Rais Dkt.Mwinyi: Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya afya hatua kwa hatua

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kadri hali ya uchumi itakavyoimarika, ili kuhakikisha inatoa huduma bora za afya nchini kote.
Dkt.Mwinyi amesema hayo katika uzinduzi wa ripoti ya ufuatiliaji wa Mkataba wa Nairobi kuhusu mkutano wa kimataifa wa idadi ya watu na maendeleo, wenye lengo la kusimamia utekelezaji wa makubaliano kuhusu utoaji huduma bora kwa akinamama na watoto, hususuani katika masuala ya uzazi, uliofanyika Hoteli ya Melia Kiwengwa Mkoa Kaskazini Unguja.

Amesema, katika mwaka huu wa Fedha wa 2022 Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Afya kwa asilimia 8.3 kutoka asilimia 7.7 iliotengwa katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, ikiwa ni juhudi za Serikali kufikia Azimio la Abuja la asilimia 15.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, DkT.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akifuatana na Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo la Kimataifa linalohusika na Idadi ya Watu na Maendeleo ya Afya ya Uzazi na Jinsia (UNFPA), Dkt.Natalia Kanem (kushoto) wakati alipowasili katika Hoteli ya Melia Kiwengwa Wilaya Kaskazini "B" Unguja Novemba 10, 2022,kuufungua mkutano wa Kimataifa wa kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya Kimataifa kuhusu utoaji wa huduma bora kwa kinamama na watoto pamoja na afya ya uzazi. (Picha na Ikulu).

Amesema, ongezeko hilo la bajeti limeweza kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya katika nyanja tofauti, ikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za watoto na vijana pamoja na uzazi wa mpango kwa jamii ya Wazanzibari kote nchini bila malipo.
Amesema, hivi sasa wananchi wote wanaweza kupata huduma bora za afya katika eneo lisilozidi kilomita tano kutoka makazi ya kudumu ya mwananchi, huku Serikali ikiwa njiani kukamilisha mpango wa Bima ya Afya.
Dkt.Mwinyi amesema kwa msaada wa washirika wa maendeleo Serikali inaendelea kuandaa mfumo wa afya, kujenga miundombinu ya afya, kuajiri rasilimali watu sambamba na kupata bidhaa zaidi za afya ili kuweza kutoa huduma bora za afya mijini na vijijini.

Aidha, amesema juhudi zinafanyika kuongeza upatikanaji wa elimu ya kina ya umri wa kujamiiana na uzazi kwa vijana wanaosoma na wasiosoma, ili kuzuia pamoja na kukabiliana na viwango vya juu vya vifo vya uzazi, magonjwa na mimba za utotoni ambazo zimekuwa zikiendeleea kujiri licha ya juhudi mbalimbali za Serikali.
Amesema pia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa inafanya kazi kwa bidii kukomesha ukatili wa kijinsia wa aina zote zikiwemo mimba za utotoni.
Alieleza kuwa, sheria, sera na mikakati iliyopo imeimarishwa ili kuakisi malengo yaliowekwa katika ngazi za Kimataifa, kikanda na kitaifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news