KIZIBAO KUTOKA ARABUNI

NA ADELADIUS MAKWEGA

NILIPOKUWA mdogo nilikuwa rafiki yangu mmoja anayefahamika kama Fredrick Mfugale, rafiki yangu huyu anazaliwa na Baba Mhehe na Mama yake ni Mpogoro.

Wahehe wa Iringa Mjini, Kilolo, Ilula, Kalenga hawa ni Wahehe ambao wapo jirani sana na Morogoro na ndiyo maana mahusiano ya Wahehe hao kuoleana na watu wa Morogoro ni jambo la kawaida tangu enzi.

Tulipokuwa wadogo tulimpa jina la utani la Black Fish ndugu huyu ndiyo kusema rafiki yangu huyu wa utotoni ananifahamu vizuri na mimi namfahamu yeye vizuri sana.

Nyumbani kwao ni Mangaya, nakumbuka wakati huo watu waliohamishwa kutoka Azimio, Temeke na Tandika kupisha barabara walipewa viwanja eneo la Mangaya wakahamia hapo, ndipo nikakutana na ndugu yangu huyu kwa mara ya kwanza.

Wao walikuwa wanaishi Tandika Magorofani hamisha hamisha hiyo walipata kiwanja wakajenga nyumba yao huku alikuwa na kaka zake wengi, ugomvi wa watoto ilikuwa ngumu sana kupambana nao maana ukoo mzima ungeweza kukufuata ulipo. Jamaa hawa hawakuwa wagomvi walikuwa watu wema, wakarimu na wanyenyekevu.

Nyumba ya akina Mfugale ilikuwa mkabala na nyumba ya familia moja ya Mzee Bofu, hii familia ya Bofu ilikuwa ni familia inayoisihi maisha ya Uisilamu na kwa hakika ule Uisilamu wao ulionekana katika maisha ya kila siku.

Kwa wale majirani waliyokuwa wakiitazama ile familia kwa mbali na hata kwa karibu hawakuhitaji kuambiwa maisha wanayoishi.

Mzee Bofu alikuwa na wake wawili mkubwa na mdogo, wale kina mama walikuwa wanapendena sana. Sijajaliwa kuona familia kama ile tena yenye upendo mkubwa miongoni mwao na ndiyo maana leo nasimulia.

Chakula anapika mke mkubwa kesho yake anapika mke mdogo na watoto wa familia hii chakula walikula kwa pamoja iwe chai, cha mchana na hata cha jioni, kila siku kwa pamoja mwanakwetu.

Kikipikwa, kinapakuliwa na kutengwa pamoja, familia nzima watoto kiume upande wao na mabinti upande mwingine huku Mzee Bofu anakaa na wake wanakula kwa amani kabisa.

Kama wanakwenda sokoni mara nyingi akina mama hawa walikuwa wanaongozana pamoja mke kubwa na mdogo, suala la mavazi kwa mujibu wa dini yao hilo kwao lilikuwa siyo jambo la kulisimulia maana lilizingatiwa mno.

Wakati tukiwa tunacheza mara nyingi niliona mke mkubwa au mke mdogo anafika kuwaita watoto wote kwa chakula kula pamoja kama nilivyosimulia.

Mzee huyu yeye na wake zake walikuwa Wandengereko wa Rufiji na nyumba yao ilikuwa inapakana na Barabara ya Mangaya na kando yake ulikuwapo Masjidi Sinina, msikiti huu wakati huo ulikuwa unajengwa.

Familia ya Mzee Bofu ndiyo waliokuwa wanasimamia msikiti huo kwa masuala hasa ya kupiga azana. Kando ya Msikiti huo kulikuwa na Madrasat Sinina kwa hiyo watoto Wakiislamu wote walisoma shule hii ya dini hapo hapo.

Ijumaa ikifika wake wa Mzee Bofu kwa pamoja walivalia nguo zao nadhifu wanakwenda kusali Msikiti wa Ijumaa Masjidi Salama(Kizuiani) kwa sababu Masjidi Sinina wakati huo haukuwa Msikiti wa Ijumaa.

Wake wa Mzee Bofu walipendana sana hakuna mtu mtaani hapo ambaye alipata ushahidi wa wakati huo kuwa hawa akina mama mmoja wao amewahi kumpandishia sauti mwenzake na hata watoto na ndugu wa familia hiyo hawakuwa na ushahidi wa tukio kama hilo.

Rafiki yangu Fredrick kwa kuwa nyumba yao ipo jirani na Masjid Sinina tangu wakati unajengwa alikuwa akishuhudia wageni mbalimbali na hata wale waliotokea Arabuni kufuatilia ujenzi wake. Ujenzi uliendelea huku kukiwa na Msikiti mdogo ukitumika kusali na Madrasa iliyokamilika.

