Simiyu, Rukwa na Pwani wapigwa msasa Mpango wa Utayari unaomwandaa Mtoto kuanza Shule (SRP)

NA MWANDISHI WETU

WASHIRIKI 34 kutoka katika Mkoa wa Simiyu,Rukwa na Pwani wanashiriki mafunzo ya Mpango wa Utayari unaomwandaa Mtoto kuanza Shule (SRP) ambayo yatadumu kwa siku tano kuanzia Oktoba 31 hadi Novemba 4,2022 jijini Dodoma.
Washiriki ni Maafisa Elimu Taaluma Wilaya, Waratibu wa Elimu pamoja na walimu mahiri wa elimu ya awali kutoka katika Halmashauri 15 za Mikoa ya Pwani, Rukwa na Simiyu.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya awali waliopewa washiriki hao ili kuwajengea uwezo Wasaidizi Jamii wa Walimu wanaowafundisha watoto ambao hawajapata fursa ya kujiunga na Elimu ya awali kutokana na changamoto mbalimbali.
Mafunzo yamelenga kumjengea mtoto umahiri katika utambuzi pamoja na matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mawasiliano huku hadithi, michezo pamoja na nyimbo zikitumika kama nyenzo za kufundishia.

Watoto watapatiwa mafunzo kwa muda usiongupungua wiki kumi na mbili ambapo hadi kufikia sasa tayari mafunzo haya yameshafanyika kwa wiki nne.

Naye Mratibu wa mradi wa shule bora kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Winfrid Chilumba amesema kuwa mbali na muendelezo wa mafunzo haya, washiriki watatumia fursa hii kutoa mrejesho wa mafunzo ya utayari yaliyokwisha fanyika kwa watoto hao kwa wiki nne.
Naye Mwanaisha Abdul Omary mshiriki kutoka katika Halmashauri ya Mji Bariadi amesema mafunzo haya yana tija katika jamii kwakuwa yanampa mtoto fursa ya kupata elimu ya awali na kumuandaa kwa ajili ya Elimu ya Msingi hasa kwa watoto ambao wanaishi mbali na shule.

Post a Comment

0 Comments