MASOMO MAKUU QATAR-1:Japo walikuja juu, Qatar waliwakata

NA LWAGA MWAMBANDE

KILA mmoja ukimtajia Taifa la Qatar inaweza kuwa rahisi kukupa jibu kuwa, ni miongoni mwa mataifa machache Duniani ambayo yameandaa Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 kwa ufanisi.

Hilo ni kweli, lakini Qatar ni nchi ya peninsula ya Kiarabu ambayo eneo lake linajumuisha jangwa kame na ufuo mrefu wa Ghuba ya Uajemi ya fukwe zilizopangika kwa namna yake.

Pia kwenye Pwani kuna mji mkuu, Doha unaojulikana kwa majumba yake marefu na usanifu mwingine wa kisasa uliochochewa na muundo wa kale wa Kiislamu, kama vile Jumba la Makumbusho la Chokaa la Sanaa ya Kiislamu. Jumba la makumbusho liko kwenye eneo la maji la Corniche.

Katika mji mkuu wa Doha ambapo ndipo shughuli ya siku 28 za Kombe la Dunia zilifanyikia, kila mmoja wetu amejifunza na kuburudika kwa namna yake.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, kwake kupitia yaliyojiri katika kombe hilo amejifunza mambo mengi ambayo yanazidi kumpa nguvu ya kuipa heshima zaidi Qatar, endelea;

1.Kuna masomo makuu, Qatar tumeyapata,
Machache nayanukuu, yale nimeyaokota,
Fainali hizi kuu, kwetu zimeshayaleta,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

2.Moja na la kwanza kuu, walilolifanya Qatar,
Ni heshima kwa mkuu, Mungu wetu huyu Tata,
Memwinua sana juu, katikati ya utata,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

3.Kukataa sikukuu, hao wanapitapita,
Usodoma uwe juu, laana tuzidi pata,
Japo walikuja juu, Qatar waliwakata,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

4.Upinde upande juu, chansi hawakupata,
Heshima kwa Mungu juu, ambayo ameipata,
Mbele ya watu wakuu, wamedhihirisha Qatar,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

5.Kwangu ubingwa mkuu, wote unakwenda Qatar
umweheshimisha mkuu, Mungu heshima kapata,
Unajisi wa majuu, huko hawajauleta,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

6.Kuna maneno makuu, vitabuni tunapata,
Tumheshimu mkuu, vingine vyote kupita,
Hiyo ni amri kuu, wameitimiza Qatar,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

7.Kumkubali mkuu, heshima akaipata,
Hilo kwetu jambo kuu, Imani zetu lavuta,
Tutazidi linukuu, kote tutakakopita,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

8.Rais wa FIFA juu, yake yale tulipata,
Presha likuwa juu, ya kwamba awe mtata,
Lakini twamnukuu, ameiheshimu Qatar,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

9.Kawaudhi wa majuu, hiyo imekwishapita,
Tamaduni zetu kuu, Imani ndiyo mafuta,
Kuenzi Mungu mkuu, kwake heri tunapata,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

10.Na kwa hili jambo kuu, kibali kiende Qatar,
Mengine ya juu juu, msamaha weze pata,
Wabebwe na hili kuu, heshima Mungu kapata,
Katikati kwenye mechi, makubwa tumejifunza.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news