Waziri Prof.Mkenda awauma sikio walimu, wamiliki wa shule nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia,Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema,jamii haiwezi kukwepa suala la malezi bora kielimu na kimaadili hivyo ni wajibu wa walimu na wenye shule kuhakikisha kuwa watoto wanapata malezi ambayo wazazi wanatarajia ikiwemo kuwepo maadili mema.
Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Novemba 6, 2022 wakati wa Mahafali ya Shule za Kiislamu za Ilala Mkoa wa Dar es Salaam, yaliyofanyika katika uwanja wa Garden uliopo Masjid Taqwah Ilala Bungoni, Dar es Salaam. Mahafali hayo yamejumuisha shule zaidi ya 10 kutoka Kanda ya Mashariki.

"Natoa wito kwa viongozi wa dini kwa kushirikiana na wamiliki wa shule na walimu wasimamie malezi ya vijana,watumie bidii zote kuhakikisha suala la maadili linakuwa muhimu sana na ninalaani vikali sana wale walioruhusu ule mchezo katika shule ile kule Kisarawe na mtu kurekodi video.
"Suala la maadili, wazazi tunakaa na watoto, lakini muda mwingi wapo shuleni wanasoma na muda mwingine tuko kazini muda wa kukaa na watoto ni mchache sana wakiwa shuleni tunarudi jioni,lakini ninaamini wazazi wote wana matamanio ya kuona watoto wanakuwa katika malezi bora na maadili mema, na hata katika imani zetu tunapenda kuona wakielewa imani zetu na waziishi.

"Hatuwezi kukwepa suala la maadili na ndio maana ile clip ya watoto wanacheza kinyume cha maadili ilipoanza kusambaa kwanza viongozi wetu...

"Walisema hii haikubaliki, wazazi walipata taharuki kubwa, walikuwa wananiuliza mimi (Prof.Mkenda) wanaiuliza serikali...suala la maadili liko sehemu zote. Viongozi wa dini kwa pamoja tuwajibike juu ya jambo hili, tusaidiane kwa jambo hili.

"Tunahitaji kuona shule zetu watoto wanapata malezi wanayoyatarajia. Wazazi wanataka kuona watoto wakiwa na malezi bora na Serikali imeweka amri kwamba mtoto aende shule na sisi tunaangalia waraka huo...nitoe wito kwa wenye shule, walimu tunakokwenda tunakuwa wakali zaidi, natoa tahadhari wenye shule za serikali na binafsi, makanisa, kwa wote hao wasimamie maadili na malezi mema ni suala muhimu sana.

Pongezi

"Napongeza kazi kubwa zinazofanywa na walimu, walimu mna kazi ya kuwasaidia wazazi, nisingependa kuona maadili yanashuka na kuporomoka, Serikali itaendelea kusimamia kwa nguvu zote na juhudi zote jambo hili muhimu kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuwa na maadili.
"Lakini zaidi ya hayo kuna mmomonyoko wa kimaadili ambao ni makosa ya jinai, kuna ambao wapo kujaribu kutafuta mahusiano na wanafunzi. Watoto, hukumu inafahamika sisi tutafuatilia, waendesha mashitaka wasimamie mashitaka hayo, sheria ipo, tutasimamia sheria wanaofanya hivi wawajibishwe vikali kukomesha tabia hii.

Msisitizo

"Labda niongeze mambo machache, suala la malezi bora na maadili ni kati ya vitu vinajadiliwa vipo kwenye rasimu ya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, sisi tuliagizwa nendeni mkapitie sera mkabadilishe mitaala kuboresha elimu kuifanya ihakisi mahitaji yetu na sisi tukasema hatutaki kukurupuka.
"Tumeanza kule ambako kazi ilishafanyika, hamuwezi kuamini tunayoyaona kwenye sera yalikuwepo kwenye taarifa ya Makweka iliundwa na Mwalimu Nyerere, tukachukua sera ya 2014 ambayo Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete alikuwa Rais (Rais mstaafu wa Awamu ya Nne) kupitia ile sera tuone ina mapungufu gani, kipengele hadi kipengele humo ndani suala moja kubwa sana limezungumzwa ni suala la maadili na malezi ya vijana wetu na mimi niwahakikishie tunakwenda vizuri sana...

"Nisingependa kuleta taharuki kusema baadhi ya vipengele ambavyo vipo kwenye mapendekezo,Serikali haijaamua bado...lakini mapendekezo yapo ni mapendekezo makubwa na mazuri ambayo yanakwenda kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wetu wa elimu, tunasubiri mchakato wa ndani ya Serikali halafu tutatoa mapendekezo ambayo yanaidhini ya kutamkwa hadharani.

