BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 52

NA WILLIAM BOMBOM 

Ilipoishia...Kwa namna yeyote alipaswa kusakwa mpaka apatikane, hawezi kuzuia kazi zetu za usiku kwa zindiko lake la ...

Endelea

Ndugu msomaji siku hiyo tulimwaga dawa za kila aina kuweza kujua wapi fundi huyo alikuwa amekwenda. 

Kila tulipomwaga dawa zetu kwenye vyungu au vibuyu badala ya kutokea picha ya yule fundi kulitokea moshi mweusi tii.
Katika taaluma ya kichawi moshi mweusi humaanisha, giza yaani mtu huyo hakuwa hai. Hata hivyo hatukuridhika na majibu hayo, tuliamua kurudi kambini kwetu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Tulipofika kambini tulikusanyika kwenye jengo maalumu kwa ajili ya shughuli kama hiyo. 

Tulimwaga madawa ya aina mbalimbali kwenye vyungu ili kubaini alipokuwa fundi huyo, siku zote wachawi huwa hawapendi kumuacha hai mtu yeyote anayezuia njia zao kwa zindiko. 

Kwa namna moja au nyingine fundi huyo alipaswa kupatikana, haijalishi awe hai au amekufa. Baada ya kuchanganya aina mbalimbali za madawa, tulifanikiwa kumuona akiwa kwa mganga. Bahati nzuri mganga huyo tulikuwa tukimfahamu.

Kwa kuwa ilikuwa ni usiku wa kuelekea saa tisa, tuliamua kumuacha siku hiyo ili kesho yake asubuhi tukamtembelee. Mganga huyu alijulikana kwa jina la Ulasohoye. 

Ndugu msomaji mganga huyu ni miongoni mwa waganga waliokuwa wakiingilia sana kazi zetu. 

Kwa kifupi ni aina ya waganga vimbelembele sana, kila mara alikuwa akituharibia mipango na kazi zetu. 

Mbaya zaidi hatukuwahi kumfuatilia maana kila alipoharibu, tulimuacha hatukuchukua maamuzi magumu dhidi yake. 

Nadhani kwa kuwa alikuwa ni mganga alikuwa amejichanja dawa ya kigwishangh'olo. 

Hii ni aina ya dawa ya kukatisha tamaa dhidi ya maadui zako, yaani mtu anakuchokoza lakini ukitaka kumlipa kisasi moyo wako unavunjika kufanya maamuzi hatimaye unamsamehe.

Dawa za namna hizi hufanyika sana kwa waganga, hufanya hivi ili kutufanya sisi wachawi kutomfuatilia mganga huyo katika shughuli zake. 

Pia dawa hizi hufanywa kwenye kesi za madai, yaani mtu unamdai kitu mwisho wake madai hayo yanayeyuka kwa mdai kupuuzia tu. 

Pia hufanyika kwenye kesi za mauaji, mtu anafanya mauaji ushaidi unapatikana lakini mwisho wa kesi hiyo inayeyuka kiaina aina. 

Nadhani mganga huyu alikuwa na dawa hii, maana yapo mambo makubwa ambayo amewahi kutufanyia mganga huyo. 

Achilia kambi yetu ya kichawi, mganga huyu alikuwa gumzo hata kwa wachawi wenzetu katika kazi zao.

Nakumbuka sakata moja aliwahi kulifanya kwa mshiriki wa kambi yetu lilituuma sana lakini hatukuchukua maamuzi. Sakata lenyewe lilikuwa hivi.

Miezi michache iliyopita kulitokea sakata la ajabu la mama mmoja mshirika mwenzetu dhidi ya mganga huyo. 

Mama huyo amebahatika kupata watoto sita, watano ni wa kike na mmoja wao ni wa kiume. 

Mtoto wake huyo hakuwahi kujua kama mama yake ni mchawi. Siku zote ni vigumu katika familia kutambua kama nyumbani kwenu kuna mchawi. 

Mara nyingi nyumba ya kichawi huwa ina mazindiko makubwa hivyo ni ngumu kujua. Nyumba ya kichawi huwa haifanyiwi uchawi kwa kuwa mchawi huyo ni mshirika mwenzao hivyo hakuna mchawi ambaye anaweza kwenda kwa mchawi mwenzake kumloga. 

Labda baina yao kuwepo mvutano ambao hauna suruhu japo ni vigumu maana huwa kuna vikao vya usuluhishi vya kichawi. Kijana wake huyo wa kiume alimpenda mpaka akatamani kumrithisha uchawi. Mizimu ya kijana huyo iligoma kupokea uchawi, kila alipojaribu kutaka kumrithisha. Kumbuka zipo njia tatu za kujifunza uchawi, njia ya kwanza ni mtoto anapozaliwa tu huwa ana alama fulani kwenye kiganja chake. 

