UNAIDS yaonesha wasiwasi kufikiwa malengo kutokomeza VVU Duniani

NA DIRAMAKINI

TATHMINI iliyofanywa na Umoja wa Mataifa kuelekea Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Desemba Mosi inaonesha pengo la usawa ni kikwazo kikubwa katika juhudi za kutokomeza janga la Virusi Vya Ukimwi (VVU) duniani.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya tathmini iliyotolewa Novemba 29, 2022 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS).

Ripoti hiyo ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa, kwa mwelekeo wa sasa ulimwengu hautafikia malengo yaliyokubaliwa ya Kimataifa kuhusu ukimwi.

Aidha, ripoti hiyo mpya ya UNAIDS, iliyopewa kichwa “Ukosefu wa Usawa wenye Hatari kubwa” inaonesha kwamba, hatua za haraka za kukabiliana na pengo la usawa zinaweza kurejesha hatua za vita dhidi ya ukimwi kwenye mstari.

Mapema mwaka huu shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilionya kwamba, hatua za mapambano dhidi ya ukimwi ziko hatarini pamoja na kuongezeka kwa maambukizi mapya na kuendelea kwa vifo katika sehemu nyingi za dunia na kukosekana kwa usawa ni sababu kuu.

Ripoti inaonesha jinsi viongozi wa Dunia wanavyoweza kukabiliana na ukosefu huo wa usawa, na kuwataka wawe na ujasiri wa kufuata kile ambacho ushahidi unaonyesha.

Aidha,ripoti hiyo,imeweka wazi athari za kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika hatua za vita dhidi ya ukimwi, ukosefu wa usawa katika makundi ya watu maalum, na ukosefu wa usawa kati ya watoto na watu wazima.

Pia inaweka wazi jinsi gani vikwazo vya kifedha vinavyoongeza ugumu wa kushughulikia ukosefu huo wa usawa duniani.

Ripoti inaonesha jinsi gani kukosekana kwa usawa wa kijinsia na mila potofu vinavyorudisha nyuma hatua za kutokomeza janga la ukimwi.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima amesema, "Ulimwengu hautaweza kulishinda janga la ukimwi wakati unaimarisha mfumo dume.

"Tunahitaji kushughulikia ukosefu wa usawa unaowakabili wanawake. Katika maeneo yenye mzigo mkubwa wa VVU, wanawake waliofanyiwa ukatili na wenzi wao wanakabiliwa na uwezekano wa asilimia 50 zaidi wa kupata VVU,"amesema.

Ripoti inabainisha kuwa, katika nchi 33 tangu mwaka 2015-2021 ni asilimia 41 tu ya wanawake walioolewa wenye umri wa miaka 15-24 wanaweza kufanya maamuzi yao wenyewe juu ya afya ya ngono.

"Ramani pekee yenye ufanisi ya kukomesha ukimwi, kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha afya, haki na ustawi wa pamoja, ni ramani ya njia ya kupigania haki za wanawake.

"Mashirika na mavuguvugu yaa kupigania haki za wanawake tayari yako mstari wa mbele kufanya kazi hii ya ujasiri. Viongozi wanatakiwa kuwaunga mkono na kujifunza kutoka kwao,"amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Ripoti inasema madhara ya kukosekana kwa usawa wa kijinsia kwenye hatari za VVU kwa wanawake yanaonekana hasa katika Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo wanawake walichangia asilimia 63 ya maambukizi mapya ya VVU mwaka 2021.

Wasichana vigori na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wana uwezekano mara tatu zaidi wa kupata VVU kuliko wavulana na vijana wa rika moja katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Sababu inayochechea hali hiyo ni uwezo. Utafiti mmoja umeonesha kuwa, kuwawezesha wasichana kubaki shuleni hadi watakapomaliza elimu ya sekondari kunapunguza uwezekano wa kuambukizwa VVU kwa hadi asilimia 50.

Hili likiimarishwa na msaada wa uwezeshaji, hatari za wasichana kuambukizwa VVU hupunguzwa hata zaidi.

“Viongozi wanatakiwa kuhakikisha wasichana wote wako shuleni, wanalindwa dhidi ya unyanyasaji ambao mara nyingi hurekebishwa ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni, na kuwa na njia za kiuchumi zinazowahakikishia mustakabali wenye matumaini,"imebainisha ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hulka mbaya za mfumo dume huwakatisha tamaa wanaume kutafuta huduma. Wakati asilimia 80 ya wanawake wanaoishi na VVU walikuwa wakipata matibabu mwaka 2021, ni asilimia 70 tu ya wanaume walikuwa kwenye matibabu.

