Rais Dkt.Mwinyi aishirikisha Japan jambo kuhusu Sekta ya Uchumi wa Buluu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameiomba Serikali ya Japan kusaida uimarishaji wa miundombinu katika maeneo yanayogusa Sekta ya Uchumi wa Buluu.
Dkt. Mwinyi ametoa rai hiyo Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Misawa Yasushi, alyiefika kujitambulisha.

Amesema, Zanzibar imeweka kipaumbele Sera ya Uchumi wa Buluu katika kukuza uchumi wake, ambapo miongoni mwa sekta zinazohusisha sekta hiyo ni pamoja na Utalii na Uvuvi, hivyo akabainisha umuhimu wa kuwepo miundombinu bora.

Amesema, kupitia sekta ya uvuvi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo wavuvi wa Zanzibar kwa kuwapatia vifaa bora na nyenzo za kisasa, ikiwemo boti za uvuvi ili kuondokana na uvuvi wa kizamani unaotegemea vifaa duni, sambamba na kuwa na Bandari za Uvuvi pamoja na Vyumba vya kuhifadhi baridi (cold rooms).

Dkt.Mwinyi aliishukuru Serikali ya Japan kwa misaada mbalimbali inayoipatia Zanzibar kupitia sekta tofauti, ukiwemo ujenzi wa soko la Samaki Malindi na kubainisha hatua hiyo kuwa ni mwanzo mzuri katika uimarishaji wa sekta ya Uchumi wa Buluu nchini.

Aliishukuru nchi hiyo kwa uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Naye, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Misawa Yasushi ameshukuru ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar na kusema utaendelezwa kwa maslahi ya nchi mbili hizo.

Pia amesema, Japan itaendelea kuinga mkono juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi kupitia sekta za Uvuvi na Utalii na kuisifia Zanzibar kuwa ni kisiwa cha kipekee kutokana na mandhari yake, huku akibainisha umuhimu wa kuwa na miundombinu bora katika kuleta ustawi wa sekta za Uchumi wa Buluu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news