DPP Mwakitalu atembelea Gereza Kuu la Isanga kusikiliza changamoto

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini,DPP Sylvester Mwakitalu ametembelea Gereza Kuu la Isanga jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili Maafisa wa Magereza katika kuwatunza wafungwa pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili mahabusu.
Mkuu wa Gereza Kuu la Isanga, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Ikobela Fumbuka akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu walipotoka kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu Wanawake waliopo katika Gereza Kuu la Isanga ambapo katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka na timu yake walipata nafasi ya kujua changamoto zinazowakabili na kuzichukua kwa lengo la kuzishughulikia. Mahabusu hao wanawake walipongeza juhudi mbalimbali za kazi zinazotekelezwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ambazo wamesema wanazifuatilia kupitia televisheni wanazoangalia wakiwa gerezani hapo.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.Sylvester Mwakitalu akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma wakiwa na Maafisa Magereza walipotembelea Gereza Kuu la Isanga lililopo jijini Dodoma kwa lengo la kuwatembelea Maafisa Magereza, Mahabusu na Wafungwa ili kuwasikiliza na kukiona changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa lengo la kuzitatua ziara hiyo imefanyika jijini Dodoma leo Desemba 5, 2022.
Baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakiongozwa na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi, Bw. Tumaini Kweka wakitoka katika Gereza Kuu la Isanga lililopo jijini Dodoma kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu waliopo katika gereza ili kuwasikiliza na kuhusiana changamoto zinazowakabili. Viongozi hao wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu (hayupo pichani ) katika ziara iliyofanyika leo Desemba 5,2022.

Akizungumza baada ya kutembelea Gereza Kuu la Isanga Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kuwa lengo la kutembelea wafungwa na mahabusu ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa misingi ya sheria na kanuni zake.
‘’Kufanya haya yote ni kuona haki jinai inasimamiwa ipasavyo, lakini tukipata hizi changamoto na kuzisikiliza tunaenda kuzifanyia kazi na kuzishughulikia. Changamoto tulizozipokea ambazo hazipo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka tunazichukua na kuzipeleka ofisi ambazo zinahusika lengo ikiwa ni kuona haki Jinai inasimamiwa ipasavyo,"amesema.

Amesema, miongoni mwa changamoto ambazo amezipokea katika ziara yake ambazo mahabusu wamezieleza ni suala zima la ucheleweshwaji wa kesi na kuchelewa kwa upelelezi ambapo ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kuzishughulikia changamoto hizo kwa kuhakikisha kuwa wameshasajili Hati za Mashtaka Mahakama Kuu ambazo hivi sasa zipo katika mchakato wa kusikilizwa.
‘’Mahabusu wengi ambao nimewasikiliza wamesema kesi zao zimechelewa upelelezi,lakini hali halisi ni kwamba kesi zao hazijachelewa upelelezi kwa kuwa tayari umekamilika na kinachosubiriwa ni utaratibu wa kisheria ambao utawezesha kesi hizo kusikilizwa na Mahakama Kuu,’’amesema.
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka nchini imeanza mwendelezo wa ziara zake katika Magereza mbalimbali nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa wa Magereza, wafungwa pamoja na mahabusu ili kuhakikisha Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa mujibu wa Ibara ya 59B ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Naye Mkuu wa Gereza Kuu la Isanga,Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Ikobela Fumbuka alimshukuru Mkurugenzi wa Mashtaka na uongozi wa Mashtaka Mkoa wa Dodoma kwa ushirikiano mkubwa walionao katika utekelezaji wa majukumu yao na Gereza Kuu la Isanga na kuomba ushirikiano huo uendelee ili kuwezesha utekelezaji wa Haki Jinai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news