Wapinzani wampa Rais Dkt.Mwinyi kongole kwa kudumisha umoja, upendo, mshikamano, uongozi bora na kuleta maendeleo

NA DIRAMAKINI

LEO Novemba 15,2022 viongozi wa vyama vya upinzani Zanzibar wamezungumza na waandishi wa habari huku wakimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kudumisha umoja, mshikamano, upendo huku akiiwezesha Zanzibar kusonga mbele kiuchumi.
Mazungumzo hayo ambayo yameongozwa na Katibu Mkuu wa Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir yamefanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale. Yafuatayo ni yaliyojiri katika mkutano huo;
"Sisi kama vyama vya upinzani Zanzibar tunatoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi wake bora ndani ya hii miaka miwili, kwani amefanya juhudi mbalimbali za kimaendeleo na kuifanya Zanzibar kusonga mbele.

"Ndani ya hii miaka miwili ya Rais Hussein Ali Mwinyi amehakikisha amani na utulivu ndani ya Zanzibar baada ya uchaguzi unadumishwa, hii ikiwa ni tofauti na kipindi cha nyuma ambapo uchaguzi ukiisha kuna kuwa na vurugu nyingi.
"Kwa mamlaka ya kikatiba na sheria za nchi, Rais ana ruksa ya kufanya teuzi mbalimbali, lakini hivi juzi Rais wetu amefanya teuzi ya makatibu wakuu na Mkurugenzi Tume ya Uchaguzi Zanzibar na kupokelewa tofauti na baadhi ya wanasiasa walio na nia ovu juu ya Rais Mwinyi na serikali yake.

"Sisi kama vyama tisa vya upinzani Zanzibar tunalaani vikali kauli iliyotolewa na chama cha ACT- WAZALENDO kwa umma kumtaka Rais Mwinyi kufanya utenguzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwani kauli hii ina ubinafsi ndani yake na kutaka kuleta uchonganishi kwa wananchi.
"Mhe.Rais ana haki ya kumteua yeyote nchi hii kwa ajili ya kumsaidia kuliongoza taifa hili na watu wake, kauli hii ya ACT Wazalendo sisi kama vyama vya upinzani tunaipinga vikali na kuwaambia waache ubinafsi na kutaka kutuharibia nchi.

"Chama cha ACT-Wazalendo kina nafasi nzuri ya kumshauri Rais kupitia Makamu wa Kwanza wa Rais na viongozi mbalimbali ngazi ya uwaziri, hivyo waache janja janja ya kutaka kumtoa rais wetu kwenye reli.
"Katika chaguzi zote zilizofanyika uchaguzi wa mwaka 2020 ndio uchaguzi iliyokuwa huru na haki bila watu kupigwa mabomu, hivyo naomba tuheshimu maamuzi ya wananchi kwa Rais wao.
"Rais Mwinyi anania nzuri na taifa la Zanzibar ndio maana ameteua kikosi kazi kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali muhimu kuhusu Zanzibar na kwa bahati nzuri kamati hiyo baadhi ya viongozi kutoka ACT-Wazalendo walikuwepo na walitoa hoja nyingi tu."

Post a Comment

0 Comments