Louis van Gaal:Hakuna namna lazima Uholanzi tuwafunge Marekani leo

NA DIRAMAKINI

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Uholanzi,Louis van Gaal amesema, timu yake haitaidharau Marekani watakapokutana katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia leo.

Louis van Gaal ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari Desemba 2, 2022 jijini Doha nchini Qatar, mkutano ambao ulikuwa na maswali mengi kuhusu mustakabali wake kama ilivyokuwa kuhusu pambano la mtoano.

Amewataja wapinzani wao wa leo kuwa wenye nguvu sana, huku wanahabari kutoka nchi jirani ya Ubelgiji wakimtaka kocha huyo mpambanaji kuchukua mikoba ya timu yao ya taifa baada ya Roberto Martinez kujiuzulu kufuatia Ubelgiji kushindwa Alhamisi.

"Lazima umshawishi mke wangu," aliwaambia Wabelgiji, jambo ambalo lilizua swali la kufuatilia kutoka kwa mwandishi. "Sidhani hivyo, lakini unapaswa kuweka chaguzi zako wazi," Van Gaal alitania, kabla ya kurejea kwenye kilichomkutanisha na wanahabari hao.

"Marekani imedhihirisha kuwa ina timu bora, ningesema moja ya timu bora, timu iliyopangwa vizuri (lakini) sio kitu ambacho hatuwezi kushinda," Van Gaal aliongeza kabla ya mchezo huo.

Uholanzi na Marekani zitaumana leo Desemba 3, 2022 katika dimba la Taifa (Khalifa International Stadium) lililopo jijini Doha, Qatar.

"Marekani ambao ni kikosi chenye nguvu sana, wana wachezaji wenye nguvu za kimwili na hilo ni gumu kwa mpinzani yeyote, na unaweza kujua kutokana na matokeo yao, lakini tutafanya kila tuwezalo kushinda na kuishinda Marekani, ndivyo hivyo."

Waholanzi hao walifanikiwa kushinda Kundi A huku Senegal wakijiunga nao katika hatua ya 16 bora kama washindi wa pili, lakini kikosi cha Van Gaal kimeshindwa kutamba hadi sasa, isipokuwa fowadi Cody Gakpo, aliyefunga mabao matatu katika mechi tatu za kundi hilo.

Kama vile kocha wa Uholanzi amefanya katika muda wote wa michuano hiyo, Van Gaal alikataa ukosoaji wa uchezaji wa timu yake.

“Kimsingi niseme tulianza tukiwa na kikosi chenye watu wengi ambao hawakuwa fiti, wote wamepewa nafasi ya kucheza na tulipitia hatua ya makundi kiulaini,” alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news