Kizibao.

Kuna siku walifika wageni kutoka Arabuni wakakagua ujenzi huo vizuri sana wakazungumza na kutoka nje na kutukuta watoto tunacheza.

Wale Waarabu wakazungumza na watoto wa madrasa huku mkalimani akitafsiri kwa Kiswahili. Ghafla likatolewa robota za nguo nyingi akakabidhiwa Shekhe Waziri (mwalimu wa madrasa) akaambiwa atugawie watoto wote tuliokuwapo hapo.

Kweli watoto wote tulipata nguo hizo mimi na ndugu yangu Fredrick Mfugale tukapata vizibao na nadhani kwa kumbukumbu zangu mimi na Fredrick hivyo vizibao vilikuwa vya kwanza kuvivaa tangu kuzaliwa.

Vizibao hivyo mwanakwetu vilikuwa vizuri sana, vina nakshi ya maua maua yaliyokozwa rangi ya dhahabu kwa mbele na vifungo vyake rangi ya dhahabu.

Siku hiyo kila mtoto pale mtaani waliokuwa wanasoma shule hii ya dini walirudi nyumbani na nguo mpya mkononi. Shekhe Waziri alitambua fika kuwa mimi na Fredrck tumepata nguo hizo na ni Wakristo na siyo wanafunzi wake.

Shekhe Waziri alikuwa anatambua fika sisi tulikuwa tunashinda kando ya Madrasat Sinina tukiwangoja wenzetu tukacheza nao, akituambia njoni msome, tukimjibu sisi Wakristo.

Eneo hilo lilikuwa na miembe mikubwa, palikuwa kivuli cha kutosha na palikuwa na uwazi mkubwa wa kuweza kucheza mpira wa miguu wa magoli madogo au mchezo wa one touch.

Tuliporudi nyumbani na vizibao kutoka Arabuni, vizibao vya gharama, vizibao hivyo hata mashekhe wakubwa pale mtaani hawakuwa navyo, mwanakwetu maswali yalikuwa mengi, haya bwana Fredrick umebadilisha dini?.

“Ahaa jamani hapana wamekuja Waarabu wa Oman wametoa nguo kwa watoto wa Madrasat Sinina wengi, siyo mimi peke yangu.”

Haya wewe unasoma hapo madrasa? “Hapana mimi nilikuwa nawangoja wenzangu tukacheze, ndiyo nikapewa Kizibao, siyo mimi peke yangu na hata mwanakwetu kapewa Kizibao.” Fredrick Mfugale mtumikiaji wa kanisani alitoa majibu hayo.Haya haya muite na huyu mwanakwetu haraka.

Nikatafutwa kwenda kwa akina Fredrick kutoa maelezo ya kina na mama yake Fredrick ambaye alikuwa mwalimu mahiri wa Darasa la Kwanza Shule ya Msingi Gerezani Ilala, Dar es Salaam wakati huo nikamueleza kuwa, “Hatujabadilisha dini, sisi walitukuta uwanjani tu na huo mgao tukapata.”

Mke wa Shekhe Waziri alipoulizwa alieleza kwa kina kilichotokea kwa hiyo hivyo vizibao vyenye nakshi ndiyo tukapata vibali vya kuvivaa.

“Kizibao kilishawekwa mezani kikimngoja Mzee Mfugale, Huyu mama Mwalimu wa Darasa la Kwanza alipotoka kwa Mke wa Shekhe Waziri ndipo nikakabidhiwa kizibao changu.” Alisimulia Fredrick Mfugale.

Sasa hata Jumapili tulivivaa na kuingia navyo kanisani vilikuwa vigumu sana, havipauki wala kuchujuka rangi zake.

Tulipokuwa tunavivaa kanisani tukitumikia ukivaa kanzu za waministranti Kizibao kilikuwa kinamulikamulika yale maua yake ya rangi ya dhahabu kwa hiyo kinavuliwa kinabaki Sakristia unavaa kanzu unatumikia misa ikiisha unakiva Kizibao chako unarudi zako nyumbani.

Sasa wakati tunarudi nyumbani tukawa tunazungumza na Fredrick, huko pale mbele umevaa kanzi yako vizuri alafu Kizibao kinamulika mulika.waamini wanaimba, “Uninyunyizie maji Ee Bwana, Ee Bwana unioshe nitakase Ee Bwana unioshe ni nitakase.”

Waamini wanaweza kushangazwa huyu mmnistranti mbona anawakawaka kwa hiyo kukivua Kizibao hicho kabla ya Misa lilikuwa jambo la muhimu sana.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Post a Comment

0 Comments