Croatia yazima ndoto za Brazil nchini Qatar

NA DIRAMAKINI

KIKOSI cha Kocha Zlatko Dalić kimekiondoa kile cha Kocha Tite katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 nchini Qatar kupitia mikwaju ya penalti.

Ni baada ya kupigwa mtanage wa nguvu katika dimba la Jiji la Elimu (City Education) Desemba 9, 2022 huko Qatar ambapo miamba hao wawili walimaliza dakika tisini wakiwa suluhu ya bila kufungana.

Seleção Canarinho (Brazil) ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 106 kupitia kwa Neymar da Silva Santos Júnior (Neymar) akisaidiwa na Lucas Paqueta. Kwa bao hilo, Neymar alifikia rekodi ya mabao 77 ya mshambuliaji mashuhuri wa Brazil, Pele.

Akizungumza baada ya kushindwa kwa Brazil katika robo fainali ya Kombe la Dunia huko Qatar, nyota huyo wa Paris Saint-Germain alipendekeza kwamba anaweza kuondoka.

"Sifungi milango yoyote kwenye timu ya taifa, lakini pia sina uhakika wa asilimia 100 kwamba nitarejea. Nahitaji kufikiria zaidi kuhusu hili, kuhusu ni jambo gani sahihi kwangu na kwa timu ya taifa,"amesema Neymar.

Baadaye, Croatia walisawazisha mechi kwa bao la dakika ya 117 kutoka kwa Bruno Petkovic katikati mwa eneo la hatari, huku Mislav Orsic akisaidia. Muda wa nyongeza uliisha kwa sare ya 1-1.

Hivyo ikaamuliwa ipigwe mikwaju ya penalti. Hatimaye, kupitia mtanage huo wa nguvu, Croatia iliishinda Brazil 4-2 kwa mikwaju ya penalti na kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022.

Kwa matokeo hayo,Croatia itamenyana na Argentina katika hatua inayofuata baada ya kuiondoa Uholanzi kwa mikwaju ya penalti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news