Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa vyuo vikuu nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amevitaka Vyuo Vikuu nchini kutimiza wajibu wake wa kutoa mchango katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Juu ya Heshima ya Udaktari (Doctor of Letters Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Dar es katika Mahafali ya 52 ya Chuo hicho yaliyofanyika Novemba 30, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais ameongeza kuwa jukumu la Taasisi za elimu ya juu katika kuleta maendeleo ni kutoa elimu stahiki, kufanya tafiti na kutoa maoni katika mwenendo wa kulikuza na kuimarisha Taifa.

“Tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikisisitiza kuwa elimu inayotolewa inapaswa kukidhi mahitaji ya jamii katika karne ya 21,”amesema Rais Samia

Ameongeza kuwa mbali ya kuongeza maarifa elimu inayotolewa katika Taasisi za elimu inapaswa kuwawezesha wahitimu kuwa na stadi zitakazowawezesha kujiajiri, kuajiriwa ama kuwa wajasiliamali na kuwa tayari kuchangia maendeleo ya Taifa wanapohitimu masomo.

Akizungumza katika Mahafali hayo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa tayari Wizara imekamilisha Mapitio ya Sera na Mitaala na kwa sasa hatua inayofuata ni kuyawasilisha kwenye vikao vya ndani vya Serikali kabla ya mjadala wa wazi wa kitaifa kuhusu maoni na mapendekezo hayo.
Kuhusu uboreshaji wa elimu ya juu Prof. Mkenda amesema katika kujenga mazingira mazuri ya utoaji wa elimu ya juu, Serikali kupitia mradi wa HEET itatumia Dola za Kimarekani 425 sawa na fedha za kitanzania Bilioni 972 kupanua na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika fani za kipaumbele cha Taifa.

Ameongeza kuwa Mradi unatekelezwa katika Vyuo Vikuu 14 vya Serikali,Taasisi 3 za Wizara zinazoshughulikia Elimu ya Juu na Taasisi 5 za Elimu ya Juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Aidha, Prof. Mkenda amesema utekelezaji wa Mradi huo utaongeza udahili katika Fani za kipaumbele cha Taifa kutoka 40,000 mwaka 2020 hadi kufikia 100,600 mwaka 2026.

Kuhusu ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu, Waziri huyo amesema Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya Mikopo ya Elimu ya Juu mfululizo kila mwaka ambapo bajeti ya Mwaka wa fedha 2017/18 ilikuwa shilingi bilioni 427 lakini kwa Mwaka wa fedha 2022/23 bajeti hiyo imefikia Shilingi bilioni 654.

Ameongeza kuwa na kama hiyo haitoshi, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha ufadhili ujulikanao Samia Scholarship kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kwamba jumla ya shilingi Bilioni tatu zimetengwa kwa mwaka wa 2022/2023 kwa ajili ya wanafunzi 640.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news