Rais Dkt.Mwinyi:Ujenzi wa madarasa unalenga kupunguza mrundikano wa wanafunzi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema hatua ya Serikali ya kuongeza ujenzi wa madarasa katika skuli za msingi na sekondari nchini, utawawezesha wanafunzi kushiriki kikamilifu katika masomo ya dini (madrasa).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Zanzibar ukiongozwa na Amiri wa jumuiya hiyo, Mwalimu Suleiman Omar Ahmed (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt.Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Viongozi wa Jumuiya kuhifadhisha Kuraan Zanzibar, ulioongozwa na Sheikh Suleiman Omar.

Amesema, ujenzi wa madarasa katika skuli mbalimbali za msingi na sekondari Unguja na Pemba, unalenga kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani, hali inayosababisha kuwepo mikondo miwili ya masomo (asubuhi na mchana).

Ameeleza kuwa, Serikali inatambua uwepo wa changamoto kwa baadhi ya wanafunzi kukosa muda wa kuhudhuria masomo ya dini katika vyuo na madrasa,na kusema wakati ujenzi huo ukiendelea Serikali kupitia Wizara ya Elimu itaangalia namna ya kupunguza tatizo hilo, hususani kwa wanafunzi wasiohusika na utaratibu wa kuingia madarasani kwa mikondo miwili.

Amesema, ili kupatikana ufanisi wa suala hilo, ushirikiano unahitajika kati ya Serikali,wazazi pamoja na wasimamizi wa madrasa na vyuo hivyo.

“Mimi ninaamini kwa nguvu tulizoweka katika kuongeza madarasa, hatua hiyo itapunguza utaratibu uliopo wa mikondo miwili ya masomo na kutoa fursa ya vijana kwenda madrasa,”amesema.

Aidha, Alhaj Dkt.Mwinyi amesema, Serikali itaangalia uwezekano wa kuwapatia nafasi za masomo ya Chuo Kikuu wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufanikiwa kuhifadhi Juzuu 30 za Kuraan, kupitia fursa zinazopatikana kutoka kwa wafadhili mbali mbali, hususan wale wa nchi za Kiislamu.

Hata hivyo, aliwashauri wanafunzi hao kuingia kwenye mchakato wa kupata fursa za masomo ya Chuo Kikuu kupitia Bodi ya Mikopo, kwa kigezo kuwa hatua hiyo itapunguza idadi ya wanafunzi wenye mahitaji.

Alhaj Dkt.Mwinyi aliutaka uongozi wa jumuiya hiyo kuwasilisha hati na michoro ya majengo ya Markaz yanayokusudiwa kujengwa katika eneo la Chwaka, Mkoa Kusini Unguja, ili juhudi za kupata wafadhili ziweze kufanyika na kufanikisha ujenzi huo hatua kwa hatua.

Katika hatua nyingine, Alhaj Mwinyi amesema, suala la ushiriki wa jumuiya hiyo katika mashindano ya kuhifadhi Kuraan mjini Dubai na kubeba Bendera ya Zanzibar lina changamoto za Kidiplomasia kama ilivyo kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) na azma yake ya kupata unachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Ametoa rai ya kuwepo mashindano kati ya washiriki wa pande mbili za Muungano ili kumpata mshindi atakayeweza kuiwakilisha nchi (Tanzania) katika mashindano hayo.

Aidha, amesema ni vyema kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) pamoja na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar kukaa pamoja na kuona namna bora ya kulishughulikia suala hilo ili kila nchi iweze kupata mwakilishi.

Hata hivyo, Alhaj Mwinyi amesema Serikali inapanga kuwaita kwa mazungumzao wadau wote wanaohusika na suala hilo, akiwemo Balozi wa UAE.

Mapema, Amiri wa Jumuiya ya Kuhifadhi Kuraan Zanzibar Amiri Suleiman Omar aliwasilisha ombi la jumuiya hiyo kwa Rais Alhaj Mwinyi akimuomba kuangalia uwezekano ya wawakilishi wa jumuiya kupata fursa ya kushiriki katika mashindano ya kuhifadhi Kuraan mjini Dubai, baada ya kuwepo kwa changamoto za kidiplomasia.

Aidha, Amiri huyo aliwasilisha ombi la kupata fursa za masomo ya Chuo Kikuu vijana waliomaliza kidato cha sita (Form VI) na ambao wamemaliza kuhifadhi Juzuu 30 za Kuraan tukufu, sambamba na wale waliomaliza kidato cha nne (F.VI) na kuhitaji kupata elimu katika ngazi ya Diploma.

Vile vile Amiri Suleiman alimuomba Alhaj Mwinyi kusaidia kupata ufadhili utakaofanikisha ujenzi wa Markazi ya Jumuiya hiyo katika eneo la Chwaka, ambapo wastani wa miaka 20 imepita tangu kupata eneo hilo na limebaki bila kuendelezwa .

Pia ameomba Serikali kuangalia namna ya kudhibiti muda wa masomo kwa wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari ili waweze kuhudhuria katika masomo ya dini, wakati ambapo hivi sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika masomo hayo ya skuli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news