Serikali kuzindua kampeni ya kupanda miti rafiki kwa maji kwenye vyanzo vya maji

NA DIRAMAKINI

WIZARA ya Maji imeandaa Mkutano Mkuu wa Nane wa Bodi za Maji za Mabonde unaotarajiwa kufanyika Novemba 16, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Eden Highlands jijini Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Maji kauli mbiu ya mkutano itakuwa ni“Utunzaji Endelevu wa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Jamii na Ukuaji wa Uchumi”.

Aidha, ufunguzi wa mkutano huo utafanyika sanjari na uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji hapa nchini. Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wizara ya Maji inatekeleza majukumu ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kupitia Bodi za Maji za Mabonde. Bodi hizo zipo tisa (9) ambazo ni; Rufiji, Wami/ Ruvu, Pangani, Ruvuma na Pwani ya Kusini, Kati, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa na Ziwa Nyasa.

Historia ya mkutano huu wa Bodi za Maji za Mabonde ilianza mwaka 2008 ambapo Wizara ya Maji ilianzisha utaratibu wa kuitisha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde kwa lengo la kukutanisha wadau ili kujadili na kupanga pamoja namna bora ya kushirikiana katika masuala mtambuka ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.

Mkutano Mkuu wa saba (7) ulifanyika mjini Kigoma, makao makuu ya Bonde la Ziwa Tanganyika Julai, 2019.

Mkutano utakuwa na matukio muhimu yafuatayo; (i) Kupanda miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji (ii) Kutia saini Tamko la Mawaziri wa Kisekta kuhusu Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji(iii) Kuzindua Mipango ya Uhifadhi wa Vidaka Maji nchini (Catchment Conservation Plans) (iv) Uwasilishaji wa matokeo ya tafiti na maandiko mbalimbali yanayohusiana na usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; na (v) Ziara ya kwenda uwandani kuona shughuli za usimamizi wa rasilimali za maji katika Bonde la Ziwa Rukwa.

Wadau wote wanakaribishwa wakiwamo viongozi wote, wananchi pamoja na Wataalam wa Wizara ya Maji, Washirika wa Maendeleo, Bodi ya Maji ya Taifa, Bodi za Maji za Mabonde, Mamlaka za Majisafi na Usafiwa Mazingira nchini; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi zisizo za Kiserikali, (AZAKI) Mashirika ya Dini, Elimu ya Juu na Utafiti, Sekta Binafsi, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji kushiriki katika zoezi la kupanda miti kwenye vyanzo vya maji na kushiriki hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Kupanda miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news