UPANDAJI WA MITI KOTE TANZANIA, MKABALA SHIRIKISHI-1

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

MAKALA haya nayaandika nikiwa na dhamira ya kuhamasisha upandaji wa miti katika mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji na vitongoji vyote vya Tanzania katika kipindi hiki cha mvua.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipanda mti kuashiria kuzindua rasmi kampeni ya kitaifa ya upandaji miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji, zoezi lililofanyika katika chanzo cha maji cha Nzovwe 1 Kata ya Mwakibete jijini Mbeya tarehe 16 Novemba 2022. (Picha na OMR).

Nimefanya safari kutoka Dar es Salaam na kupita katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma na Manyara na kote mvua inanyesha.

Hivyo kufuatia mvua hizi na hali ya ukame na upunguvu wa maji tuliopitia katika miezi kadhaa ni dhahiri kama jamii ni wajibu wetu kupanda miti ili kulinda na kuhifadhi mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

Kimsingi, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya na inaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa njia na mbinu mbalimbali.

Wizara ya Muungano na Mazingira chini ya ofisi ya Makamu wa Rais ndiyo kinara katika juhudi na jitihada hizo bila kusahau wadau mbalimbali wananchi wakiwa ndiyo washika dau wakubwa.

Katika kipindi hiki cha mvua ni vema tukahakikisha tunapanda miti ya kutosha na miti hiyo iwe ni ile inayoendana na mandhari husika ambapo bila shaka wataalamu wetu hutoa elimu hiyo.

Upandaji huu wa miti utakuwa wa tija zaidi ikiwa tutaufanya kuwa ni shirikishi zaidi kama azma ya serikali inavyoelekeza. Kwa mnasaba huo, napendekeza ushirikishwaji katika upandaji miti kama ifuatavyo:

Mosi Ngazi ya Familia

Hakika familia ndiyo msingi wa jamii yoyote ile iwayo na kama kila kitu kizuri kikianzia katika ngazi ya familia basi huenea katika jamii nzima.

Kwa kulitambua hilo,Serikali imeelekeza kila familia kupanda miti angalau mitatu na kuisimamia vizuri kuhakikisha inakuwa.

Mbinu au utaratibu huu ni mzuri sana na ni vema viongozi wetu wa ngazi za vijiji, mitaa, vitongoji na kata wakasaidia katika kulisukuma vizuri jambo hili kwa kutoa elimu na ufuatiliaji.

Kutoa elimu kwa jamii kutasaidia kuufikisha vizuri ujumbe huu wa kila familia kupanda miti mitatu na kupata muitikio mzuri. Binafsi nipo tayari kuendelea kutoa elimu hiyo kwa njia mbalimbali ikiwemo hii ya kuandika makala.

Upandaji miti katika ngazi ya familia utasaidia kujenga utamaduni wa wanajamii wote wakiwemo watoto ambao ndiyo taifa la leo na kesho na pindi watakapokuwa watu wazima na kuchukuwa majukumu katika jamii basi wataendeleza utamaduni huu mzuri wa kupanda miti.

Miti ndiyo chanzo kikubwa cha maji na pia ndiyo muhimili muhimu katika kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.

Maji yanapokosekana tunapatwa na njaa, umeme kukosekana, uchumi kupunguwa kasi, biashara kupunguwa, bidhaa kupanda bei na ajira pia kupungua kutaja kwa uchache.

Upandaji wa miti unapokuwa umeimarika katika ngazi ya familia basi utakuwa endelevu na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yataepukika kwa kiasi kikubwa.

Pili Ngazi ya Vitongoji,Mitaa na Vijiji

Hizi ni ngazi muhimu sana katika kuhakikisha upandaji wa miti unafanyika katika kila kaya, lakini pia kusimamia, kulinda na kuhifadhi misitu, na mapori tengefu yaliyopo katika maeneo yao ya utawala.

Kama nilivyosema hapo awali viongozi wetu katika ngazi hizi ndiyo mabalozi wa serikali wa kuhakikisha elimu juu ya upandaji miti katika familia inatolewa kwa wananchi ili waendelee kufahamu faida za kupanda miti na hasara za kukata miti hovyo bila utaratibu na mipango endelevu.

Kazi hii ya kutoa elimu wanaweza kuifanya kwa kushirikiana na taasisi ama asasi mbalimbali ambazo zinapatikana katika maeneo yao.

