Rais Dkt.Mwinyi:Serikali inathamini sana mchango wa taasisi ziziso za kiserikali nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inafarijika kuona taasisi zisizo za kiserikali zinasaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo afya na elimu.

Dkt.Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na uongozi wa Taasisi ya ‘Mwanamke Intiative Foundation’, uliofika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema, Serikali inafarijika pale inapotokea taasisi iisiyo ya Kiserikali kuunga mkono juhudi za Serikali katika masuala mbalimbali, ikiwemo uimarishaji wa sekta za elimu na afya, kwa kuzingatia kuwa haina uwezo wa kufanya kila kitu.

Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wadau mbali mbali wa elimu ili kufanikisha dhamira ya kuimarisha sekta hiyo, na akatumia fura hiyo kubainisha maeneo matano ambayo yamepewa kipaumbele.

Alieleza kuwa, Serikali imeweka kipaumbele katika uimarishaji wa miundombinu kwa kuanzisha ujenzi wa skuli mpya, kukarabati skuli za zamani pamoja na madarasa ya zamani pamoja na kujenga maabara na maktaba.

Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni uimarishaji wa rasilimali watu katika kada ya ualimu, kwa kuzingatia uwepo wa walimu wachache wenye kiwango kidogo cha elimu, hususan katika masomo ya sayansi.

Amesema, Serikali inalenga kuongeza nguvu katika upatikanaji wa nyenzo mbali mbali, ikiwemo madawati pamoja na vitabu.

Aidha, Dkt.Mwinyi Mmwinyi amesema kipambele kingine cha Serikali katika uimarishaji wa sekta ya elimu ni uimarishaji wa kada ya ICT, akibainisha umuhimu wa kuwafunza mapema wanafunzi matumizi ya mifumo ya Teknolojia; ili waweze kwenda sambamba na mahitaji ya Dunia.

Dkt.Mwinyi amesema, uendelezaji wa Sekta ya Elimu unategemea zaidi bajeti ya Serikali kwa asilimia mia moja na kusema fedha hizo haziwezi kutosheleza mahitaji, hivyo akabainisha azma ya Serikali ya kutafuta njia mbadala za kuongeza fedha.

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Elimu iko tayari kukutana na kushirikiana na Taasisi za ‘Planet One’ ili kuona namna itakavyosaidia sekta hiyo, sambamba na Taasisi ya ‘G.S Group’ inayoshughulikia masuala ya ICT.

Dkt.Mwinyi aliishukuru Taasisi ya ‘Mwanamke Initiative Foundation’ kwa programu iliyoianzisha katika Mkoa wa Kusini Unguja inayolenga kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Mkoa huo katika Mitihani yao ya Taifa, akisema imeanza kuleta matokeo chanya.

Aidha, alitilia mkazo umuhimu wa kuelekeza nguvu katika uimarishaji wa Vyuo vya Amali, kwa kigezo kuwa kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaoanza katika ngazi za msingi, idadi inayopungua kadri kiwango cha elimu kinavyoongezeka na kuwaacha vijana wengi wakishindwa kutumia fursa mbalimbali katika soko la ajira.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation, Wanu Hafidh Ameir pamoja na mambo mengine, alisema taasisi hiyo imekuwa katika juhudi kubwa za kuinga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uimarishaji wa sekta za Afya, Elimu pamoja na Kilimo.

Amesema, miongoni mwa programu iliyoanzishwa na taasisi hiyo ni ile ya kutokomeza sufuri (division O) kwa skuli za Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo wanafunzi na walimu kutoka skuli 32 wamepatiwa mafunzo, kupatiwa vitabu pamoja na wengine kupata udhamini katika vyuo vya Amali Tanzania Bara katika masomo ya umeme na ushoni.

Amesema, katika juhudi za kuunga mkono juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya elimu, taasisi hiyo imefanikiwa kupata taasisi tofauti kutoka mataifa mbali mbali ikiwemo Planet One kutoka Dubai pamoja na G.S. Group kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu kupitia nyanja mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments