SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA TAASISI ZA DINI KWA TAIFA-DKT.MABULA

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa taasisi za dini katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo miradi mingi ya kijamii inayosimamiwa na mashirika ya kidini hususani sekta ya afya, elimu na maji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akiwasili katika Kanisa la AICT Kizota tayari kuzindua Dayosisi mpya ya Kanda ya Kati ya Kanisa hilo pia kushiriki kusimikwa na kuwekwa wakfu Askofu Mteule Amos Katoto Ngeze kuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa la African Inland Church Dayosisi ya kati Dodoma.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt Angeline Mabula alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani kwenye uzinduzi wa Dayosisi mpya ya Kati ya Kanisa la Tanzania Inland Church Jijini Dodoma.

Pamoja na uzinduzi wa Dayosisi ya Kati Kanisa hilo pia limeshuhudia uwekaji wa jiwe la Msingi la Kanisa Kuu na Kusimikwa kwa Askofu mpya wa Dayosisi hiyo Askofu Mteule Amosi Katoto Ngeze kuwa kiongozi mpya wa kanisa hilo Dayosisi ya Kati.

Dkt. Mabula Katika hotuba yake hiyo amebainisha kuwa Watanzania wengi wamenufaika na wanaendelea kunufaika na huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi na mashirika ya dini na madhehebu mbalimbali na kutoa shukrani zake kwa mchango mkubwa wa kanisa akiliomba kuendelea kuwahudumia Watanzania.

‘’Kutuunga mkono kwa namna hiyo ndiko kunachangia sana nchi yetu kupiga hatua kubwa kwenye maendeleo hususan kufikisha huduma kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,"ameongeza Dkt. Angeline Mabula Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Dkt.Mabula pia aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhebu ya dini kuboresha maisha ya Watanzania na kupokea ushauri kama ambayo serikali imekuwa ikipokea na kufanyia kazi ushauri huo na kuwashirikisha katika mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akiweka tayari kukata utepe kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kanisa Kuu la Africa Inland Church Tanzania Dayosisi ya kati Dodoma.

Aidha Dkt. Mabula aliongeza kuwa serikali inatambua mchango wa kanisa katika kulinda na kudumisha amani katika nchi akilitaja suala la amani kuwa ni suala muhimu sana kwani bila ya amani hakuna maendeleo.

Dkt. Mabula alibainisha kuwa Taifa bila amani, hata haki na uhuru wa kumwabudu na kumtukuza Mungu wetu utakuwa mashakani hivyo, hatuna budi kusimamia haki sambamba na kuenzi na kuitunza amani yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.

Kwa sababu hiyo, Dkt. Mabula aliwasihi sana viongozi wa dini kuwakumbusha mara kwa mara waumini, na watu wote, kuhusu umuhimu wa kusimamia haki na kudumisha amani aliyotuachia Bwana wetu Yesu Kristu na kuiombea nchi na viongozi wake. ‘
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akikata utepe kuzindua Ujenzi wa Kanisa Kuu la Africa Inland Church Tanzania Dayosisi mpya ya kanda ya kati Dodoma.

Kuhusu Suhala la maadili Dkt.Mabula aliwaomba viongozi wadini wasichoke kufundisha na kulea vijana katika maadili mema na kuthamini kufanya kazi halali.

‘’Katika nyakati hizi, ni ukweli ulio wazi kuwa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii yetu. Vitendo viovu na mambo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu yanazidi kuongezeka, Mambo ambayo siku za nyuma yalikuwa nadra sana kutokea au kusikika sasa yanakuwa habari za kila siku na wakati mwingine huonekana ati ni kawaida,’’aliongeza Dkt.Mabula.

Waziri Mabula anaamini kwa dhati kuwa watu, wakiwa pamoja na sisi viongozi wa Serikali na wa vyama vya siasa wakishika mafundisho ya dini, wakawa na hofu ya Mungu, maovu mengi yatapungua sana na nchi yetu itaongozwa vizuri.

Naye Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Mussa Masanja Magwesela amesema kuwa Kanisa la AICT linayo maono ambayo ni kuona “Watu wote wanamwabudu Mungu katika roho na kweli na wanaishi maisha ya utoshelevu”.
Askofu Mteule Amos Katoto Ngeze mara baada ya kuwekwa Wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa kwanza wa kanisa la African Inland Church wa kanda ya Dayosisi ya kati Dodoma.

‘’Hii maana yake ni kwamba tunatambua kuna watu bado hawajamjua Mungu wa kweli hivyo wanahitaji kufikiwa. Katika Petro 3:9 Neno la Mungu linasema “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba,"aliongeza Baba Askofu Magwesela.

Aidha,Askofu Magwesela aliongeza kuwa kanisa linao wajibu wa kuwafikia watu kwa mahitaji yao mbalimbali, maana tunaishi katika nafsi tatu, mwili, roho na nafsi. Vyote vinahitaji kuhudumiwa, na nijukumu la Kanisa la Mungu kuwafikia watu wote kwa kuwaangazia mambo yote haya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news