Kwa mfano, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinapatikana katika mikoa yote ya Tanzania Bara na vituo vya uratibu Unguja, Pemba, Kahama na Tunduru. Chuo kina wataalamu ambao wanaweza kushirikiana na viongozi hao wa ngazi tajwa katika kutoa elimu na ushauri wa masuala ya mazingira ikiwemo upandaji wa miti.

Chuo hiki ni mfano mzuri wa upandaji miti kimetenga kila Aprili Mosi ya kila mwaka kuwa ni siku ya kupanda miti katika maeneo yote ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania nchi nzima.

Sambamba na kupanda miti katika maeneo ya chuo pia hupandwa katika maeneo mengine kama katika shule za msingi na sekondari.

Tatu Vyombo vya Habari

Katika suala la upandaji wa miti vyombo vya habari vina nafasi na mchango mkubwa sana. Vyombo vya habari kama redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii viandae vipindi mahususi vya kuhamasisha jamii katika upandaji wa miti katika kipindi hiki cha mvua.

Vipindi juu ya kutunza miti hiyo pia navyo viwepo ili miti itakayopandwa itunzwe vizuri. Tunafahamu kwamba, vyombo vya habari vimekuwa vikifanya jambo hili ila kwa sasa tunaomba vipindi vya hamasa ya kupanda miti viwe vingi zaidi kwa sababu ndiyo msimu wenyewe wa mvua umeanza.

Nne:Ngazi ya Taasisi za Umma, Binafsi na Vyombo vya Dini


Taasisi mbalimbali zina nafasi na mchango maridhawa katika upandaji wa miti. Taasisi zinaweza kutoa hamasa kwa wadau wake wakiwemo wafanyakazi na wateja juu ya upandaji wa miti.

Pia, taasisi zinaweza kutenga bajeti maalumu ya kuwezesha zoezi la upandaji miti kila mwaka. Bajeti hiyo inaweza kusaidia taasisi kupanda miti na kuitunza na wakati mwingine bajeti hiyo inaweza kusaidia vikundi vya mazingira vilivyo jirani na taasisi husika.

Mbali na hayo, katika shule zetu za msingi, sekondari, vyuo vikuu na vyuo vya kati vikiwemo vya VETA kila mwanafunzi kuhakikisha anakuwa na mti wake ambao atahakikisha unamwagiliwa maji na unatunzwa vizuri mpaka unakuwa.

Hili likifanyika kikamilifu, nchi yetu itakuwa na miti mingi ndani ya kipindi kifupi na dhana au utamaduni wa kupanda na kutunza miti itaendelea kuenea katika mioyo ya Watanzania.Ninafahamu jambo hili lipo basi kwa sasa tulipatie msukumo mpya wenye nguvu na kasi zaidi.

Vyombo vya dini vitumie sehemu ya mafundisho, hotuba na mahubiri kuwataka waumini wao na wananchi kwa jumla kupanda miti.

Hili lifanyike kila wanapokusanyika katika ibada kama zile za mwisho wa wiki za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ambapo waumini wengi huhudhuria ibada.

Mbinu hii nayo ni nzuri kwani itasaidia katika kuwazindua na kuwafunguwa zaidi wananchi kumakinikia suala la upandaji miti na kulipatia uzito stahiki.

Si hivyo tu bali pia, vyombo na taasisi za dini zihakikishe zinapanda miti katika maeneo yao yote ili kuwa kiigizo chema kwa waumini wanaoaswa na kuombwa kupanda miti.

Hitimisho

Mazingira mazuri ni uhai wa taifa na hivyo ni vema kila mwanajamii kuhakikisha anapanda miti ili kuwa na mazingira endelevu na kwa maana hiyo kuwa na uhai katika maisha ya jamii.

Katika makala haya nimewasilisha nukta chache za namna jamii yetu inavyoweza kushiriki katika upandaji wa miti hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazonyesha katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

Fuatilia sehemu ya pili ambapo nitaendelea kubainisha na kueleza juu ya ushirikishwaji wa wananchi katika upandaji wa miti.

Maelezo katika makala haya yanaonesha na kuthibitisha kwamba mbinu shirikishi za wananchi katika kupanda miti zilizotajwa kwa pamoja zitakapotumika zitaweza kuongeza kasi ya upandaji wa miti katika nchi yetu ya Tanzania.

_Mfululizo_ _wa_ _Insha_ _na_ _Makala_ _za_ _Maendeleo_ _kutoka_ _kwa_:


MWANDISHI

Dkt.Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Babati-Manyara
26/12/2022

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news