Waziri Mkuu:Rais Samia ameridhia wanafunzi 28,000 waendelee na usajili vyuoni

*Abainisha uwepo wa mifumo mipya ya kiutumishi na mishahara

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kusoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma leo Novemba 11, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Bungeni leo Novemba 11, 2022 wakati akiahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 12, jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 31, mwakani.

Waziri Mkuu amewashukuru Wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Amesema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mkutano huo ni hoja ya ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

“Nyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo, lilikuwa ni kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 ambao walikuwa hawajapangiwa mikopo, kutokana na ukomo wa kibajeti,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hadi sasa taasisi za umma 455 zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotarajia kustaafu.

Akizungumzia utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha na kuweka mifumo imara ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa mifumo iliyopo na inayojengwa inasaidia kuharakisha utendaji kazi na usimamizi wa watumishi na inakuwa na taarifa sahihi kwa lengo la kuongeza tija na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema mfumo huo mpya ambao ulianza kutumika rasmi Mei 2021, umeunganishwa na mfumo wa PSSSF kwa ajili ya kubadilishana taarifa za michango ya watumishi na nyaraka za hitimisho la ajira; mfumo wa mikopo ya elimu ya juu (HESLB) kwa ajili ya kubadilishana taarifa za mikopo ya elimu ya juu kwa watumishi; mfumo wa ajira portal kwa ajili ya kubadilishana taarifa za waajiriwa wapya na mfumo wa NIDA kwa ajili ya kubadilishana taarifa za utambulisho wa Taifa wa watumishi.

Ameitaja mifumo mingine iliyojengwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za upimaji wa utendaji kazi wa watumishi na mikataba ya utendaji kazi ya taasisi kuwa ni Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma (PEPMIS) na Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma (PIPMIS).

“Ujenzi wa mifumo hiyo mipya umekamilika. Hivi sasa inafanyiwa majaribio na inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa majaribio na kutoa mafunzo kwa watumishi katika taasisi zote za umma,” amesema.

Amesema hatua ya mifumo hiyo kuwa ya kielektroniki itaondoa muhali, hisia za kupendeleana au kuoneana katika usimamizi wa utendaji kazi na itahamasisha uwajibikaji wa hiari wa watumishi wa umma itakayosaidia utoaji huduma bora na kwa wakati kwa umma wa Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news