Ndoto ya wana-Karatu yatimia baada ya hospitali ya wilaya kuanza kutoa huduma

NA SOHPIA FUNDI

NDOTO ya wana Karatu mkoani Arusha ya kusubiri huduma ya hospitali ya wilaya sasa imetimia baada ya hospitali hiyo kuanza huduma zake rasmi.
Wilaya hiyo ambayo haikuwa na hospitali ya wilaya tangu kuanzishwa kwake, wananchi wake walikuwa wakitegemea kupata huduma katika Hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania au Mount Meru mkoani Arusha imeanza huduma yake katika baadhi ya majengo huku ikiendelea na ukamilishaji wa shughuli zingine zilizobaki.

Akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo, mkuu wa wilaya hiyo, Dadi Kolimba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ambayo ilikuwa hitaji la Wanakaratu.
Pia amewashukuru wadau mbalimbali walioshiriki kuchangia wakati wa ujenzi na baadhi kutoa vifaa lengo likiwa ni kukamilisha ujenzi ili kutimiza ndoto ya Wanakaratu ambapo aliwaomba kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali, kwani bado inahitajika thamani ndani ya majengo hayo.

Akisoma taarifa ya wilaya mganga mkuu wa wilaya, Dkt.Lucas Kazingo alisema kuwa ujenzi wa majengo tisa ambayo yamekamilika kwa ajili ya hospitali yamegharimu shilingi bilion 2.6 ikiwa shilingi bilioni 1.6 imetolewa na Serikali na shilingi milioni 700 ikatolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kama ujirani mwema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Karia Magaro alisema kuwa kwa sasa wameanza kutoa huduma katika majengo mawili ya wagonjwa wa nje (OPD) na maabara kutokana na kutokamilika kwa thamani ndani ya majengo hayo.

Alisema kuwa, wataendelea kuanza huduma katika majengo mengine kadiri vifaa vitakavyopatika ambapo aliwaomba wadau kushirikiana katika kuunga mkono juhudi za serikali.
Magaro alisema kuwa, hospitali hiyo inatarajia kuwahudumia wagonjwa zaidi ya 290,000 ambao ni wakazi wa Karatu na nje ya Karatu pamoja na nje ya nchi kutokana na wilaya hiyo kuwa lango la utalii.

Post a Comment

0 Comments