:2 (2.2) na 17(33 na 60) ya Championship kuhusu taratibu za mchezo.

Mechi Namba 55: Fountain Gate FC 1-0 Ndanda FC


Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la mashabiki wake kwenda kusimama nyuma ya goli la klabu ya Ndanda na kuanza kumtolea lugha za matusi golkipa wa timu hiyo, wakimtuhumu kuwa ameweka kitu golini ambacho kinazuia Fountain Gate kupata ushindi.

Aidha, mashabiki hao walimshinikiza mtoto muokota mipira (ball kid) kwenda golini na kuchukua chupa ya maji ya golikipa huyo kisha kuitupa nje.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.
 
First League;-Mechi Namba 68 kati ya Mbao FC na Mwandui FC ambazo ziliibuka kwa ushindi wa 1-1

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, klabu za Mbao na Mwadui zimepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).Mbao waliwakilishwa na maafisa wanne huku Mwadui wakiwakilishwa na maafisa wawili badala ya watano walioainishwa kikanuni.

Aidha, katika kikao hicho, Mwadui walikuwa na seti moja ya jezi za wachezaji wa ndani bila jezi za magolikipa wala soksi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2 (2.2) na 18:60 ya First League kuhusu taratibu za mchezo.

Wakati huo huo, kamati imemfungia michezo mitatu mtunza vifaa vya klabu ya Mbao, Bw.Chriss Shimbe baada ta kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwa kosa la kurudia mara kadhaa kupinga maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo.

Aidhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:21 ya Fist League kuhusu udhibiti wa viongozi.

Mechi Namba 6B:Cosmopolitan FC dhidi ya Majimaji FC


Klabu ya Cosmopolitan imepewa ushindi wa alama tatu na mabao matatu huku klabu ya Majimaji ikitozwa faini ya shilingi milioni mbili na kupokwa alama 15 katika msimamo wa ligi kwa kosa la kushindwa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo na baadae Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu,

Maafisa wa mchezo huo walisubiri dakika 30 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni kabla ya kuahirisha mchezo huo baada ya klabu ya Majimaji kutoonekana uwanjani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 31:1 (1.6) ya First League kuhusu kutofika uwanjani.

Mechi Namba 10A:African Lyon FC dhidi ya Njombe Mji FC

Klabu ya Africa Lyon imepewa ushindi wa alama tatu na mabao matatu huku klabu ya Njombe Mji ikitozwa faini ya shilingi milioni mbili na kupokwa alama 15 katika msimamo wa ligi kwa kosa la kushindwa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo na baadae Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu.

Maafisa wa mchezo huo walisubiri dakika 30 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni kabla ya kuahirisha mchezo huo baada ya klabu ya Njombe Mji kutoonekana uwanjani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 31:1 (1.6) ya First League kuhusu kutofika uwanjani.

 Mechi Namba 10B:Stand United 2-1 Rhino Rangers FC

Klabu za Stand United na Rhino Ranger zimepewa onyo kwa kosa la kuwakilishw ana maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,timu hizo ziliwakilishwa na maafisa wanne kila mmoja badala ya watano walioainishwa kikanuni.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2 (2.2) na 18:60 ya Fistr League kuhusu taratibu za mchezo.

Mechi Namba 11B:TMA FC 2-0 Alliance FC

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Klabu ya Alliance imepewa onyo kwa kosa la kutoingia kwenye chumba cha kuvalia katika mchezo tajwa hapo juu kwa kile walichoeleza kuwa walisahau ufunguo wa mlango wa chumba hicho ambao walikabidhiwa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:20 na 18:60 ya First League kuhusu taratibu za mchezo.

Post a Comment

0 Comments