"Na tutayapitia mwakani, mchakato wa kufanya maamuzi ambayo unaotuweka wote katika utekelezaji ambao tutakuwa na ratiba ya awamu ya kutekeleza bila kukurupuka, bila kuharibu au kutoka katika mfumo,"amefafanua Prof.Mkenda.

Pia amesema,suala la maadili liwepo hata katika kusimamia mitihani, kwa kuwa unapowafudisha watoto kuibia mitihani unawafundisha kuwa wezi hapo baadaye.

Kwa wahitimu

"Napenda kutoa pongezi nyingi za dhati kwa wahitimu kumaliza kidato cha nne salama, na pongezi hizi ninazipeleka kwa walimu na wazazi pamoja na walezi.

"Zamani kuna wakati watu walikuwa wakidhani shule ikiitwa Islamic basi itakuwa watu hawafaulu na hawafanyi bidii katika masomo, leo nimeona shule hizi zimefanya vizuri sana na kutunukiwa tuzo. Leo shule zinazoitwa Islamic zinafanya vyema,watoto wanafaulu vyema na kufika mbali zaidi.
"Na hapa mlipofika wahitimu wote hapa sio mwisho ni kituo tu, lakini safari ya elimu lazima iendelee mmejiwekea msingi,jukwaa la kusonga mbele zaidi ninawatakia kila la heri kwenda form six, vyuo vikuu vyuo vya kati na kwenda kuongeza elimu zaidi na kuweza kumudu maisha yenu zaidi, kila la heri vijana na watoto wetu ambao mnahitimu masomo yenu.

"Tafadhali huu usiwe mwisho, kwa shule binafsi, taasisi binafsi tunawahitaji sana, mnachofanya mnasaidia serikali mnapoongeza ubora wa elimu kwa hizi shule binafsi mnasababisha leo hii wazazi hawahitaji tena kuwaweka watoto wao kwenye mabasi kuwapeleka Kenya au Uganda.

"Nadhani imeandikwa kwenye maandiko tafuteni elimu, watu walikuwa wakihangaika kutafuta elimu, lakini sekta binafsi imeisaidia sana Serikali na itakuwa nanyi bega kwa bega kushirikiana na kuwezesha mazingira ya uwekezaji wa elimu kupata wasomi wazuri katika Taifa letu.

"Ninaamini kama Kamisaa niliyepewa dhamana na Rais sikupewa dhamana hii kwa ajili ya Serikali pekee bali pia sekta binafsi zote kwa maendeleo ya nchi yetu nitahakikisha hatuwi vikwazo bali wawezeshaji kwa dini zote katika uwezeshaji,"amesema Prof. Mkenda.
Naye Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Dkt. Musa Salim, amesema katika uislamu suala la elimu limepewa kipaumbele, kwamba tangu mtu anapozaliwa hadi anapofariki anapaswa kuendelea kujifunza hivyo kuwataka wanafunzi hao kuishika elimu.

"Ni jambo la kufurahisha sana Mheshimiwa Waziri (Prof.Adolf Mkenda) kuungana nasi siku hi ya leo. Na Elimu ni uhai wa Waislamu leo tunapowaaga watoto hawa kidato cha nne hatuwaagi kwamba ni safari ya mwisho ya elimu,bali tunawaaga kwa maana ya kuwatia nguvu na kuwahamasisha kwamba safari bado sana.

"Tunawahusia watoto wetu, tunaowaaga leo na watakaoendelea,kushikamana na maadili, elimu haina maana yoyote mbele ya jamii iliyokosa maadili, ninyi ndio taifa la baadaye, nchi hii inawategemea katika suala la madili, endapo taifa litakosa maadili ni sawa na kusema taifa hilo ni mfu.
"Katika Uislamu suala la elimu tunalipa kipaumbele tangu siku mtu anapozaliwa hadi anaingia kaburini kwa maana kwamba unapoingia kwenye ulimwengu huu wewe ni mtu wa kuendelea kujifunza, kuitafuta elimu mpaka unamaliza maisha yako huo ndio mtazamo wa elimu katika Uislamu kwamba Uislamu ni dini ya elimu.

"Tunaona kwamba Mungu alipomuumba Adamu aweze kuuendesha ulimwengu alimpa elimu ndio kitu cha kwanza na utaratibu huo uliendelea kwa manabii wote.

