BREAKING NEWS:DCEA yateketeza kilo 584.55 za heroine, cocaine zikiwemo tani mbili za bangi...

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza zaidi ya kilo 584.55 za dawa za kulevya zinazojumuisha kilo 569.25 za heroin na kilo 15.3 za cocaine zikiwemo tani mbili za bangi na mirungi.
Uteketezaji huo umefanyika leo Desemba 21, 2022 katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga (Tanzania Portland Cement Company Limited-TPCC) kilichopo Tegeta Wazo jijini Dar es Salaam.

Zoezi la uteketezaji limekuwa likifanyika katika viwanda vya saruji nchini kwa lengo la kuepuka dawa hizo kuharibu mazingira na kuathiri afya za watu.

Katika hatua nyingine, uteketezaji wa dawa za kulevya huwa unafanyika kwa uwazi mbele ya wadau wote muhimu wanaotambulika kisheria na kushuhudiwa na waandishi wa habari ili kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya wananchi kwamba, baada ya dawa za kulevya kukamatwa hurejeshwa mtaani na kuuzwa tena.

Veronica Matikila akizungumza kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Gerald Kusaya amesema, uteketezaji huu ni wa kawaida na huwa unafanyika baada ya mashauri ya dawa za kulevya kukamilika mahakamani.

"Na dawa hizi ambazo tunaziteketeza leo zinatoka katika mahakama tofauti tofauti Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,lakini tuna baadhi ya dawa zinatoka Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi pamoja na Rushwa."amesema na kuongeza kuwa,

"Kuna dawa ambazo zinatoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani, lakini pia tuna mahakama za Hakimu Mkazi Kinondoni pamoja na Kigamboni na Mahakama ya Wilaya ya Temeke.

"Ninaomba nitoe rai tuendelee kupeleka elimu kwa jamii kwamba dawa za kulevya si nzuri tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha tunaiweka Tanzania kuwa salama na jamii yetu kuwa salama. Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana." amesema.
 
Aidha, uteketezaji huo unaenda sambamba na ule ambao uilifanywa Februari 22, 2022 mkoani Mtwara ambapo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliteketeza jumla ya kilo 250.7 za dawa za kulevya zinazojumuisha kilo 51.7 za heroin.

Sambamba na kilo 199 zenye mchanganyiko wa heroin na cocaine katika kiwanda cha Saruji cha Dangote (Dangote Cement Tanzania) mkoani Mtwara.

Uteketezaji huo ni kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mahakama iliyotolewa katika kesi Namba 2 ya Mwaka 2018 kwenye kikao cha Mahakama Kuu kilichoketi mkoani Lindi mbele ya Jaji Latifa Mansour mwishoni mwa mwezi Oktoba na kumalizika Novemba 5, 2021.

Kesi hiyo iliwahusisha washtakiwa Sano Sidiki na Tukure Ally ambao wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja.

Pia amri nyingine ya uteketezaji ilitolewa Novemba 29, 2021 na Jaji Isaya Arufan kwenye kesi Namba 25 ya mwaka 2019 iliyowahusisha washtakiwa Mohamed Nyamvi na Ahmad Said Mohamed. Katika kesi hiyo washtakiwa hao walihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),zoezi hili limefanyika kwa mujibu wa Kanuni Namba 14 ya Kanuni za Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya za mwaka 2016 za Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015.

Kanuni hiyo inaelekeza kuteketeza dawa za kulevya baada ya shauri kumalizika mahakamani na kwa dawa za kulevya zenye tabia ya kubadilika au kuharibika endapo zitakaa kwa muda mrefu uteketezaji wake unaweza kufanyika kabla au wakati shauri husika linaendelea kusikilizwa mahakamani.

Pia uteketezaji huo ulikuwa ni wa pili kufanyika katika kiwanda cha saruji cha Dangote kwani Juni 15, 2021 ulifanyika uteketezaji mwingine uliojumuisha jumla ya kilo 355 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.

Kwa nini DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news