Rais Dkt.Mwinyi:Tuzidi kumtegemea Mwenyenzi Mungu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema madhumuni ya binadamu kuletwa duniani ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, hivyo amesisistiza wajibu wa waislamu kujifunza dini yao pamoja na kuwafunza watoto wao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la Ufunguzi wa Masjid Hussein Ghana Kichakani Wilaya ya Kati Unguja ambapo pia alijumuika na wananchi katika Ibada ya sala ya Ijumaa iliyofanyika katika msikiti huo Novemba 18, 2022.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi amesema hayo Novemba 18, 2022 katika Ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa ‘Masjid Hussein’ ulioko Ghana Kichakani, Wilaya Kati Unguja, hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya sala ya Ijumaa.

Amesema, dhamira ya binadamu kuletwa duniani, ni kumcha Mola wake pamoja na kuwafunza watoto elimu ya dini ili waweze kutekeleza dini yao kwa usahihi kama ilivyoamrishwa.
Alieleza kuwa, suala la kutafuta elimu ni muhimu na lenye manufaa makubwa duniani na akhera, hivyo akaunga mkono azma ya waumini wa msikiti huo ya kuendeleza elimu ya dini na kusema ni jambo jema.

Alhaj Mwinyi ameahidi kuchangia ujenzi wa Madrsa katika eneo la pembezoni mwa msikiti huo pamoja na kufanikisha ujenzi wa uzio kuzunguka msikiti huo.

Amewashukuru waumini na viongozi wao kwa hatua yao ya kuita msikiti huo jina lenye mnasaba na jina lake la ‘Hussein ‘ .
Aidha, amewataka waumini kuendeleea kuutunza na kuufanyia matengenezo ya mara kwa mara msikiti huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.

Alhaj Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi, wanakijiji pamoja na waislamu wote waliochangia kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.

Naye, Mufti Mku wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisema ana imani kubwa kuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi atafanikiwa kuwaunganisha Wazanzibar kama alivyofanikiwa Mtume Muhammad (SAW).

Aidha, kwa niaba ya wanakijiji wa Ghana Kichakani, Comodo Azana Hassan Msingiri aliishukuru Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kati Unguja kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.
Amesema pamoja na msikiti huo kutumika kwa shughuli za ibada, lakini pia utakuwa chachu ya kubadili tabia za baadhi ya wanakiijiji wa maeneo hayo.

Mapema, Katibu katika sala hiyo ya Ijumaa, Ustadhi Rajab Abdillah Haji alitoa ahadi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinfduzi la kuutunza msikiti huo, sambamba na kuutumia kikmailifu kwa ajili ya kutoa elimu ya dini kwa waumini wa maeneo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news