Uingereza yaipiga nusu dazeni ya mabao Iran iliyogoma kuimba wimbo wa Taifa

NA DIRAMAKINI

PENGINE makasiriko ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamewagharimu wawakilishi wao timu ya Taifa ambayo inacheza michuano ya Kombe la Dunia la FIFA 2022 nchini Qatar.

Picha na AFP.

Ni baada ya kugoma kuimba wimbo wa Taifa leo Novemba 21, 2022 muda mfupi wakati mtanange huo ukianza katika Dimba la Khalifa International Stadium uliopo jijini Doha, Qatar hali iliyoibua hisia tofauti huku maswali yakiwa watu hao wanawakilisha Taifa gani ambalo hawaliheshimu?.

Waingereza (England) wao hilo halikuwahusu kwani, wameamua kuwabebesha nusu dazeni ya mabao wana Iran hao, huenda wataona namna ya kugawana.

Katika mtanage huo wa Kundi B, Jude Bellingham wa England alitupia nyavuni bao la kwanza, Bukaya Saka akatupia bao la pili dakika ya 43 ambapo walifunga dakika 45 za mwanzo wakiwa na mabao mawili kibindoni.

Dakika ya 46, Raheem Sterling alitupia bao lingine ambapo kabla Wairan hawajakaa vizuri Bukayo Saka alivutia risasi nyingine nyavuni dakika ya 62, ingawa Mehdi Taremi wa Iran dakika ya 65 alitupia bao la mwanzo la kufutia machozi, bao ambalo kabla halijawapooza dakika ya 71 Marcus Rashford alitupia bao la tano kwa England.

Mtanage huo uliendelea hadi dakika ya 90 ambapo Jack Grealish alikamilisha nusu dazeni ya mabao ya England huku Iran ikijifariji kwa bao la pili ambalo lilipelekwa kambani na Mehdi Taremi dakika ya 103.

Awali wachezaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hawakuweza kuimba wimbo wao wa taifa wakati wa mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia dhidi ya Uingereza.

Uamuzi huo waliufikia kama njia ya kuunga mkono waandamanaji wanaoipinga serikali katika nchi yao. Kabla ya mchezo huo nchini Qatar, nahodha Alireza Jahanbakhsh alisema timu hiyo itaamua kwa pamoja kukataa au kutoimba wimbo huo ili kuonesha mshikamano kwa maandamano ambayo yametikisa utawala nchini Iran.

Wachezaji wa Iran walisimama kwa jazba na nyuso zenye huzuni huku wimbo wao ukipigwa kuzunguka Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa mjini Doha.

Iran imetikiswa na miezi miwili ya maandamano ya nchi nzima tangu kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 katika kizuizi cha polisi kwa kukiuka maadili mnamo Septemba 16.

Amini, Mirani mwenye umri wa miaka 22 na mwenye asili ya Kikurdi, alifariki siku tatu baada ya kukamatwa mjini Tehran kwa madai ya kukiuka kanuni za mavazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya wanawake, ambayo ni pamoja na uvaaji wa hijabu.

Baadhi ya wanariadha wa Iran wamechagua kutoimba wimbo wa taifa au kusherehekea ushindi wao ili kuunga mkono waandamanaji.

Jahanbakhsh, ambaye aliwahi kuchezea klabu ya Brighton ya Uingereza, alikasirishwa wiki iliyopita na swali la mwandishi wa habari wa Uingereza kuhusu suala la wimbo wa taifa huku akimtaka kuacha kumpangia maisha.

Tangu kifo cha Amini kimesababisha karibu watu 400 kuuawa, kulingana na kundi la utetezi wa Haki za Kibinadamu la Iran huko Oslo.

Hali hiyo ya leo,imesababisha maswali iwapo timu hiyo inawakilisha Iran au utawala ambao umetawala kwa mkono wa chuma tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.(Mashirika)

Post a Comment

0 Comments