MENGINE NGEKEWA

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWAKA 1992 nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Tambaza, Dares Salaam ilipata ugeni wa mwanamuziki Kanda Bongo Man mwenye asili ya Kongo, mimi na wezangu kadhaa tulitoka shuleni kwenda katika onesho hilo viwanja vya Mnazi Mmoja pale Anatouglou upande wa Mnara wa Mashujaa na wakati huo mabasi yanayoenda nje ya Dar es Salaam yalikuwa yakipakia na kushusha abiria hapo na Kisutu.
Ndani ya kiwanja hicho kuna sehemu kama jukwaa na kuna maji yanazunguka na kuna mwanasesere ya ngoma inapigwa, sifahamu kama mandhari hiyo hadi leo kama ipo. 

Viwanja hivi wakati huo vilikuwa havina uzio tangu shule ya msingi Mnazi Mmoja, Mnazi Mmoja Hospitali hadi Mnara wa Mashujaa.

Watu walikuwa wengi sana wanamgonja Kanda Bongo Man katika Onesha la bure, Mwanakwetu bure aghali! Nia ya onesho hilo lilikuwa kuhamasisha watu waende katika onesho alilokuwa akifanya jioni yake katika ukumbi maalumu na baadaye mwanamuzi huyo aende mikoa mingine ya Tanzania.

Hapo Anatouglou nilikutana na dada zangu wawili Helena Ntinda na Happiness Mitimingi waliokuwa wanasoma sekondari ya Zanaki. 

Nilipowaona tu niliwasalimia,nakusema nawaona mmpendeza! Wakasema kaka wapi! Kawaida tu. Nikawaambia nayaona Marinda ya sketi zenu yamenyooka ! Wakacheka sana, Helena akasema kaka marinda yepi ?. Nikamjibu hayo marinda ya V iliyogeuka, Wakaniambia, kaka sisi dada zako, utani waachie wengine, nikawajibu sawa.

Mwanakwetu hawa wanafunzi wa Zanaki tangu enzi shule hii ni ya wasichana ilikuwa na marinda mbele ya sketi yaliyochanua kwa chini karibu na pindo la sketi ya sare zao linalofanana na herufi V iliyegeuka, sina hakika kama marinda haya kama bado yanaruhusiwa mabinti zetu wa sekondari ya Zanaki kushona katika sketi zao. Marinda haya yalinivutia mno wakati huo na ndiyo maana hadi kesho ninayakumbuka.

Mungu bahati dada zangu hawa wawili Wafipa: binti Ntinda na binti Mitimingi walikuwa na miili iliyojengeka vizuri sana, walikuwa pia warembo sana na sketi hizo ziliwapendeza zaidi. Mjini palikuwa pazuri kweli kweli Mwanakwetu.

Kumbuka tupo Anatouglou, Bongo Man akafika akafanya onesho lake fupi kwa dakika kama kumi akiimba nyimbo mbili mfululizo Inde Monie na lisa, onesho lilipokwisha mimi na dada zangu hawa tuliondoka zetu na kurudi nyumbani Mbagala.

Kwa nini leo hii nimekumbuka kisa hicho? Novemba 10, 2022 katika mitandao ya kijamii ilisambaa filamu fupi ikionesha vijana wawili mtanashati na mrembo wakicheza wimbo wa Muchana wa mwanamuziki huyu. 

Mtashati alivaa shati la kijivu, suruali nyeusi, viatu vyeusi na akiwa amenyoa upara naye mrembo alivalia gauni la kijivu, viatu vyeusi kichwani kwake akisuka rasta ndefu nzuri nyeusi. 

Kubwa kuliko yote wakicheza huku wakiendana na midundo ya vyombo vya wimbo huo. 

Kwa sekunde chache vijana hawa wakionesha umahiri mkubwa wa kuucheza wimbo huo uliotolewa kwa mara ya kwanza katika mtindo wa Zouk mwaka 2010. 

