UJENZI WA MIRADI YA UTALII MAENEO YALIYOHIFADHIWA UTAONGEZA PATO LA TAIFA-MHE.MAKOA

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Ally Juma Makoa amesema kuwa miradi ya uendelezaji utalii iliyokamilika na ile inayoendelea kujengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika maeneo yaliyohifadhiwa itasaidia kuongeza Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 17 iliyopo sasa.
Mhe. Makoa ameyasema hayo Novemba 14, 2022 wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua utekelezaji miradi ya fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi .

"Tunajua Wizara hii kupitia Ilani ya CCM inatakiwa kuongeza idadi ya watalii ifikie milioni 5 ifikapo 2025 hivyo kwa kazi anazozifanya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kweli zinawavutia watalii wengi na tunaendelea kumuomba sana Mhe Rais azidi kuiangalia Wizara hii kwa sababu Pato lake liko nje nje,"amesisitiza Mhe. Makoa.
Amesema,kamati imetembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kushuhudia ujenzi wa lango la kisasa la kuingilia ,nyumba za watumishi,viwanja vya ndege, miundombinu ya maji na ukarabati wa barabara na maegesho ya magari na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuipatia Wizara hiyo fedha kiasi cha shilingi Bilioni 90.2.

"Tunatarajia kwamba watalii wataongezeka na hata wakifika watakuta miundombunu mizuri na matokeo yake Pato letu la Taifa litaongezeka," Mhe. Makoa ameongeza.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Mary Masanja (Mb) amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zimeharakisha utekelezaji wa miradi ya kuendeleza utalii katika maeneo yaliyohifadhiwa.

"Wizara ya Maliasili na Utalii ilipata fedha kiasi cha shilingi bilioni 90.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyo ndani ya maeneo tunayoyahifadhi na fedha hizi zilikua zinatokana na changamoto ya UVIKO 19 ambapo Hifadhi ya Mkomazi ilinufaika na fedha kiasi Cha shilingi Bilioni 4.3," Mhe. Masanja amesema.

Amesema miradi hiyo itasaidia kuongeza watalii na Pato la Serikali na kutoa Ajira kwa wananchi ikiwemo kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Aidha, ameiomba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuendelea kupitia na kukagua miradi hiyo maana wao ni jicho na moyo wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiahidi kuisimamia kwa vitendo kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais kuhusu usimamizi mzuri wa fedha hizo ili ziendane na thamani halisi ya miradi iliyojengwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imehitimisha ziara yake katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news