UNAKOPESHAKOPESHA? Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni yako

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 24, 2022 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imebaini kuwa,kuna baadhi ya taasisi,kampuni na watu binafsi wanaojihusisha na biashara ya utoaji mikopo nchini bila kuwa na leseni.Jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga ameyabainisha kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma kuwa,taasisi, kampuni na mtu binafsi wasio na leseni husika hawaruhusiwi kufanya biashara ya kukopesha.

Aidha,Prof.Luoga amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (2) (a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 3018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa sheria hiyo ni pamoja na faini isiyopungua shilingi milioni 20 au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili.

Benki Kuu ya Tanzania pia imewaasa wananchi kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambao hawana leseni.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,tusikubali miteremko, yafaa kuzingatia taratibu za ukopaji kwa kuwafikia watu au taasisi sahihi, kwani orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zilitolewa na Benki Kuu ya Tanzania ambayo inapatikana kwenye tovuti ya https://www.bot.go.tz endelea;


1.Unakopeshakopesha, watu unawawezesha,
Biashara wanogesha, idadi unafungasha,
Vipi umehalalisha, leseni yako yatosha?
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

2.Sheria huduma ndogo, hiyo yakulazimisha,
Kutoa huduma ndogo, hata watu kukopesha,
Bila leseni mzigo, rungu kwako itashusha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

3.Kama wewe ni kikundi, bora kujisalimisha,
Hata mtu si kikundi, biashara halalisha,
Huo hasa ni ufundi, huduma kuzifikisha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

4.Adhabu ni kubwa sana, usipojisalimisha,
Utapata tabu sana, kama wewe wavimbisha,
Tunakuhimiza sana, fanya yale yanakosha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

5.Milioni ishirini, shilingi utatemesha,
Bila kuwa na idhini, ukizidi kukopesha,
Sijikute msambweni, nenda kujihalalisha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

6.Na wananchi kumbuka, msije kujiangusha,
Kwa wakopesha kufika, bila kujihakikisha,
Leseni zakamilika, na siyo wa kupotosha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

7.Hebu kaa mbali sana, hao wanaokopesha,
Huku leseni hawana, wasije wakawarusha,
Ikibidi ulizana, muweze kujiridhisha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

8.Makundi yote matatu, Sheria inawezesha,
Kufika sehemu tatu, huduma kuhalalisha,
Msifanye yenye kutu, kutaka kubabaisha,
Benki Kuu yakuonya, kajipatie leseni.

9.Ni Kampuni taasisi, Benki Kuu yaziwasha,
Pia watu binafsi, ambao wajizungusha,
Kupata leseni hasi, huko wao wakopesha,
Benki Kuu yawaonya, kajipatie leseni.

10.Usalama wakitaka, ili wazidi kopesha,
Bila kuwa na mashaka, kwa pilato kufikisha,
Kapate leseni shika, endelea kukopesha,
Benki Kuu yawaonya, kajipatie leseni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news