Filamu hiyo fupi ilinishawishi kuutazama wimbo huo katika filamu halisi. Nikiona ubora wake kwa waimbaji na hata upigaji wa vyombo hivyo.

Safari yangu haikuishia hapo nilitazama onesho la mwanamuzi huyu alilofanya huko The Emperors Palace Johannesburg Afrika ya Kusini niliona waimbaji wamebadilika, sauti zimebadlika, upigaji vyombo umebadilika na hata Kanda Bongo Man mwenyewe amebadilika hadi sauti yake, sivyo kama alivyoimba kwa ubora wake wa awali. Nikatazama hata waliofika ukumbini walikuwa watu wa rika fulani hakuna vijana wengi.

Hata hawa waliokwenda ukumbini si kwamba Kanda Bongo Man alikuwa anaimba vizuri la sana la hasha walikwenda kwa heshima yake aliyoijenga wakati huo alipokuwa anaimba vizuri. Wengi ninaamini walienda kukumbuka enzi zao na kumuenzi mwanamuziki huyu.

Wapigaji wa vyombo hivi wa onesho hili la Johnnesburg walionekana wanajitahidi kupiga kama wimbo huo ulivyopigwa kwa mara ya kwanza lakini walishindwa kufikia viwango kwa kuwa hawakuwepo wimbo huo siku unatungwa na kurekodiwa kwa mara ya kwanza. 

Pengine waliorekodi awali walishafariki dunia, wengine wamelala vitandani wakiwa wagonjwa, wengine walishaachana kabisa na shughuli za muziki.

Nilitazama filamu nyingine ambayo Kanda Bongo Man alikuwa katika onesha la moja kwa moja katika mji mwingine, hali ilikuwa vilevile akiimba kidogo sana, hakuwa na maneno mengi, akicheza taratibu sana sivyo kama zamani lakini alisaidiwa sana na vijana wadogo wawili wanenguaji wa wakiume na wakike ambao kwa hakika kwa umri wao ilinionesha wazi kuwa hawakuwepo wakati wimbo huo unatolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 lakini walicheza vizuri sana.

Mwanakwetu nikapata maswali mengi Kanda Bongo Man umri umesonga, muziki wake unapendwa basi kwanini asimchukue mtoto wake aifanye kazi hiyo? Nikapata swali lingine Je huyo mtoto wake anaupenda muziki ? Hata kama anaupenda je anacho kipaji cha kuweza kuimba kama alivyokuwa yeye? Je Kanda Bongo Man aliingia muziki kwa kuwa baba yake alikuwa mwanamuziki?.

Nikapata majibu mengi kuwa mwamuziki huyu anaweza kufanya hivyo kwa kuwa rasimali anazo lakini Je mtoto wake ataweza kuonesha umahiri katika jukwaa la muziki kama alivyokuwa yeye? Je mtoto wake anaweza kustahimili misukosuko ya jukwaa la muziki?

Jukwaani kuna mengi, maharamia na mahasidi wanaweza wakamtwanga konde moja maridadi na takatifu, mtoto huyu anaweza kusema, aha jamani mniache mie nifanye shughuli zangu kazi hii ilikuwa ya baba, mimi nilingia basi tu? Ngoja nirudi Ufarasa nikapumzike.(Ngoja nirudi Ufaransa nikapumzike.)

Nikawakumbuka wale dada zangu wawili wa Kifipa: binti Ntinda na binti Mitimingi waliopendeza mno na marinda ya sketi zao shuleni. Dada zangu hawa sasa inawezekana wamezaa mabinti zao, leo hii wakitazama picha za mama zao wakati wakisoma zitawavutia sana, inawezekana mama zao wakatamani mabinti zao wawe kama wao lakini je wanaweza kupendeza kama mama zao enzi hizo? Mwanakwetu hilo abadani kwa maana ya mama si ya mtoto na ukipata wewe shukuru Mungu mengine ni ngekewa.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Post a Comment

0 Comments