Alama hizo hufanana kwenye kiganja cha kushoto na zile za kiganja cha kulia.

Alama hizo ni rahisi kwa mchawi kuzigundua kwa mwanae, kama mtoto ana alama hizo na unahitaji baadae awe mchawi huwa anashikishwa mzizi fulani wa kichawi. 

Hivi ndiyo vitoto ambavyo huanza kusumbua ingali bado vidogo, mara nyingi wachawi wa namna hii ni hatari sana maana uchawi wao ni wa kurithi kwenye damu na siyo kujifunza. 

Wachawi wa namna hii huwa mizimu yao ni ya kichawi muda wote, ndiyo huja kuwa viongozi wa wachawi baadaye maana wao uchawi upo damuni.

Aina ya pili ya uchawi ni ile ya mtu kujifunza kupitia kwa ndugu zake mara nyingi kafara yao huwa haina mashariki makari, wachawi wa namna hii ni wale kwao kuna mlolongo wa kichawi. 

Aina ya tatu ni ile ya wenzangu na mimi, yaani mtu kwao hakuna asili ya uchawi, hawa hujifunza kwa gharama kubwa. Hutoa kafara za watoto, waume, wake, mama au baba zao.

Katika njia zote hizo tatu kwa kijana huyo ilishindikana hivyo mshirika mwenzetu aliamua kuachana naye. 

Ukiona nyumbani kwenu mzazi wako anapenda kukuita wewe ni mvuta bangi, alihali huwa hautumii bangi basi tambua kuna kitu hapo alikishindwa kwako. 

Kama ilivyo kawaida kijana huyo alibahatika kuwa na rafiki wa kike, walipendana sana na binti huyo. Ikafikia muda wakataka kuoana. 

Lakini mshirika mwenzetu hakutaka kijana huyo amuoe binti huyo, maana binti huyo naye alikuwa mchawi kwenye kambi ndogo mji wa majengo.

Wachawi ni watu wa ajabu sana, mara nyingi hawapendi watoto wao wa kiume kuoa wachawi. 

Hutumia njia zozote kuhakikisha ndoa hiyo inapeperuka na kusambaratika kabisa. Mama huyo alipogundua uhusiano wa kijana wake na yule binti mchawi alimuita kijana wake. 

Alijaribu kumhadaa kwa kumwambia kuwa binti huyo siyo mzuri pamoja na familia yake. Kama ilivyo nguvu ya mapenzi kijana hakumuelewa hata kidogo mama yake. 

Maana mama hakuthubutu kuusema ukweli unaomfanya kumkataa binti huyo. Mama huyo aliwahi kunishirikisha THE BOMBOM katika sakata hilo, alitamani hata tumuue binti huyo lakini sheria za kichawi zilikuwa zinamlinda binti huyo mchawi.

Siku zilipita huku mapenzi ya kijana na binti huyo yalishamiri, kijana hakusikia la mnadi swala wala la mhadhini. 

Alikuwa kafa kaoza kwa binti huyo, mara nyingi unapoona mzazi wako anakuzuia kufanya mahusiano na familia fulani chunguza. 

Huwa kuna siri kubwa ndani yake, unaweza ukawa unakatazwa labda binti au kijana huyo ni mchawi. 

Ama unaweza ukawa unakatazwa kwa kigezo cha kuwa binti huyo ni damu yako yaani dada yako, maana wazee nao wana mambo mengi. 

Kijana huyo aliendeleza uhusiano kwa binti huyo mpaka mji mzima wa majengo wakatambua mahusiano hayo. 

Kwa upande wa binti mahusiano hayo yalikuwa na faida kubwa, maana kupitia uzao wao ingekuwa rahisi kwa watoto wao kurithi uchawi wa pande zote mbili. 

Siku moja asubuhi na mapema mama huyo mshirika mwenzetu alimuita kijana wake chumbani kwake. Mama alionekana kuwa na hasira mithili ya nyuki, alikuwa kadhamiria kumwambia ukweli mwanae.

Kijana aliitikia wito kutoka kwa mama yake, siku hiyo mama huyo alikuwa tofauti na asili yake. Mama alionekana kuwa mbogo kwa mara ya kwanza kujana akawa muoga kwa mama yake. Mama alianza kwa kumwambia kijana wake. "Mwanangu kumbuka wewe ni uzao wangu..."

Ndugu msomaji endelea kufuatilia kisa hiki ili ujue hatima yake. Je, nini kilimpata kijana huyo.

Jiandae kusoma simulizi ya KANISA LA KICHAWI na KABURI LA RAIS WA HOVYO zitakazokuwa zinatoka mara mbili mbili kwa juma.

ULAKOZE CHANE!
THE BOMBOM

Post a Comment

0 Comments