Waziri Dkt.Mabula asitisha vibali vya ujenzi vituo vya mafuta

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula amesitisha utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo vya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo kwa muda wa miezi mitatu kuanzia sasa.

Waziri ametoa agizo hilo ili kutoa nafasi kwa Wizara ya Ardhi na wizara zinazohusika na utoaji vibali kufanya tathimini ya kina kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta kufuatia kuwepo kwa ujenzi unaokiuka maelekezo ya mipango kabambe iliyopo.

Waziri Mabula ametoa agizo hilo leo Novemba 10, 2022 mbele ya vyombo vya habari jijini Dodoma nakuongeza kuwa baadhi ya wamiliki wamekuwa wakiomba vibali vya ukarabati wa majengo chakavu mijini na baadae kufanya uendelezaji wa maeneo hayo kinyume na mipango kabambe iliyopo.

Waziri Mabula ameongeza kuwa, pamoja na kuwepo kwa kanuni husika, kumekuwepo na hujenzi holela wa vituo vya mafuta nchini usiozingatia matakwa ya Sheria ya Mipangomiji na Kanuni zake jambo linalochagiza uwepo wa agizo hilo la kusitisha vibali hivyo.

Aidha, Waziri Mabula ameelekeza kusitisha kutoa vibali vya ujenzi vinavyokiuka mipango kabambe ya Majiji, Manispaa, Miji na kusitisha ugawaji viwanja kiholela unaopelekea taswira ya miji yetu kuharibika akisisitiza kuwa kama kuna mpango wa kujenga magorofa eneo husika ufuatwe mpango uliopo.

Aidha Dkt. Mabula amezitaka mamlaka za upangaji kuhakikisha uendelezaji upya maeneo ya ndani ya miji na mgawanyo wa maeneo unaofuata Mipango Kabambe iliyopo na mipango kina iliyoandaliwa.

Waziri Mabula amewaelekeza wataalamu katika ofisi za ardhi kote nchini zisimamiwe utekelezaji wa Mipango Kabambe na kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha mapendekezo ya mipango hiyo yanatekelezwa.

Waziri Mabula ameitaja Sheria ya Mipango miji Sura 355 kupitia fungu 77(1)b kuwa inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, mamlaka ya kutoa kanuni za viwango vya matumizi ya ardhi.

Dkt. Mabula ameitaja Sheria hiyo na kanuni ya 93 ya mwaka 2018 kuwa ndiyo inayotoa maelekezo kuwa umbali wa kituo kimoja hadi kingine ni mita 200 kwa maeneo yaliyopangwa na mita 500 kwa maeneo yasiyopangwa.

Aidha, Waziri Mabula amesema tayari Wizara yake imeidhinisha Mipango Kabambe 26 ikiwemo ya Majiji 6 ya Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Tanga pamoja na Mipango Kabambe ya Mikoa ya Iringa, Morogoro, Mtwara Mkindani, Songea, Singida, Tabora, Kigoma Ujiji, Mpanda, Sumbawanga, Bukoba, Shinyanga na Musoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news