Aidha, kuongezeka kwa programu za kubadilisha mtazamo wa kijinsia katika sehemu nyingi za dunia ni muhimu katika kukomesha janga hili kwani kuendeleza usawa wa kijinsia kutanufaisha kila mtu.

Ripoti inaonesha kuwa hatua za kukabiliana na ukimwi zinarudishwa nyuma na kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa matibabu kati ya watu wazima na watoto.

Wakati zaidi ya robo tatu ya watu wazima wanaoishi na VVU wanatumia dawa za kurefusha maisha, zaidi ya nusu ya watoto wanaoishi na VVU wanatumia dawa ya kuokoa maisha.

Hii imekuwa na matokeo mabaya kwani mwaka 2021, watoto walichangia asilimia nne tu ya watu wote wanaoishi na VVU, lakini asilimia 15 ya vifo vyote vinavyohusiana na ukimwi hivyo kuziba pengo la matibabu kwa watoto kutaokoa maisha.

Ripoti imesema kuwa ubaguzi, unyanyapaa na uharamishaji vinagharimu maisha na kuzuia ulimwengu kufikia malengo yaliyokubaliwa ya ukimwi.

Uchambuzi huo mpya unaonesha kuwa, hakuna kupungua kwa maambukizi mapya miongoni mwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume katika maeneo ya Magharibi na Kati mwa Afrika na Kanda za Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Ripoti inaainisha kuwa, kukabiliana na maambukizi ya virusi, kushindwa kupiga hatua za maendeleo kwa makundi muhimu kunadhoofisha hatua za kutokomeza ukimwi na kuainisha hatua ndogo zilizopigwa katika vita hivyo.

Duniani kote,kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNAIDS zaidi ya nchi 68 bado zinaharamisha mahusiano ya ngono ya jinsia moja.

Uchambuzi mwingine ulioangaziwa katika ripoti hiyo umegundua kuwa wanaume mashoga na wanaume wengine wanaofanya mapenzi na wanaume wanaoishi katika nchi za Kiafrika zenye sheria kandamizi zaidi wana uwezekano mdogo wa kujua hali zao za VVU mara tatu zaidi kuliko wenzao wanaoishi katika nchi zenye ukandamizaji mdogo wa kisheria , ambapo maendeleo yanakua kwa haraka zaidi.

Pia wafanyabiashara ya ngono wanaoishi katika nchi ambazo biashara ya ngono imeharamishwa wana nafasi kubwa mara saba ya kuishi na VVU kuliko katika nchi ambazo biashara ya ngono imehalalishwa kwa kiasi fulani.

Ripoti inaonesha maendeleo dhidi ya ukosefu wa usawa yanawezekana na inaangazia maeneo ambayo hatua dhidi ya ukimwi zimepata maendeleo makubwa.

Kwa mfano, wakati tafiti miongoni mwa makundi muhimu mara nyingi huangazia huduma za chini kati ya watu muhimu, kaunti tatu nchini Kenya zimefikia kiwango cha juu cha matibabu ya VVU miongoni mwa makahaba wa kike kuliko miongoni mwa idadi ya jumla ya wanawake wenye umri wa miaka kati ya 15-49.

Hii imesaidiwa na programu dhabiti za VVU kwa miaka mingi, ikijumuisha huduma zinazoongozwa na jamii. Ripoti imesisitiza kwamba uwekezaji mpya wa kushughulikia pengo la usawa unaohusiana na VVU unahitajika haraka.

Wakati ambapo mshikamano wa kimataifa na kuongezeka kwa ufadhili kunahitajika zaidi, nchi nyingi za kipato cha juu zinapunguza misaada kwa afya ya kimataifa.

Mwaka 2021, ufadhili uliopatikana kwa programu za VVU katika nchi za kipato cha chini na cha kati ulikuwa pungufu wa dola bilioni 8.

Pia kuongezeka kwa usaidizi wa wafadhili ni muhimu ili kurudisha hatua za kupambana na VVU kwenye mstari ambapo ripoti imefafanua kuwa, bajeti zinahitaji kuweka kipaumbele kwa afya na ustawi wa watu wote, hasa watu walio hatarini ambao wameathiriwa zaidi na ukosefu wa usawa unaohusiana na VVU. (UN)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news