Ruzuku ya TASAF ilivyobadilisha maisha ya muosha viatu hadi kuwa muuza viatu Karatu

NA SOPHIA FUNDI

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kuzipa thamani ndoto za wananchi mbalimbali ambao awali walikuwa wamekata tamaa ya kusonga mbele kiuchumi kutokana na hali ngumu ambayo walikuwa wanapitia katika maisha yao.
Ally Gwangay ambaye ni mkazi wa Karatu Mjini wilayani Karatu mkoani Arusha ni mmoja wa wanufaika wa ruzuku kutoka TASAF Awamu ya Tatu. Akiwa ni muosha viatu katika maeneo ya Karatu mjini ameieleza DIRAMAKINI historia yake na changamoto alizopitia hadi leo hi akiwa na biashara yake ya kuuza viatu.

Ally amesema kuwa, anaishukuru Serikali kwa kuleta Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao umesaidia kaya maskini, kwani imekuwa msaada mkubwa katika maisha yake.
 
"Sina cha kusema zaidi ya kuelekeza shukurani za kipekee kwa Serikali yetu kuanzia zilizopita hadi hii ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kupitia ruzuku ya TASAF mimi Ally Gwangway nimeweza kutoka kweye kuosha viatu na kupiga rangi hadi leo hii kuwa na biashara yangu ya kuuza viatu,"ameieleza DIRAMAKINI katika mazungumzo mjini Karatu.

Amefafanua kuwa, biashara yake ya kuosha viatu na kupiga rangi alianza miaka ya 1996 akiwa na mtaji wa sh.20,000 ambapo aliendelea nao kwa kusuasua hadi leo hii akiwa na mtaji wa shilingi laki tano baada ya kuweka fedha za ruzuku anazozipata kwenye mfuko wa TASAF
Amesema kuwa, alianza kupokea ruzuku ya TASAF mwaka 2015 akiwa anapokea shilingi 4,8000 ambapo alianza kuweka kiasi kidogo kidogo akiwa na malengo yake ya kuanzisha biashara ya kuuza viatu.

Biashara ya kuuza viatu alianza mwaka 2018 akiwa na mtaji wa shilingi 70,000 ambapo alianza na pea sita za viatu jambo ambalo aliendelea nalo akiwa anapata faida ya shilingi 3,000 kwa siku na kufanikiwa kuweka shilingi 1000 kama akiba.

Wakati huo huo, Ally ametoa wito kwa wanufaika kutotosheka na ruzuku wanazozipata badala yake waanzishe miradi itakayowapatia kipato, kwani pale Serikali itakapositisha ruzuku watabaki bila kitu chochote na maisha yatakuwa magumu sana.

Amesema kuwa, wanufaika wengi wamekuwa wakichezea ruzuku wanazozipata aidha kwa kuzipeleka kwenye pombe na kutoweka akiba yoyote itakayowaingizia kipato chochote jambo ambalo litakuwa na hatari kwao pale ambapo muda wa mfuko kumalizika wa ruzuku kutolewa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news