Machawa wamchefua Askofu Dkt.Maboya, asema watu wafanye kazi

NA DIRAMAKINI

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG), Mtume Dkt.Dunstan Maboya amewataka Watanzania wafanye kazi, kwani njaa ni mbaya ndio maana inasababisha uwepo wa watu ambao wanajiita machawa.

Chawa ni jina mbadala la mpambe ambaye ni mtu anayekuwa na kiongozi au mwenye uwezo muda wote na anazidiwa kipato, hivyo kuandamana na muhusika kuna manufaa anayoyapata hususani kiuchumi.

Dkt.Maboya ameyasema hayo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam akiwa ametoka nje ya nchi.

“Njaa ni mbaya, njaa inaweza kusababisha wambeya wanakuwa wengi hapa mjini, mtu anapeleka news (habari) za uongo uongo tu anakuwa chawa ili alishwe, sasa vitu kama hivyo sio vizuri na utakuta wengi wanaokuwa machawa hawana kitu kwa sababu ni wavivu na uvivu ni dhambi.

“Ningependa Watanzania tusiwe wavivu, kuna vitu vitatu muhimu lazima upate kibali mbele za Mungu, Serikali na mbele za wazazi,”amesema Dkt.Maboya.

Mtume Dkt.Maboya akizungumzia ziara yake nje ya nchi ikiwemo katika nchi ya Sudan amesema, “Mfano katika nchi ya Sudan utakuta Mungu amewabariki wana mashamba mengi sana na mto Nile ni mkubwa mno, lakini wameshindwa kulima kwa sababu ya vita, hivyo tuombe Mungu vita visitokee katika nchi yetu,"amesema.

Kwa upande wake Mchungaji Christina Mbelwa wa Kanisa la Valley of Life amesema, “Kama nchi nyingine zimeona mazuri aliyonayo na akaenda kuwafundisha ina maana na sisi kwetu tunatakiwa tufunguke macho tuweze kuwatumia watu hao ambao Mungu ametupatia kwenye nchi yetu, wataweza kutuelekeza, kutufundisha na kutusaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine,”amesema Mchungaji Mbelwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news