Hakimu akutwa amefia gesti bila kuacha ujumbe

NA DIRAMAKINI

HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Michael Royan (31) anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu katika nyumba ya kulala wageni ya Safari Bar iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Theopista Mallya amesema, tukio hilo lilitokea Novemba 27, mwaka huu majira ya saa tano asubuhi baada ya marehemu kutoamka kutoka kwenye chumba alichokua amelala katika nyumba hiyo ya kulala wageni.

Amesema kuwa, asubuhi ya siku hiyo ofisa upelelezi wa mkoa wa Rukwa alipigiwa simu na mtu anayeitwa Benard Wilfred ambaye alijitambulisha kuwa ni mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni na kueleza kuwa, katika nyumba yake ya kulala wageni kuna mteja ambaye amelala na hajaamka na inaonekana kuwa amepoteza fahamu.

Kamanda huyo amesema, baada ya polisi kufika eneo hilo waliingia ndani ya chumba hicho na kumchukua mtu huyo kisha kumkimbiza Hospital ya Rufani ya Mkoa ya Sumbawanga ambapo alipokelewa na baada ya uchunguzi wa awali wa kitabibu ilibainika kuwa mtu huyo tayari amefariki dunia.

Aidha,Kamanda Mallya amesema kuwa, polisi walipoanza uchunguzi wa tukio hilo walibaini kuwa marehemu alikua ni mtumishi wa serikali katika Idara ya Mahakama mkoani hapa katika Mahakama ya mwanzo na kituo chake kilikuwa ni Mahakama ya Mwanzo Kasanga.

Kamanda huyo amesema kuwa,uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda marehemu alikunywa sumu, lakini baadhi ya viungo vyake vya mwili vimechukuliwa na kupeleka sampuli kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kupata majibu sahihi ya nini kilichosababisha kifo cha Hakimu huyo.

Wakati huo huo, Kamanda huyo amesema kuwa, marehemu hakuacha ujumbe wowote hivyo imekua ni vigumu kufahamu sababu za tukio hilo, lakini alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na litatoa taarifa baada ya uchunguzi huo kukamilika karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news