Pele atikisa katika Kombe la Dunia Qatar 2022

NA DIRAMAKINI

TAIFA mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022, Qatar limeonesha kumuunga mkono gwiji wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento (Pele) na kuwasha katika majengo yake ujumbe wa "Pona Haraka" kwa nguli huyo wa soka wa Brazil.
Picha iliyopigwa Desemba 3, 2022 jijini Doha,Qatar wakati wa michuano ya Kombe la Dunia la Qatar 2022, ikionesha mnara wa Mwenge wa Doha unaojulikana pia kama Aspire Tower, ukiwashwa na skrini inayoonyesha nyota wa Brazil, Pele huku pia ukisomeka ujumbe wa kumtakia afya njema mchezaji huyo wa zamani wa soka wa Brazil ambaye anakabiliwa na changamoto za kiafya wakati akiendelea na matibabu hospitalini huko Sao Paulo, Brazil. (Picha na Nelson Almeida/AFP).

Uwanja wa Lusail mjini Doha, utakaoandaa fainali ya Kombe la Dunia Desemba 18,2022 na Aspire Tower karibu na Uwanja wa Khalifa, ulipambwa kwa picha za Pele akiwa katika jezi yake maarufu namba 10.

Kwenye uwanja wa Corniche, sehemu ya mbele ya bahari ya mji mkuu wa Qatar, ndege nyingi zisizo na rubani zilichora jezi ya Brazil yenye jina la Pele na namba 10 mgongoni.

Pele alilazwa hospitalini mjini Sao Paulo mapema wiki hii kwa kile madaktari walisema ni "kutathminiwa upya" kwa tiba ya kemikali ambayo amekuwa akifanyiwa tangu upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye utumbo mpana Septemba, mwaka jana.

Wachezaji nchini Qatar wameelezea hisia zao kuhusu afya ya mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia, ambaye sasa ana umri wa miaka 82.

Mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe siku ya Jumamosi alitweet kuwa, "Ninamuombea Mfalme." Akimaanisha anamuombea Pele ambaye ni mfalme na gwiji wa soka duniani.

Naye nahodha wa Uingereza, Harry Kane alitoa salamu zake kwa Pele katika mkutano na waandishi wa habari mjini hapa wakati akizungumzia kuhusu mtanange kati ya Taifa lake dhidi ya Senegal.

"Tunatuma salamu zetu za heri kwake na ni wazi familia yake yote pia," alisema Kane. "Yeye ni nguzo miongoni mwa mchezo wetu na mwanasoka wa kipekee na mtu wa ajabu. Tunamtakia heri."

Pele ameingia kwenye Instagram yake na kuwashukuru watu wenye mapenzi mema kwa onesho lao la kumuunga mkono.

"Siku zote ni vyema kupokea jumbe chanya kama hizi. Asante kwa Qatar kwa heshima hii, na kwa kila mtu anayenitumia jumbe nzuri,"ameeleza Pele.

Pele ambaye alizaliwa Oktoba 23,1940 ni miongoni mwa magwiji wa soka duniani kutokea nchini Brazil ambaye anatajwa na wengi kuwa mchezaji bora zaidi wa wakati wote.

Gwiji huyo, alicheza kama mshambuliaji wa kati. Aliisaidia Taifa lake la Amerika Kusini,Brazil kutwaa kombe la Dunia 1958, 1962 na baadaye tena mwaka 1970.

Pia gwiji huyo aliweka rekodi mwaka 1958 ya kuwa mchezaji mdogo kuliko wote duniani kucheza katika fainali ya kombe la dunia alipocheza akiwa na umri wa miaka 17.

Pele, alivuma sana katika miaka ya 1970 duniani kote. Mwaka 1999 alichaguliwa na Shirikisho la Soka Duniani kuwa mchezaji bora wa karne.

Kwa mujibu wa FIFA, Pele alikuwa mfungaji bora wa muda wote kwa kufunga magoli 1281 kati ya mechi 1363. Ana wastani wa goli moja kwa kila mechi katika uchezaji wake wote. Katika kipindi cha uchezaji wake alikuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news