"Na leo watoto wetu ambao mko hapa uwepo wa viongozi wetu hapa, wazazi wenu hapa, wanawaonesha thamani ya elimu, wanawaonesha elimu ndio kila kitu katika maisha endeleeni kujifunza, kusoma na hakuna jambo kubwa linaloambatana na elimu.
"Pia zingatieni maadili, manabii wote walizingatia maadili mpaka kufikia kwa mtume wetu Mohamad. Manabii waliotangulia walifundisha tabia njema na mtume Mohamed alikuja kukamilisha hizo tabia njema. Tunawausia watoto wetu waendelee kushikamana na maadili, taifa linawategemea, elimu bila maadili haina faida yoyote mbele ya watu waliostaarabika. Ninyi ndio viongozi wa baadaye, ninyi ni wazazi wa baadaye nchi hii inawategemea katika suala zima la maadili.

"Taifa lolote lile, heshima na utu wake ni yale maadili na tabia njema. Taifa likikosa maadili ni sawa na taifa mfu tunatarajia kuwaona mkiwa na maadili mema.

"Mimi niseme wazi kwa shule zetu za kiislamu,jamii ya kiislamu kwa nini shule za kiislamu ziongoze katika mmomonyoko wa maadili, ukikamata panya road 10 wenye majina ya kiislamu wapo, ukienda mitaa ya madada poa unakuta majina ya Kiislamu wanakuwa wengi kuliko wenzetu wakati Mtume wetu amekuja kutimiza kufundisha maadili mema.

"Ni lazima tubadilike, ni aibu kwa walimu, mnaitia aibu Serikali yetu mkienda maeneo ya singeli mkitazama jamii wacheza singeli wengi ni watoto wa kiislamu. Kuna baikoko na kadhalika zote hizo ukiangalia majina ya Kiislamu ni mengi kuliko wenzetu, lazima tuhakikishe maadili ndio kila kitu ukiwa huna maadili elimu yako haina maana yoyote ile,"amesema Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Dkt. Musa Salim.

Taarifa ya shule

Wakati huo huo, taarifa ya maendeleo ya shule hizo iliyosomwa kwa niaba na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Al-Haramain amesema, mahafali hayo yamekutanisha wahitimu kutoka shule 11.

"Sherehe hizi zimekutanisha wahitimu wa kidato cha nne kwa mwaka 2022 kutoka shule za sekondari 11, shule hizi zimekuwa na mashirikiano makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo programu za kitaaluma, malezi, mafunzo kwa wafanyakazi na kufanya sherehe za pamoja na huu ni mwaka wa 11 tumekuwa tukifanya sherehe hizi kwa pamoja katika viwanja hivi.
Amesema, shule zote hizo zinaendeshwa kwa kufuata kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

"Katika shule hizi tunafundisha michepuo ya Sayansi, Sanaa na Biashara kauli mbiu yetu ni elimu na malezi bora.

"Programu zinazoendeshwa, ni pamoja na semina elekezi kwa wahitimu, kutafuta nafasi za masomo kwa wahitimu wa kidato cha nne na kidato cha sita katika vyuo vya ualimu Chuo cha Ualimu Kigogo, Chuo cha Afya Ununio, Chuo cha Biashara na Maendeleo ya Jamii Bagamoyo, na vyuo vikuu vya ndani na nje.

"Lakini pia tuna programu za kitaaluma,mapitio,programu za familia, ziara za mafunzo, mijadala ya makundi, mitihani ya kushitukiza na ziara za mafunzo na programu za malezi, midahalo, kutunga na kuwasilisha mada, midahalo na kushiriki makongamano mbalimbali,"amesema Mkuu huyo kwa niaba ya wenzake.

Kuhusu maendeleo ya kitaaluma amesema, shule hizo zimekuwa zikifanya vizuri kutokana na usimamizi madhubuti na makini wa shule hizo.

"Katika sherehe za mahafali ya mwaka 2021, tuliwaaga wanafunzi wahitimu 513 katika mtihani wa kidato cha nne, wanafunzi 501 sawa na asilimia 98 walifaulu kujiunga kidato cha tano na vyuo vya kati.
"Hi ni idadi kubwa sana ya wanafunzi kuhitimu na kufaulisha kwa asilimia 98 ni juhudi kubwa sana zimefanyika hakika. Walimu, walezi na wazazi wanastahili pongezi kubwa sana, kwani idadi hii inakaribia idadi ya wahitimu wa kidato cha nne katika Halmashauri ya Mlele huko mkoani Katavi,"amesema.

Kidato cha Sita

Akizungumzia kuhusiana na matokeo ya kidato cha sita amesema kuwa, "Mwaka huu tuliwaaga wahitimu 182 kutoka shule hizi hizi na matokeo yao wanafunzi wote wamefaulu na kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya juu katika vyuo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi,"amesema.

