Rais Dkt.Mwinyi awaeleza jambo viongozi wa Dunia kuhusu Sekta ya Utalii nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inategemea pato lake kwa asilimia 29.2 katika Sekta ya Utalii huku akieleza kuwa, Serikali imeweka hatua za makusudi katika mazingira wezeshi kwa kujumuisha sera, mifumo ya kitaasisi na kisheria ili sekta hiyo ikue kwa njia endelevu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa nane kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Dunia ambao wanashiriki mkutano huo jijini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo katika Kongamano la Kimataifa la 22 la Mkutano wa Baraza la Usafiri na Utalii Duniani (World Travel &Tourism Council Global Summit) lililofanyika jijini Riyadh,Saudi Arabia katika Hoteli ya Ritz-Carlton ambapo, Dkt.Mwinyi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema,ukuaji wa Sekta ya Utalii inatarajiwa kuwavutia wageni wenye uwezo mkubwa ambao watatumia fedha zaidi ili kulinda rasilimali za bahari pamoja na uchafuzi wa mazingira.

Akifungua kongamano hilo, Waziri wa Utalii wa Saudia Arabia, Mhe.Ahmed Al Khateeb amesema, anatarajia majadiliano ya kongamano hilo yatoe njia sahihi za kutatua changamoto za utalii,usafirishaji na mazingira kwa ujumla.

Pia,kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani ambapo walipata fursa ya kuchangia mada mbalimbali huku likiongozwa na mwandishi nguli nchini Marekani wa CBS,Peter Greenberg ambaye alikuwa mtayarishaji wa filamu ya Royal Tour Tanzania.

Wakati wa mkutano wa pamoja kati ya waandishi wa habari uliofanyika Jumatatu na Julia Simpson, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Usafiri na Utalii Duniani (WTTC), Waziri Al-Khatib alisema, "Tunaamini katika umuhimu wa ushirikiano.

"Kwa hiyo, tunatarajia kwa kuwa mwenyeji wa usafiri na utalii. Mkutano wa kilele mwaka huu utachangia katika kuunganisha juhudi za Kimataifa, kupitia mchango wenye ushawishi wa washiriki katika mkutano huu,"alibainisha.

Waziri Al Khateeb aliongeza kuwa, kipaumbele kwa watu na uendelevu wa rasilimali za sayari kutaunda mustakabali mpya hivyo kuifanya sekta ya utalii kustawi zaidi kwa matokeo bora.

Aidha,katika muktadha huo, Al-Khatib alibainisha kuwa,Saudi Arabia kwa sasa inachukuliwa kuwa mojawapo ya maeneo bora zaidi ya utalii duniani, kutokana na maagizo ya uongozi wake na rasilimali zilizotengwa kwa sekta hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Usafiri na Utalii Duniani (WTTC), Simpson, kwa upande wake, alibainisha kuwa, wajumbe wa baraza hilo walikuwa wakipanga katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuzindua uwekezaji mkubwa wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 10.5 nchini Saudi Arabia.

“Tukio hili linawaleta pamoja viongozi na maofisa mashuhuri na muhimu katika sekta ya usafiri na utalii duniani kote, lengo likiwa ni kujadili njia za kuhakikisha mustakabali wa sekta hii kwa muda mrefu, ambao ni muhimu sana kwa uchumi wa Dunia, uzalishaji wa ajira, na maendeleo ya maisha katika sehemu mbalimbali za Dunia hii,” aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.

Mkutano huo, unaoendelea hadi Alhamisi ya wiki hii, unachukuliwa kuwa moja ya hafla muhimu zaidi za kusafiri na utalii katika kiwango cha Kimataifa.

Aidha, miongoni mwa wazungumzaji wanaopanda jukwaani ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Theresa May, Waziri Mkuu wa pili mwanamke wa Uingereza baada ya Margaret Thatcher.

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Wakuu wa Dunia, aliashiria juhudi kubwa zilizofanywa wakati wa uongozi wake kuunga mkono maendeleo endelevu, akisisitiza jukumu kubwa la mataifa katika kuandaa njia na kusaini Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris na kuhamasisha juhudi za viongozi wa dunia kulinda mazingira na kudumisha uwiano wa hali ya hewa.

Muigizaji na Mkurugenzi wa filamu aliyeshinda tuzo ya Golden Globe, Edward Norton ambaye ni mtetezi wa nishati mbadala na mfuasi mkuu wa Wakfu wa Wanyamapori wa Afrika atashiriki katika kipindi cha kipekee cha maswali na majibu.

Aidha, mkutano huo ambao unafanyika chini ya kauli mbiu, “Safiri kwa Mustakabali Bora”, unaangazia thamani ya sekta hiyo, sio tu kwa uchumi wa Dunia, bali kwa sayari na jamii kote duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news