RAIS SAMIA KUKUTANA NA MABALOZI ZANZIBAR

NA MWANDISHI WETU

MKUTANO wa kwanza wa Mabalozi wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Sita chini uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unafanyika mjini Zanzibar kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akitoa hotuba kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika mkutano wa Mabalozi unaoendelea Zanzibar.

Mkutano huo umefunguliwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) unalenga kufanya tathimini ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuweka mikakati mipya itakayowezesha Tanzania kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na mataifa mengine duniani pamoja na mashirika ya kimataifa ili Taifa liweze kunufaika kiuchumi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiwasilisha hotuba yake kwa mabalozi (hawapo pichani). Mkutano huo umeanza leo Zanzzibar na utamalizika tarehe 21 Novemba, 2022.

Balozi Mbarouk katika hotuba yake ya ufunguzi aliwasihi Waheshimiwa Mabalozi kuutumia mkutano huo kupata mawazo mbadala yanayolenga kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili nchi ili kuboresha utendaji kazi wa Wizara utakaoleta mchango mkubwa kwenye kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kukuza uchumi wa Taifa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akitoa tathmini ya mkutano wa mabalozi unaoendelea Zanzibar.

Mkutano huo ambao unatarajiwa kuhutubiwa na viongozi wakuu wa Serikali na Chama Tawala wakiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, Katibu Mkuu wa CCM, Comrade Daniel Chongolo pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mha. Zena Ahmed Said wakuu wa Taasisi za umma na binafsi zinazohusika na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utaweka mweleko mpya wa namna ya kutekeleza diplomasia ya uchumi kama kaulimbiu ya mkutano huo inavyobainisha “Mwelekeo Mpya Katika Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi”.
Sehemu ya mabalozi wakifuatilia kikao.

Mada ambazo Waheshimiwa Mabalozi na wadau wengine watazijadili kwa kina na kutoka na maazimio ya utekelezaji ni pamoja na mwenendo wa dunia na taathira yake katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi; nafasi ya intelejensia katika kutekeleza diplomasia ya uchumi; fursa na mikakati ya kuiwezesha Tanzania kunufaika na Eneo Huru la Biashara katika Bara la Afrika (AfCFTA); utaratibu wa mikopo ya karadha (mortgage financing, hire purchase, lease purchase) kwa ajili ya uendelezaji wa uendelezaji wa vitega uchumi, ununuzi wa majengo na vitendea kazi katika balozi; fursa za uchumi Zanzibar katika maeneo ya uchumi wa buluu na uwekezaji katika miundombinu na nafasi ya chuo cha diplomasia katika kuendeleza diplomasia ya Tanzania.
Baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakiongozwa na Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine (katikati) na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Amani, Balozi Stephen Mbundi wakifuatilia kikao.

Wakati wa mkutano huo Waheshimiwa Mabalozi na washiriki wengine watapata fursa ya kutembelea vivutio vya Zanzibar na miradi ya kimkakati pamoja na kushiriki mchezo wa mpira wa miguu kati ya Waheshimiwa Mabalozi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung tarehe 17 Novemba 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news