MWALIMU MUUZA VISHETI

"Mwanakwetu haya mambo unayajua vizuri sana tangu tunasoma. Unakumbuka mwalimu hasahihishi madaftari yetu hadi visheti vyake vyote vinunuliwe? Mapumziko utanunua ice cream, maandazi na mihogo lakini pesa ya kisheti cha mwalimu lazima uiweke ili daftari lako lisahihishwe vizuri. Vinginevyo wewe kila siku daftari lako halitosahihishwa kamwe. Nikionekana katika sherehe watasema jamaa kaacha kituo cha kazi, sasa yupo katika sherehe tu, si mnamuona?".

 
NA ADELADIUS MAKWEGA

MWISHONI mwa mwezi Oktoba 2022, nilikuwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam, hapo nilikutana na mwanasiasa mmoja kijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuzungumza naye mambo mengi sana.

Kijana huyu amefanya kazi mbalimbali, kwa maoni yangu nina hakika katika kila nafasi aliyowahi kupewa amezitendea haki, japokuwa anakutana na changamoto nyingi.

Kwa maoni yangu ya hakika pahala ambapo kuna misuguano mingi ndipo maendeleo ya wengi yanaweza kupatikana. Sehemu isiyo na misuguano moto hauwezi kuwaka na mara zote watu watakula chakula kibichi.

Katika ulimwengu wa leo, Je yupo anayependa kula chakula kibichi ? Mwanakwetu hapana ndilo jibu lake. Misuguano lazima iwepo kwa manufaa ya wengi.

Kwa bahati nzuri kijana huyu mahiri niliyekutana naye binafsi namfahamu sana tangu akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bunge, huku mimi nilikuwa nikidoea kusoma hapo kwa kufanya mitihani ya majaribio kila Jumamosi, kwa hisani baba yangu ambaye alikuwa mwalimu wa shule hii kongwe ya umma.

Shule hii aliyosoma kiongozi huyu tangu enzi ilikuwa na wanafunzi wengi ambao baba na mama zao wakiwa viongozi serikalini na kwa wakati huo kupata nafasi ya kuingia darasa la kwanza ilikuwa kazi kidogo.

Ndugu yangu huyu tangu wakati huo hulka yake ya ukweli, ya kueleza jambo wazi wazi alikuwa nayo. Binafsi sikuwa jirani naye, kwani kazi yangu ilikuwa ni kwenda kufanya mitihani hiyo na kuondoka zangu, mitihani yangu niliyoifanya nilikuwa napewa jumamosi inayofuata kwa hisani ya baba.

Shule hii aliyosoma ndugu yangu huyu ilikuwa na watoto wengi wa viongozi wakiwamo hata watoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Ali Hassan Mwinyi, sitaki kujadili tabia zao, hulka zao na hata majina ya watoto hao wa viongozi waliosoma wakati huo maana leo hilo siyo ajenda yangu, lakini huyu jamaa alisoma nao.

Binafsi sifahamu ndugu huyu aliwezaje kusoma shuleni hapo? Nadhani alipokuwa analelewa wakati huo jijini Dar es Salam palikuwa nyumbani pa mkubwa.(Sitaki kuingia ndani katika hili kwa kuwa siyo ajenda yangu ya leo.)

Kumbuka msomaji wangu nipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, niko na ndugu yangu huyu, sasa akaniuliza habari za mwalimu wake, nikamjibu hajambo na kumpatia nambari yake ya simu.

Akampigia simu lakini mwalimu hakupokea simu hiyo na hilo likatupa mafasi tukaendelea na mazungumzo yetu.

Nikaulizwa Mwanakwetu mbona katikati ya jiji leo hii kulikoni ? Una biashara hapa Posta? Nikamjibu nitoe wapi kaka! Nikasema hapa kuna kazi moja naifanya, nikualike ushiriki? Akacheka sana, halafu akasema kaka unanitakia mema? Akasema,

“Mwanakwetu haya mambo unayajua vizuri sana tangu tunasoma. Unakumbuka mwalimu hasahihishi madaftari yetu hadi visheti vyake vyote vinunuliwe? Mapumziko utanunua ice cream, maandazi na mihogo lakini pesa ya kisheti cha mwalimu lazima uiweke ili daftari lako lisahihishwe vizuri. Vinginevyo wewe kila siku daftari lako halitosahihishwa kamwe. Nikionekana katika sherehe watasema jamaa kaacha kituo cha kazi, sasa yupo katika sherehe tu, si mnamuona? Kama yale yale ya mwalimu muuza visheti. Wanafunzi kuepusha maneno unakuwa na pesa ya kununua visheti vya mwalimu”

Nikacheka sana nikauliza Je visheti vyao vimechomwa vizuri? Je vina sukari ya kutosha? Je vimeiva? Jamaa akajibu, “Mwanakwetu jukumu lako ni kuvinunua tu ili mwalimu akusahihishie daftari lako, ukivila au ukivigawa shauri ni lako. Unapokuwa na damu ya kunguni, mwanakwetu ishi wa tahadhari.”

Nikamwambia hilo kweli kabisa, maana mwenye godoro akilala akishaumwa na kunguni na mwili wake kuanza kumuwasha asubuhi lazima aanze kuwasaka kunguni hao mmoja baada ya mwingine. Kama ataanika juani, atapiga dawa, atatumia maji moto kubwa ni kuwasaka kunguni tu katika godoro, kitanda au nguo zake.

Wakati mwingine unaweza ukatokea moto ukamuunguza mwenye godoro, godoro lenyewe na kunguni, hii ni hasara kwa wote. Lakini mwenye godoro anaweza kufariki watu wanagawana urithi wa vitu vya marehemu–magodoro/vitanda /nguo na samani zote. Kumbe hapo mnapogawana na wengine wanarithi kunguni. Hapo mwanakwetu inakuwa bahati ya kunguni kupata makazi mapya.

“Mungu kaumba viumbe vyake kaka, hata kunguni na wao wamo na ndiyo maana kuna bahati ya kunguni kama hii.” Ndugu yangu huyu akacheka sana.

Wakati wewe unasema una damu ya kunguni kumbuka pia kuwa kuna bahati ya kunguni ya kuwepo katika mgao wa samani za marehemu, ndugu huyu alikuwa anacheka zaidi.

Kweli ndugu yangu huyu alipomaliza mazungumzo haya alituaga na kwenda zake kurudi kituo chake cha kazi na mimi kubaki hapo nikikamilisha majukumu yangu, kubwa nilimkumbuka mwalimu wangu mmoja wa Kichaga aliyekuwa anauza visheti shuleni Mnazi Mmoja wakati huo na hasahihishi madafatari hadi visheti vyake viishe.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Post a Comment

0 Comments