Amesema changamoto kubwa katika uendeshaji wa shule hizo ni pamoja na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa vijana.

"Tukupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia eneo hili la maadili kwa vitendo kwa kupitisha waraka wa kihistoria wa kusimamia maadili shuleni,"amesema Mkuu huyo kwa niaba ya wenzake.
Naye Ofisa Elimu Wilaya ya Ilala, lhaji Musa Ally, amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imepokea Sh.bilioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ili kuweka mazingira mazuri ya kufundishia katika Mkoa huo.

Wahitimu

Akisoma risala ya wahitimu kwa niaba ya wenzake, mhitimu Mwanaisha amesema kuwa,wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuvuka salama katika kipindi cha miaka minne na wanatarajia kwenda mbali zaidi kimasomo.

"Maisha ni safari kama zilivyo safari zote kuwa na vituo kadhaa. Kituo cha Elimu ni miongoni mwa kituo muhimu na adimu katika safari hii ya maisha. Nasi kama sehemu ya jamii iliyostaarabika tulianza kupiga makasia kwenye bahari ya maarifa tangu dahari.
"Safari ya kutafuta elimu haikuwa nyepesi, tulikutana na kila aina ya mawimbi na misukosuko papa na nyangumi waliohatarisha usalama wa safari na hata uhai wetu, lakini tuliendelea kushikilia.

"Ndugu mgeni rasmi, katika kipindi chote cha miaka minne ya elimu ya sekondari mwaka wetu wa mwisho tunoouhitimsha katika kufanikisha kuona mkakati wa kila mwanafunzi anafikia malengo yake kitaaluma na anaondoka akiwa na hamasa ya kuitumikia jamii, shule zetu ziliamua kuendesha programu mbalimbali za kimasomo kwa kipindi chote, tunaomba Mwenyezi Mungu awalipe mema duniani na kesho ahera.

"Tukiangalia tulikotoka na hapa tulipo wakati huu tunadiriki kusema kwa kipindi chote kimekuwa kifungu ambacho kimetujengea uwezo mkubwa wa kitaaluma, nidhamu maarifa ya kumjua mwenyezi Mungu hamasa ya kuitumikia jamii na kuwasaidia wengine, haya yamewezekana kutokana na masomo ya kiada tuliyokuwa tukifundishwa darasani ambayo ni hivi punde tumetoka kuyafanyia mitihani wiki iliyopita.

"Na mafunzo ya ziada kama kusoma Quran, michezo, ushiriki wa shughuli mbalimbali, usafi na mazingira,programu za kuwatembelea wagonjwa hospitalini pamoja na kuchangia damu kwa wahitaji.
"Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo tumezungumza tuliyoyapata na yapo mengi ambayo tunatamani kuyazungumza na kuyaelezea lakini wakati ni ukuta.

"Ndugu wanafunzi mnaobaki,kama tukitakiwa kuwaachia zawadi ya kudumu katika maisha yenu yote ya shuleni na hata nje ya shule basi hatuna cha ziada na chenye thamani kubwa zaidi ya nidhamu.

"Pia, igeni mazuri tuliyofanikiwa kwayo, mtuwie radhi kwa yale tuliyoteleza na kukosea pia heshimuni walimu wenu kwani wao ndio njia ya kuwasaidia katika mapito yenu.

"...ndugu walimu hakuna maneno nitakayosema yatakayosadifu kiwango cha shukrani zetu kwenu, wengi wametazama siku ya leo kama nafasi ya kuwaona wahitimu wa kidato cha nne na kuanza maandalizi ya mitihani ya kuingia elimu ya Sekondari ya Juu na elimu ya vyuo vikuu.

"Mlitupigania kwa kila hali na nyakati zingine kukesha nasi, lengo ni kuhakikisha tunafikia malengo yetu na hatimaye leo tunahitimu na mnatukabidhi kwa wazazi wetu, sisi ni nani hata tusiseme asante kwa yale yote mliyotufanyia yakatufikisha tulipo.
"...ndugu walimu, mkitafuta mkamilifu hatika dunia hii hamtampata, sisi pia tuliwakwaza na kuwakosea sana, sisi ni nani hata tusiwaombe radhi na msamaha pale tulipowakwaza, tunaamini msamaha wenu kwetu ni muhimu. Pia niwashukuru mno walimu na wazazi wetu, waliotushika mkono kwa safari hii na wewe Mheshimiwa Waziri Prof.Mkenda kwa kuhudhuria hapa,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news