Kuwait yakataa mapendekezo ya mshauri wa Kimataifa kuhusu kubinafsisha shule za umma

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Kuwait kupitia Wizara ya Elimu imekataa mapendekezo ya mshauri wa Kimataifa yaliyoangazia mahitaji ya miaka 50 ijayo kwa ajili ya kujenga programu za kisayansi kwa shule na elimu nchini humo.

Kwa mujibu wa Kuwait Times, vyanzo vya ndani vilieleza kuwa, mapendekezo hayo yalihusisha pia ubinafsishaji wa shule zote nchini Kuwait, chini ya usimamizi wa serikali kwa kuzingatia mpangilio, udhibiti, ufaulu na uwajibikaji.

Vyanzo hivyo vimeieleza Kuwait Times kuwa, Serikali imeyakataa mapendekezo hayo kwa sababu haiamini kwamba yanalingana na mahitaji ya jamii ya Kuwait na kuna tuhuma kwamba yanaweza kuwa kinyume cha katiba ya Taifa hilo.

"Mapendekezo kutoka kwa timu yalionesha wazo hili linatekelezwa katika nchi nyingi, na baadhi ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC) tayari zimeanza taratibu za kufikia lengo hili," vyanzo vilisema, vikisema kuwa inaweza kuokoa fedha nyingi za Kuwait zinazotumiwa katika elimu bila kufikia malengo, matokeo hafifu huku matokeo ya elimu katika shule binafsi yakiwa bora zaidi ikilinganishwa na shule za umma.

“Bajeti ya Wizara ya Elimu imezidi Kuwaiti Dinar (KD) bilioni mbili na inatarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka michache ijayo.

"Hata hivyo, ufaulu kwa ujumla ni dhaifu, kwani mitaala ya elimu haikidhi viwango vya siku zijazo. Zaidi ya hayo, taasisi za elimu ya juu nchini Kuwait zinathibitisha kuwa hazipokei wahitimu wa shule ya upili katika kiwango kinachohitajika,” vyanzo vilieleza.

Vyanzo hivyo viliongeza kuwa, Wizara ya Elimu haikukubali wazo la ubinafsishaji wa shule, kwani elimu bila malipo ni sehemu ya Katiba ya Kuwait, na serikali haina mfumo wazi wa jinsi ya kukabiliana na mabadiliko yoyote.

Kwa mujibu wa ripoti ya Elimu ya GCC ya Kituo cha Kifedha cha Kuwait (Markaz) ya hivi karibuni, shule binafsi ukanda huo wa Asia zimekuwa zikitoa elimu bora, lakini, imekuwa ghali zaidi jambo ambalo limechangia wazazi wengi kukata tamaa.

Wengi wanaamini kuboreshwa kwa elimu kupitia shule za umma ambazo mara nyingi zimekuwa zikitoa elimu bila malipo ndiyo msingi bora zaidi na kimbilio kwa familia nyingi ambazo zinashauku ya kusomesha watoto wao ingawa kipato chao ni cha kawaida.(Kuwait Times/Markaz)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news